Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii lakini nitakuwa na mambo ya ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais ambaye ameondoa tatizo la miaka 20 kwenye Msitu wa Makere Kusini, maarufu kama Kagera Nkanda. Tatizo limekwisha, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais alikuja na ameliondoa tatizo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoomba Mheshimiwa Waziri mipaka mipya imewekwa, eneo ambalo Mheshimiwa Rais amelitoa kwa wakulima wa Wilaya ya Kasulu linajulikana, tunaomba askari wa wanyamapori waheshimu mipaka iliyowekwa sasa. Eneo lile hatukupewa na Wizara kwa sababu Wizara kwa miaka 20 imeshindwa, tumepewa na Mheshimiwa Rais. Kwa kweli, alipotutembelea nilimnong’oneza jambo hilo akalielewa. Sifa ya Mzee yule jambo akilielewa na akaliamini anatoa uamuzi. Kwa hiyo, tunaomba sana mipaka mipya sasa iheshimiwe ili Kagera Nkanda watu waishi kwa amani na wafanye shughuli zao za kilimo bila usumbufu wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo la shukrani kwa Mheshimiwa Rais, nina jambo ningetaka AG anisikilize. Hili jambo nataka nili-address kwa AG kwa sababu ndiyo Mshauri wa Mambo ya Sheria katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba hizi, hii ya Wizara na hotuba ya Kamati ni mbingu na ardhi, ni vitu viwili tofauti. Wenzetu hawa wamekuja na mambo mahsusi ambayo ni lazima yafanyike kuboresha tasnia ya uhifadhi na utalii lakini hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hakuna mkakati mahsusi unaoonekana humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hilo kwa AG na more serious ukurasa wa 16 na 17, hawa Wabunge wenzetu 24 ambao wamechambua bajeti hii, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa AG, wameeleza vifungu ambavyo vimekosewa kisheria na matamko ambayo yanaathiri tasnia ya uwindaji.
Labda ni-declare interest, mwaka 2013 nilikuwa kwenye Kamati ya Kumshauri Waziri juu ya Ugawaji wa Vitalu hivi, nimetembea mapori yote najua kinachoendelea huko na tulitoa mapendekezo. Sasa Mheshimiwa AG nakuja, sheria zimevunjwa, hivi sheria ikivunjwa maana yake ni nini? Ndiyo hoja yangu. Mheshimiwa Mwenyekiti na wewe ni Mwanasheria utanisadia, sheria imevunjwa maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wabunge 24 wanasema, labda nisome, ‘Kamati inaitaka Serikali kurejesha utulivu katika tasnia hii ya uwindaji na kuondoa au kuhuisha barua yake ya ugawaji wa vitalu ya tarehe 16 Januari, 2017’. Hii tasnia tunaiua wenyewe kwa sababu Waziri wewe huna powers za kukiuka sheria. Nashangaa Wizara hii ina watu makini sana, una Katibu Mkuu makini sana, vipi mnavunja sheria? Hawa wawekezaji kwenye tasnia ya uwindaji wa kitaalii mnawauwa, mnawa-frustrate, hawafanyi kazi na wamewekeza fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli on a serious note napenda AG kwa kweli alieleze Bunge hili sheria ikikiukwa katika misingi kama hii na Wabunge 24 hawa wanasema aaah, hii haiko sawa. Maana yake ni wawili au Mheshimiwa Waziri aje hapa aseme jamani ile barua ya tarehe 16 nakwenda kuifuta kwa sababu haiko kisheria ili wawekezaji wale wawe na amani katika tasnia ya uwindaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa tu, tasnia hii ya uwindaji ni muhimu sana na inatuingizia fedha nyingi sana. Nimeshuhudia jambo hili tena wakati huo tunafanya kazi na TRA hata baadhi ya watu waliokuwa hawalipi kodi tulishauri sana watu wale wafuatiliwe walipe kodi. Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana, alisema Mheshimiwa Msigwa asubuhi umeanza kutulia, muendelee kutulia, tasnia hii ni muhimu sana sana, sana. Hawa wawekezaji hawa wana maslahi ya kulinda na tunawahitaji tupate fedha. Ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri jambo hilo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo la uvunjaji wa sheria na unaweza ukaiona katika ukurasa 16 na 17 wa kitabu cha Kamati halafu Wizara kwenye hotuba ukurasa wa 18. Tena Mheshimiwa Waziri mwenye anakiri anasema kwa kutambua umuhimu wa tasnia hii ya uwindaji wa kitalii na kukuza uchumi wa nchi yetu, Wizara kupitia TAWA inaendelea kurekebisha muundo na utaratibu wa kugawa vitalu vya uwindaji. Hatua hiyo inahitaji mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori ambayo inafanyiwa kazi, Waziri mwenyewe amekiri hapa bado inafanyiwa kazi. Sasa mnatoaje matamko ambayo yanawa-frustrate wawekezaji? Hiyo pesa ya kigeni tunapata wapi? Ni mambo ambayo lazima tuyaangalie haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda nilizungumzie ni promotion drive ya Mbuga za Gombe, Mahale na Katavi kwa sababu ya corridor ile moja. Mheshimiwa Waziri humu sioni kabisa hata sentensi moja inazungumzia habari ya promotion drive ya Gombe na Mahale. Nimeona Katavi kidogo lakini Gombe na Mahale sioni. Mbuga hizi ni unique sana, ziko kwenye mwambao wa Ziwa Tanzanganyika. Ni mbuga ambazo ni tofauti na Serengeti na Ngorongoro, ni unique. Ningeshauri strongly Mheshimiwa Waziri na wataalam muwe na mkakati mahsusi wa corridor ile ya Katavi, Mahale na Gombe National Parks, ni utalii mzuri sana. Hata wataalam wengi wa sayansi wanakwenda sana kwenye maeneo yale kwa ajili ya scientific research ambazo nazo zinatuingizia fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingineambalo napenda niliseme, uhifadhi unahitaji mito. Ukizungumza Ruaha National Parks unazungumzia Mto Ruaha, ukizungumzia Gombe, Mahale, Kigosi, Moyowosi unazungumzia Mto Malagarasi. Ukizungumzia habari ya Kilombero, Serengeti unazungumzia Grumeti, ukizungumza habari ya Ugara Game Controlled Area unazungumzia Mto Ugara. Nashauri, Serikali ni moja, Wizara mkae pamoja Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Maji na Waziri wa Mazingira, mje na strategy ya pamoja kulinda mito hii. Hii mito Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla isipokuwepo hakuna uhifadhi.
Hawa wanyama wote watatoweka. Naomba hilo mlichukue muweze kuwa na strategy ya pamoja kuweza kulinda mito mikubwa hii ambayo hakika ndiyo inalisha kwenye National Parks zetu, Games Controlled Areas na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ushauri tulioutoa mwaka 2013 ambao unazungumzia mapori ambayo yamekosa sifa ya uhifadhi kupewa wafugaji. Hilo tumelizungumza tangu 2013 leo ni 2018 na mapori hayo yapo mengi. Kwa mfano, open area ya Wembere mnaiweka ya kazi gani wapeni wafugaji wafugie mifugo yao pale. Ile hifadhi Mheshimiwa Waziri imeshapoteza sifa ya uhifadhi tangu mwaka 2013. Yako maeneo mengi huko Ruafi katika Mkoa wa Katavi hata maeneo ya Kigosi Moyowosi ukiacha Njingwe 1 na Njingwe II maeneo mengine yote yameshakosa sifa za uhifadhi ni vema maeneo hayo wapewe wafugaji wayatumie kwa sheria ambazo zitakuwa zimewekwa ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni suala la Ngorongoro. Hivi Ngorongoro tunaitaka kweli Mheshimiwa Waziri. Huu mgogoro wa Loliondo hauishi. Nilimsikia Mbunge wa Arusha anazungumzia habari ya kumalizika mgogoro wa Loliondo haujaisha ule bado unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo kubwa kabisa kuliko yote ni co-existence ya wafugaji wa Kimasai wale na wildlife, hivi vitu haviwezi kwenda pamoja mazingira yamebadilika. Zamani zile walikuwa Wamasai 8,000 tu leo hii Loliondo wako Wamasai maelfu kwa maelfu. Ile ikolojia haiwezi ku-sustain tena, tutapoteza Ngorongoro kama hatua mahsusi hazitachukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekwenda Ngorongoro pale …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)