Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na namuomba sana Mungu leo aniwezeshe nisije nikalia humu kwa jinsi watu wa Tarime wanavyoteswa na Serikali hii.

Mheshimiwa Spika, watu wa Tarime wameteswa sana kwenye masuala ya madini, mpaka na sasa wanateswa sana kwenye suala la mbunga na mambo ya TANAPA.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Waziri wa Ardhi yuko humu atuambie ni nani hasa kati yake au kati ya Wizara yake na watu wa TANAPA au Wizara ya Utalii wanaohusika na masuala ya ardhi ya nchi hii? Kwa sababu leo tunavyozungumza na nataka niunge mkono taarifa ya Kamati iliyosema mambo yanayoitwa vigingi vinavyowekwa kwenye miji ya watu na kwenye ardhi za watu yasitishwe mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sijui kama nchi hii tunafikiria vizuri kwamba leo wafugaji wa nchi hii wakiamua hata kwa siku 10 peke yake kuzuia mifugo yao kuuzwa kwa ajili ya nyama mtatoa wapi nyama katika nchi hii? Sijui kama tumewahi kulifikiria hilo. Leo wafugaji ambao ni zaidi ya milioni 10 wamekuwa watumwa katika nchi hii, wanaishi kama watu ambao hawatakiwi katika nchi hii, Serikali yao wenyewe inawatesa watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wiki moja iliyopita watu wa Tarime, Kata ya Kwihancha wameenda watu wa TANAPA na DC na group la watu wake anajua alipolitoa, wanakwenda kwenye vijiji, Mwenyekiti wa Kijiji hajui, Diwani hajui, wanavamia, wanaweka kitu kinaitwa buffer zone mpaka ndani ya shule, zahanati, ndani ya miji ya watu, kwenye vungu za watu wanaingia wanachimba ndani wanaweka buffer zone, ndani kwenye mji wa mtu.

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Gibaso kina kaya 120 zote ziko ndani, wanaambiwa watoke hapo, wameishi tangu mwaka 1975 na kijiji hicho kina usajili. Vijiji vya Karakatonga, Gibaso, Nyabirongo, kaya zaidi ya 200 zinaambiwa zihame. Ukienda Kata ya Gorong’a, Vijiji vya Kenyamosabi, Masanga, Nyanungu, Nyandage na Kegonga kaya zaidi ya 2,000 zingine zinaambiwa zihame. Hawa watu hawafuati utaratibu, hawafuati GN, hawafuati chochote. Ukienda pale kuna GN Na. 235 ya mwaka 1968 iliyosainiwa na Mwalimu Nyerere inaonesha mipaka yote kuanzia chini mpaka juu upande wa ile mbuga, they just don’t care. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanakwenda pale, wanavamia, wanapiga watu, wanaswaga ng’ombe za watu wanaingiza mbugani. Mwanakijiji mmoja ng’ombe wake 250 wameswagwa wameingizwa mbungani, hii hapa risiti aliyoandikiwa ya shilingi milioni 25. Ng’ombe 250 wakiwemo ndama ambao hawana thamani ya shilingi 20,000 analipishwa shilingi milioni 25. Fikiria hata Mbunge mwenyewe ambaye anapata mshahara hapa aambiwe kutoa shilingi milioni 25!

Mheshimiwa Spika, ukichukua hizi karatasi, mwingine ana ng’ombe 54 analipishwa shilingi 540,000, mwingine ana ng’ombe 54 hao hao analipishwa shilingi 5,400,000, risiti fake. Watu wanalipishwa mpaka shilingi milioni 100. Hebu imagine katika nchi hii shilingi milioni 100 unamlipisha mfugaji? Ng’ombe zaidi ya 15,851 wamekamatwa na watu wa TANAPA. Kijana mmoja baba yake alikamatwa …

SPIKA: Wamekamatwa kwenye buffer zone au ndani ya hifadhi?

