Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nianze kabisa kusema kwamba naunga mkono taarifa ya Kamati, hii taarifa ni nzuri sana na imewasilishwa kitaalamu kweli kweli, niwapongeze Wanakamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utalii atika Taifa letu, kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2012 mpaka 2015/2016 utalii ulikuwa unakuwa kwa takribani asilimia 13.98 lakini mwaka 2016/2017 utalii umeshuka mpaka asilimia 3.3. Hii inatokana na kutokutekelezwa kwa sheria, matamko ya ajabu ajabu, kutokutabilika kwa kodi, sijui tunaenda wapi? Kwa sababu utalii 2013/2014 ulikuwa umekuwa kwa asilimia 17.5 na mwaka huu wanasema asilimia 17 lakini Serikali hii ilisema utalii ifikapo 2020 utakuwa umekuwa kwa asilimia 30 lakini badala yake umeshuka mpaka asilimia 3.3; kulikoni Serikali ya Awamu ya Tano? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mazingira rafiki ya utalii; nilishawahi kusema tena hapa na narudia, Tanzania tunahitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania. Ukiangalia kodi katika sekta ya utalii ziko zaidi ya 57, lakini kodi hizi kila kukicha kodi. Dubai juzi wametangaza ufutaji wa kodi kwenye sekta ya utalii na pia wanatoa viza kwa foreigners kwa zaidi ya miaka kumi katika ku-invest seriously kwenye utalii, lakini hapa kwetu kutoa kibali cha foreigner kwenye utalii ni dola 4,000 na ni kwa miaka miwili mpaka miaka minne. Sasa kupanga ni kuchagua, je vivutio vya utalii tunavifanyaje?

Mheshimiwa Spika, Mapato Yanayotokana na Utalii. Kati ya fedha zinazopatikana kutokana na utalii, na Waziri wa fedha alikuwa hapa; kwa mfano takribani dola za Kimarekani bilioni 10 utalii peke yake inachangia asilimia 25 takribani dola za Kimarekani bilioni 2.3, inafutiwa na bandari transit goods bilioni mbili, dhahabu bilioni 1.6. Kwa hivyo hawa giant watatu ni zaidi ya asilimia 61 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Tanzania miaka miwili, mitatu iliyopita tulikuwa wa pili kwa vivutio vya utalii duniani kati ya nchi 133, lakini kwenye miundombinu ya utalii tunashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133.

Mheshimiwa Spika, sasa utalii maana yake ni nini? Tutafikiaje watalii 8,000,000? Kwa mfano utafiti ulikuwa umefanyika, lazima tuwekeze kwenye miundombinu ya utalii, lazima tuwekeze seriously na tuamue kwamba kwenye sekta hii ya utalii, kwa sababu kwa mfano TANAPA leo hii, Ngorongoro na wale wengine wote. Inakuwaje Serikali inachangia Mfuko Mkuu wa Serikali na Serikali hiyo hiyo inachukua corporate tax kwenye mashirika?

Mheshimiwa Spika, kwa mfano fedha ambazo zimepatikana TANAPA kwa mwaka 2017/2018 zilikuwa ni takribani shilingi bilioni 214, Ngorongoro yenyewe ni shilingi bilioni 104. Mwaka huu tunategemea TANAPA yenyewe wapatikane shilingi bilioni 292.8 Ngorongoro shilingi bilioni 156. Sasa lakini miundombinu ya utalii ipo hoi bin taabani.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia huwezi ukatangaza, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema wameweka mpango mkakati wa TBC kutangaza utalii. TBC itamtangazia nani duniani? Ningetaka nisikie kwamba katika kutangaza huku, mashirika kama CNN, BBC, Voice of America, Aljazeera, India, China, Sky News na mengineyo mengi ndio wanaotangaza utalii. Utafiti umeonesha tukiwekeza vizuri kwenye utalii, kwa miaka mitatu/minne tutakuwa tunapata dola za Kimarekani bilioni 16.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa kiasi kikubwa kwa mfano TANAPA kati ya hifadhi 16 hifadhi tano zinatoka Serengeti, Mlima wa Kilimanjaro, Tarangire, Manyara, Arusha. Kwa miaka kumi mfululizo kwa mfano, Mlima wa Kilimanjaro peke yake uliliingizia taifa hili fedha shilingi bilioni 471.5; uendeshaji ulikuwa shilingi bilioni 67.5 miradi katika vijiji ambavyo vinazunguka mlima huo ambavyo vilikuwa 88 zilikuwa shilingi bilioni 8.2 ambayo chini ya asilimia 0.48 ilhali sera inasema ni asilimia 7.5. Tukiendelea namna hii ni kwamba tunaua utalii wetu sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, utalii Kaskazini kwa mfano, kuna tamko lililotolewa kwamba watu wa Kaskazini wasubiri kwanza, nilisema eeh Mwenyezi Mungu atujaalie, nilitumia Zaburi ya 141:3. Nilisema Mwenyezi Mungu awasaidie viongozi wa Taifa hili walinde vinywa vyao na awe mngojezi pa midomo mwao kabla hawajatamka. Huwezi ukaligawa taifa kwa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha za kigeni asilimia 25 zinatoka Kaskazini au zaidi ya asilimia 98 zinatoka Kaskazini. Nakubali Ruaha na sekta nyingine zote lakini kwenye classification theory ya kawaida tu, aliye class A unaendelea ku-maintain kubaki class A wakati unamnyanyua na huyu mwengine aweze kufika class A. Huwezi ukasema kwamba huyu wa class A unamwambia stop, unamshusha tuu aende chini, thinking ya wapi hii?

