Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii. Kabla sijaanza kuchangia hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia sote fursa hii ya kuwepo katika jengo lako hili Tukufu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, pia baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, kama ilivyo kawaida, napenda niwashukuru wazazi wangu wawili, Mzee Kijaji na Mke wake Mama Aziza Abdallah, nawashukuru sana kwa malezi yao kwangu yaliyonifikisha hapa nilipo siku hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa hili kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo alizunguka Taifa hili kuinadi ilani hiyo. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, hakika yuko makini anatekeleza kile ambacho aliwaahidi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza pia, Mheshimiwa Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, mama wa mfano kwa Taifa la Tanzania. Amekuwa ni mama yetu wa mfano, sisi wanawake tunajivuna kuwa na mama kama yeye, aendelee kupambana sisi wanawake wenzake tuko naye sambamba kuhakikisha tunayatenda kwa ajili ya watoto wa kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo yake kwetu sisi tulio chini yake. Kwa kweli, ni kiongozi imara, ni kiongozi makini, busara zake zinatuwezesha kufika hapa tulipo siku hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru wewe pia, kaka yangu, Mheshimiwa Spika Job Yustino Ndugai, kwa uongozi wako imara kwa Bunge letu Tukufu na Waheshimiwa Wenyeviti na watendaji wote wa Bunge letu Tukufu. Naomba niseme kwamba, najivunia na najisikia faraja kuwa ni Mbunge kutoka moja ya Majimbo ya Dodoma ambako wewe ni mlezi wetu, najivunia sana Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nimshukuru Mheshimiwa Waziri wangu wa Fedha. Kwa mara ya kwanza niliposimama ndani ya Bunge hili, miaka miwili iliyopita, tukiwa tunawasilisha bajeti ya Serikali kama hivi, nilimwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba, najivunia kufanya kazi chini yake. Miongozo yake, ushauri wake kwangu kwa kweli, ameweza kunifanya nisimame na kuwa ni mmoja wa Manaibu Waziri imara kabisa.

Mheshimiwa Spika, ulisema huwezi kujisifu mwenyewe, lakini naomba nijisifu mwenyewe na sijafika hapa ni kwa sababu, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ananipa nafasi ya kutenda haya ninayoyatenda. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na nakuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kukuimarisha, busara yako inatungoza sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia, niwapongeze sana watendaji wote ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Mheshimiwa Dotto James. Niliwaeleza tulipoanza mchakato huu mwezi Machi nikawaambia, kama ni siku basi ilikuwa alfajiri ule mwezi wa Machi na leo hii tarehe 26 mwezi Juni basi ni saa 12.00 jioni. Naomba niwaambie siku yetu tumeikamilisha kwa ufanisi mkubwa, Watendaji wote wa Wizara ya Fedha najisikia faraja sana kufanya nanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kusema na kama ilivyo kawaida yangu naomba ni-site Aya mbili ndani ya Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu, Quran na hii naomba iende kwa Mheshimiwa Rais wetu. Mheshimiwa Rais namwambia maneno haya ya Mwenyezi Mungu kutoka Surat Al-qalam, Aya ya 7 - 8; Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 7 kwamba:

“Falaatutwiil-mukadhdhibina, waddu lautudihinu fayudihinuun” Mwenyezi Mungu anasema hivi, wala usiwatii wale wanaokadhibisha yale unayoyatenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwambia Mheshimiwa Rais, asiwatii hata kidogo wale wanaokadhibisha jitihada zake anazozifanya kwa ajili ya wananchi wanyonge wa Tanzania. Dunia inaona, jamii inaona, Watanzania wanaona, Watanzania wanasema. Pia nimwambie Mheshimiwa Rais wangu kwamba, hii yote Aya ya pili niliyosema, Mwenyezi Mungu anasema, hao wanaokadhibisha wanatamani ulegeze japo kwa sekunde moja, ili waweze kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwambia Mheshimiwa Rais aendelee kupambana. Sisi tunaona, Watanzania wanaona na Mwenyezi Mungu akipenda 2019 haya ninayoyasema yatadhihirika ndani ya Taifa la Tanzania. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais endelea kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niseme machache katika hoja ambazo zimewekwa mezani na Waheshimiwa Wabunge wamesema. Hoja ya kwanza nayo imekuwa ni kuhusu Serikali ya Awamu ya Tano kuelekea kuziua halmashauri zetu. Jambo hili limesemwa kwa uchungu na msisitizo mkubwa na Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge lako Tukufu. Naomba niseme yafuatayo:-

Mhesimiwa Spika, limesemwa jambo hili kwa kisingizio cha kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua makusanyo ya property tax, lakini pia makusanyo ya ushuru wa mabango. Tulipitisha sheria ndani ya Bunge lako Tukufu na ndipo tulipoanza kutekeleza hili ambalo linalalamikiwa leo.

