Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Sasa hivi kwa taarifa za Mheshimiwa Waziri suala la utalii wa uwindaji umeanza kupungua. Hata ukiangalia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri mapato ya utalii yameanza kupungua, ukiangalia vitalu vingi vya utalii vimeanza kurudishwa na pia kuna mchakato unafanyika nchi za nje kuhakikisha kwamba wanazuia, kwa mfano sasa hivi kuna maeneo ambayo nyara za tembo zimezuiwa kuingia, nyara za simba zimezuiwa kuingia, kwa hiyo, lazima kujikita zaidi kwenye utalii wa picha ambao ndiyo utalii wenye faida kubwa na endelevu. Ndani ya Wami Mbiki kuna Mto Wami unapita pale katikati, una samaki wa kila aina lakini kuna uwanda wa aina mbalimbali, kuna eneo unakuta tembo peke yake, unakuta twiga peke yake, unakuta swala pala (impala) na vitu vya aina hiyo. Kwa hiyo, ningependa sana kwa location ya eneo lile WMA hii iwe chini ya TANAPA.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tunasisitiza sana utalii wa ndani. Eneo la Wami Mbiki ni eneo ambalo mtu anaweza kutoka Dar es Salaam akafanya utalii, Mbunge anasafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ana-spend siku moja pale anakwenda Dar es Salaam, eneo lile kwa potentiality yake nashauri Serikali ilifanye liwe chini ya TANAPA liweze ku- utilize vizuri rasilimali ambazo ziko pale ndani ya WMA ya Wami Mbiki.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni vitalu. Tulipitisha hapa sheria mwaka 2009, tulibadilisha Sheria ya Wanyamapori kwa sababu tasnia ya utalii wa uwindaji ilikuwa inamilikiwa na wageni kwa asilimia 100. Tukasema haiwezekani tasnia hii iwe ndani ya mikono ya wageni peke yao na ili Watanzania waingie tukarekebisha sharia. Tukaishauri Serikali Watanzania wenzetu wawezeshwe kimitaji ili waweze kuingia kwenye tasnia hii. Pia kuwepo na masharti nafuu kwa Watanzania ili waweze kuingia kwenye tasnia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, yote haya hayakufanyika, hakuna mitaji waliyopewa na bahati mbaya kwenye utalii wa uwindaji kuna investment kubwa sana, uwekezaji wake ni mkubwa bila kuwezeshwa kimitaji hawawezi. Matokeo yake wamechukua vitalu, wameshindwa kuviendesha, vimerudi Serikalini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali bado tuna ulazima wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki kwenye tasnia ya utalii. Nachoomba tuwawezeshe kimitaji na tuwape masharti nafuu. Bahati nzuri wale Watanzania wenzetu wakinufaika na utalii ule wanawekeza ndani ya nchi, wenzetu wale wa nje wanakwenda kuwekeza kwao. Kwa hiyo, suala la sekta ya utalii wa uwindaji tunaomba sana Serikali iingilie kati isaidie wazawa waweze kushiriki kikamilifu kwenye tasnia ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Hifadhi ya Mikumi ambayo iko karibu sana hapa, barabara kubwa inayotoka Morogoro kwenda Kilosa na kwenda Kusini inapita pale, lakini wanyama wanauwawa sana kila mwaka. Kila siku tembo na twiga wanauawa, ukipita barabara ile utaona huruma. Ninachoshangaa tulipendekeza angalau kuwepo na geti mwanzoni na mwishoni mwa ile barabara, nasikia TANROADS wamekataa hakuna kuweka geti, watu wanapita pale wanatalii bure bila kulipa chochote. Hata shilingi 1,000 kwenye basi moja kwa siku, tungeweza kupata fedha za kuendelea kutunza eneo lile lakini Serikali imekataa.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tulipendekeza barabara ile ichepuke ipite mbele ya hifadhi lakini bado imeshindikana. Sasa rasilimali zetu wenyewe Watanzania ni za kutusaidia sisi wenyewe iweje tuwe na hifadhi ile katikati yetu hapo hapo Mikumi tunashindwa kuiwekea mazingira ya kuingiza zaidi kiasi kwamba mpaka sasa hivi inategemea hifadhi nyingine kwa ajili ya kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iangalie suala la barabara ile ambayo inaua sana, pale speed inatakiwa 50 wanapita kwa 120 au 140, matokeo yake wanaua wanyama hata wakilipishwa lakini bado wanaendelea kuua. Kwa hiyo, ili tuweze kunufaika na ile hifadhi, naiomba Serikali iweke utaratibu wa kuwa na geti mwanzoni na mwishoni. Mimi nimetembea mpaka nchi za nje, huwezi kupita katikati ya hifadhi bure, haiwezekani, ni hapa kwetu nashangaa. Hata ukienda Namibia barabara zote hata kama ni za udongo maadamu inapita katikati ya hifadhi lazima kuna tozo fulani inayotozwa ili hifadhi ile iendelee kulindwa.