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nazungumzia masuala ya buffer zone. Kijana mmoja ng’ombe wao 400 wamekamatwa, baba yake akapata mshtuko akafa, mama yake naye akafa anasoma Mzumbe wakarudi wakazika. Wamefanya kesi, wamefika mpaka High Court, High Court ime-rule kwamba wapatiwe ng’ombe wao 400 amekuta ng’ombe 25 peke yake. Huo ndiyo unyama ambao watu wa nchi hii wanafanyiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wa Tarime wamepigwa risasi, Chacha Gasaya, Wang’enyi Muhere, Marwa Goyagwe, Chirawe Marwa Sira, hawa ni watu ambao wamepigwa risasi na wamekufa. Thobias Waitara, Chacha Gioto, Marwa Ryoba, Kebacho Kebacho, Mwera Muhere hawa ni watu ambao wameuawa kwenye mipaka hii ambayo ipo na watu wameishi hapo, vijiji vimesajiliwa tangu mwaka 1974. Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa bila aibu wanadanganya. Adam Malima ambaye juzi ametishiwa pale Dar es Salaam akapiga yowe dunia nzima ikasikia anakwenda kuwaambia watu wa Tarime kwamba atawashughulikia na Jeshi yaani kwamba Rais amempa mamlaka hayo ili akawashughulikie watu wa Tarime badala ya kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, naongea haya kwa uchungu mkubwa sana halafu wanasema uongo, wanasema watu wamewarushia mishale. Mimi nimemuuliza Waziri, pale Nyanungu kijiji kizima kina watu zaidi ya 5,000 warushe mishale kwa watu 14, mshale hata mmoja usimpate hata mtu mmoja miongoni mwao. Wamerusha mawe hakuna hata gari moja lililopatwa na jiwe yaani kijiji kizima hakina shabaha kiasi cha kushindwa kulenga hata kwenye kioo cha gari moja. Wamekamata watu 100, wamekaa nao siku nne Polisi, DC anawaimbisha nyimbo kwamba sisi ni wahalifu, akina mama, watoto wanaimba Kituo cha Polisi wanapiga makofi, sisi ni wahalifu, tunapaswa kufungwa, kwenye nchi hii. Mazao ya watu yanaharibiwa na ng’ombe wa watu wanataifishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa namuomba Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, msilete machafuko na chuki kubwa kwenye Taifa hili. Haya mambo yanaumiza kweli kweli, yanatia simanzi kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, watu wa Tarime tumelinda hiyo mbuga kwa miaka yote, haina faida yoyote na watu wa Tarime. Haijawahi kutujengea darasa au bati moja. Naomba msilete machafuko kati ya watu na mbuga. Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla nenda kaondoe zile buffer zone kaweke kule ambako beacon zinaonesha zinatakiwa kuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri chukua GN Na. 235 iliyoachwa na Mwalimu Nyerere fanyia kazi. Msitake kuua watu wa Tarime, tumechoka kuuawa, tumechoka kufanywa wanyama katika nchi hii, kila kitu kwetu ni hasara tu. Madini hayajasaidia watu wa Tarime, mbuga nayo imegeuka kuwa mauaji kwa watu wa Tarime. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mbuga hii hapa ya Selous leo Serikali imetoa kibali cha kwenda kukata zaidi ya miti milioni tatu, hamuoni hilo ni tatizo? Hamuoni kama ni uharibifu wa mazingira lakini ardhi yetu waliyoacha mababu zetu, tunaishi pale watu wamezikwa kuna makaburi wanakwenda kuchimba kwenye kaburi la mtu wanaweka kigingi, juu ya kaburi mtu anaweka kigingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, analeta GPS, GPS ilikuwa wapi mwaka 1968? Kulikuwa na GPS katika Taifa hili mwaka 1968? Watu wamepigwa hapa, kuna wazee wako hapa wa Kisukuma wanalia, wengine anatoka kwenye Jimbo la Mheshimiwa Doto na Majimbo mengine, watu wanateswa.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ichukue hatua kwenye masuala haya yataleta machafuko mabaya sana. (Makofi)