Mheshimiwa Spika, na sheria tuliyoipitisha, Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017 ilituruhusu kukusanya mapato haya kwenye halmashauri zetu zote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali siku zote ni sikivu na hasa Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, ni Serikali sikivu; ilisikiliza maoni yaliyotolewa katika ripoti ya Kamati yako Maalum, maarufu kama Chenge One. Chenge One katika taarifa ile walisisitiza kwamba, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato ya Tanzania ikusanye kodi ya majengo, ikusanye na kodi ya mabango na Serikali iko sikivu tukaanza kuyatenda haya.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tumefanya hivyo? Tumefanya hivyo, ili kama ilivyoshauriwa ndani ya Chenge One ni kuimarisha makusanyo ya mapato hayo, ili tuweze kuyapeleka kwa Watanzania kwa Taifa zima. Nimshukuru sana na niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliosema kabla yangu, wale waliokema ile kuligawa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nilisema mwaka jana wakati nachangia Bajeti ya Wizara ya Fedha kwamba, tuko kwenye hatari kubwa ya kuligawa Taifa hili vipandevipande, ule umimi tuuache ndugu zangu. Tunachokifanya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuyakusanya mapato haya na kuhakikisha tunayarejesha kwenye halmashauri zetu kulingana na bajeti za halmashauri husika na ndicho ambacho tumekuwa tukikifanya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge waelewe hiyo dhamira njema ya Serikali yetu, tumekuwa tukifanya hivyo, hakuna halmashauri ambayo imekosa bajeti ya maendeleo, wala bajeti ya matumizi ya kawaida katika utendaji wetu ndani ya miaka mitatu iliyopita. Katika kudhihirisha haya Serikali yetu imekuja na mpango wa kuziwezesha halmashauri zetu kuweza kuja na mipango imara, mipango mikakati kwa ajili ya kuongeza mapato ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, hili napenda kulisema, tuelewane jambo moja, Wakurugenzi wa Halmashauri ni watendaji wakuu wa halmashauri zetu. Hawa wanaitwa ni CEO wa halmashauri zetu zote na misingi ya mafanikio ya mtendaji yoyote wa taasisi haijawahi kubadilika kati ya sekta binafsi na sekta ya umma. Ndio maana sasa Serikali imekuja na mpango huu kwamba, tunataka kupima ubunifu wa watendaji wetu, ili tuweze kuwawezesha kuwapa pesa, ili waweze kutekeleza mipango ya maendeleo, lakini yenye tija kwa wananchi wanaowaongoza. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge sisi ni madiwani katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kaka yangu Jafo tulifanya kikao tarehe 14 Mei, pale Wizarani tukisaini mikataba ya shilingi bilioni 131.5 kwa ajili ya halmashauri zile zilizoonesha ubunifu wa kubuni miradi ya maendeleo itakayoleta tija kwa wananchi wao, itakayoleta tija kwa halmashauri zao kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Spika, naomba niwasifu sana Wakuu wa Mikoa wafuatao: Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawasifu Wakuu hawa wa Mikoa kwa sababu, wana-vision, wana ndoto ndani ya mikoa yao. Wamekaa na watendaji wao baada ya sisi kutoa mwongozo wa kuja na mikakati hii kwa ajili ya kuongeza mapato ya halmashauri, Wakurugenzi wao wakaja na maandiko mazuri ambayo yamepata fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi Jumamosi nilikuwa Mkoani Simiyu. Wengi wakanishangaa, unakwenda kuhitimisha bajeti kesho kutwa, umefikaje Simiyu leo? Nikawaambia niko Simiyu kwa sababu, ni utekelezaji wa bajeti tunayoipitisha. Nilikwenda Simiyu kuangalia viwanda vilivyoanzishwa ndani ya Mkoa wa Simiyu na Halmashauri za Wilaya ndani ya Mkoa wa Simiyu. Nikawa namuuliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa, nikamwambia baada ya kuanzisha kiwanda hiki cha chaki kwa mwaka mmoja unakusanya mapato kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, akaniambia ndio wameanza, wanakusanya zaidi ya milioni 600 kwa mwaka kwa kiwanda hicho kimoja. Nikamwambia una sababu sasa wewe na Baraza lako la Madiwani la kwenda kusimama kusubiri mapato ya kusubiri mtu anayetoka kujisaidia chooni kwamba, unakusanya mapato? Akaniambia hana sababu kwa sababu, ana miradi ambayo inamuongezea mapato na hana sababu ya kulalamika hajapata mapato kutoka Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, hili napenda lieleweke na liende kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote 185 kwamba, Serikali iko tayari. Mkoa wa Simiyu peke yake mikataba tuliyosaini juzi wamepata shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo na ndio maana nimekuwa
nikisema tatizo la Serikali ya Awamu ya Tano sio pesa, tatizo unataka pesa ukafanye nini. Hilo ni jambo la msingi sana, lazima tukae pamoja tuelewane kama viongozi, ili tujue ni nini tunakwenda kufanya na Watanzania tunaenda kuwapa nini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge hili la kulalamikia mapato haya yaliyokusanywa yamekusanywa yanakwenda wapi?Yamekusanywa halafu yanarejeshwa kwenye halmashauri kulingana na bajeti.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukiacha hiyo ya kurejeshewa hiyo tumekuja na mkakati wa kuongeza mapato ya halmashauri. Kwa nini tusikae na Wakurugenzi wetu tukaelekezana, wakaandaa maandiko, tukatekeleza, Serikali haijazuia kuanzisha viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Spika, naomba sisi tuwe wa kwanza kutenda maono ya Mheshimiwa Rais, tuwe sisi ni wa kwanza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, iliyosema 2025 Tanzania itakuwa ni Tanzania ya viwanda. Mwaka 2025 Tanzania itakuwa ni Tanzania ya watu wenye kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayawezekani haya kama tusipokuwa wabunifu sisi viongozi na tukawaelekeza wananchi wetu, tukaainisha fursa zilizomo ndani ya maeneo yetu katika kutenda ili kuja kuiona Tanzania ya viwanda na Tanzania ya uchumi wa pato la kati. Haya yanawezekana, mikoa niliyoitaja wameonesha dhamira hii kwa kuanza kutenda, wengine tuige ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi, naomba niziseme hizi mbili tu, najua muda sio rafiki, ilikuwa ni Serikali ya Awamu ya Tano kuvunja Katiba na Sheria kwa kukusanya pesa za Mifuko Maalum na kuziingiza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali bila kuzipeleka kwenye matumizi yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie hili, hakuna Serikali inayoheshimu Katiba, Serikali inayoheshimu sheria zilizotungwa na Bunge lako kama Serikali ya Awamu ya Tano. Nasema haya kwa sababu tunaielewa Katiba, Ibara ya 135 (1) na (2), Ibara ya 136(2), Ibara ya 143(2)(a) na (b) tunaifahamu kama Wizara ya Fedha na tunaifahamu Sheria ya Bajeti iliyotungwa na Bunge lako Tukufu. Hatuko tayari kuvunja Katiba yetu wala kukiuka sheria zilizotungwa.

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu kwanza mapato ya Serikali yako ya aina mbili, hayo yanayokusanywa kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali ambayo yametajwa katika Katiba 135(1) na (2), ambayo hayo yakikusanywa kutoka kwenye Revenue Collection Account ya TRA moja kwa moja huenda katika Mfuko Mkuu wa Hazina yakisubiri kupangiwa matumizi ili yapelekwe yanakotakiwa. Aina ya pili ni haya yaliyotajwa 135(2) na 136(2) ambayo ni mapato yenye Mifuko Maalum, matumizi yake ni maalum.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu, tunailinda Katiba, tunatekeleza Sheria. Hakuna mapato yoyote kutoka kwenye vyanzo maalum yanayoingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Mapato haya yakishakusanywa kutoka kwenye Petroleum Levy Deposit Collection Account yanakwenda moja kwa moja kwenye mifuko husika. Naomba kusema yafuatayo kwa data zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wetu wa Nishati Vijijini, mpaka kufikia tarehe 30 Mei, tulishakusanya shilingi bilioni 309.209. Nini tumepeleka kwenye Mfuko wa REA? Tumepeleka zaidi ya shilingi milioni 333.528 zaidi ya asilimia 108 ya tulichokikusanya kwenye kipindi hiki cha miezi 11. Kwa nini zimezidi hizi asilimia nane? Zimezidi kwa sababu huwa kuna lag period. Zinazokusanywa Juni, huwa zinakwenda kwenye REA Account mwezi Julai.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana mnaona hii 8% inayozidi. Ndiyo maana napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba tuko tayari, tuliapa kuilinda Katiba na kuisimamia Sheria. Hatuko tayari kuvunja Katiba wala Sheria.

Mheshimiwa Spika, huo ulikuwa ni Mfuko wa REA. Tukienda kwenye Mfuko wa Barabara, mpaka tarehe 30 Mei, 2018 tumekushanya zaidi ya shilingi milioni 740,655. Nini tumepeleka kwenye Mfuko wa Road Fund? Tulichokipeleka ni shilingi milioni 783,141 zaidi ya asilimia
100 imezidi 6%. Kwa hiyo, hakuna sehemu ambako fedha hizi za Mifuko Maalum zinakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, hapana. Tutalinda sheria na pia tutaisimamia.

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Reli, mpaka tarehe 30 Mei, 2018 tumekusanya shilingi milioni 203,974 na tumepeleka shilingi milioni 221,971 zaidi ya asilimia 109.

Mheshimiwa Spika, najua ni kengele ya pili, yako mengi ya kusema, lakini nataka kusema haya yanayoonesha image ya Wizara ya Fedha kwamba tunavunja Katiba na Serikali yetu, nasema hapana, hatuvunji Katiba. Tuko tayari kufanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu, kuhakikisha Taifa hili linasimama kiuchumi, tunafikisha maendeleo kule kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kile nilichomwambia Mheshimiwa Rais wangu nilipoanza kusema hapa, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri wangu wa Fedha kwamba Falatutwii-l-mukadhdhibina, waddu Lautudihinu, fayudihinuun. Wala usigeuke nyuma, utageuka jiwe Mheshimiwa Waziri. Chapa kazi, tuko tayari kukusaidia kufanya kazi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.