Mheshimiwa Spika, kweli nimeshangaa sana, Taifa hili ni moja na ndiyo maana Mathayo 5:9 wanasema heri wapatanishi wanakuwa wana wa Mungu. Tunakuwa ni kitu kimoja, roho ya umoja Baba wa Taifa uliyoijenga ndani ya Taifa hili, Taifa hili ni moja. Watu wengine wa kutoka Kaskazini sasa hivi wanaanza kuonekana kama si watu wa Tanzania, hapana. Mama tibaijuka ameongea vizuri, yaani tumeanza kugawana kwa misingi ya kikabila, ukanda, taifa letiu linakwenda wapi? Tanzania ni yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusipoangalia tunakokwenda; nilisoma Kumbukumbu ya Yoshua bin Sira leo asubuhi, anasema kama huna macho yaani huna mboni ya jicho basi huwezi kuona na kama huna ufahamu huwezi kuwa na hekima. Wimbo wetu wa Taifa unazungumzia hekima, umoja na amani, ni rai yangu kwa viongozi wa taifa hili wazingatie wimbo wa taifa kwenye ile hekima, umoja na amani ili tuweze kukuza utalii vizuri ndani ya Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hoteli za Tanzania ziko hoi, nimeangalia hotuba ya mwaka jana inaonesha idadi ya hoteli tulizokuwa nazo na huduma za hoteli ziko 1,424 vitanda 35,000 ambapo ni sawa sawa tu na vilivyopo mji wa Mombasa peke yake. Sasa tunasisitiza kukuza utalii hapa kwetu, lakini tunapoanza kusema angalia ufukwe wa Bahari ya Hindi una kilometa 1,424. Serengeti peke ake ina kilometa za mraba 14,750 Masai Mara ina 1,510 ambayo inaingia mara kumi ndani ya Serengeti, lakini Masai Mara inashindana na hizi 14,750, tunafikiriaje sisi? Lazima tufikiri seriously.

Mheshimiwa Spika, suala la vigingi, nilienda kule Ngarenanyuki na Momela. Hiyo bila hata ya ubishi wowote. Nimekwenda binafsi mpaka Makanisa ya KKKT yamefungiwa ndani, shule zimefungiwa ndani, watu wamepigwa makanisani, mambo gani haya? Nchi hii ya utawala wa sheria?

Mheshimiwa Spika, na mwaka huu tunatimiza miaka 70 ya tamko la ulimwengu na haki za binadamu ambalo lilianzishwa tarehe 10/12/1948 siku ya Ijumaa, lakini mpaka sasa miaka 70 tunapiga watu mpaka tunaingilia kwenye makanisa wanakosali Jumapili!

Mheshimiwa Spika, nilikwenda mwenyewe Momela mpaka wazee wanajificha ndani ya kanisa ndiko wanatupa chakula kule Ngarananyuki? How? Why? This is not possible.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani ndani ya nchi hii hiii? Halafu Serikali iko kimya kwenye ukiukaji huu mkubwa? Ndiyo maana Tanzania leo hii tunashika nafasi ya 153 kati ya nchi 156 kwenye happiness index, yaani sisi tuko na Burundi, tuko na Yemeni tuko na wapi huku, si unajua, hata Somalia wametupita kwenye ukiukwaji wa haki za binadamu. How? Nchi gani? With due respect hapana hatuwezi tukakubali, Taifa hili tuwekeze akili zetu vizuri, tuangalie tunataka kufanya nini.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye miundombinu kwa nini tusiwakubalie ngugu zetu wa TANAPA na wengine wote, Ngorongoro na wengine, badala ya ule mfuko wa kuweka Serikali Kuu, japo ipo kwa mujibu wa sheria? Tuwekeze kwenye miundombinu ya utalii, miaka miwili, mitatu, minne, mitano, ijayo tayari tuna-double tunachopata au mara tatu; utafiti wa World Bank wamesema ni dola za Kimarekani bilioni 16 kama tukiwekeza vizuri.

Mheshimiwa Spika, mbuga nyingine za Ruaha, Katavi, kote huko tuzinyanyue lakini zinyanyuke kwa Serikali kukiri kuwekeza vizuri. Tukiwekeza kwenye utalii vizuri ndani ya Taifa hili litatoka, angalia hata kwenye ajira, utalii peke yake ni direct ni ajira zaidi ya 500,000 kati ya ajira 2,500,000.

Mheshimiwa Spika, sasa kila siku tunasuasua tunaongea lungha hii hii kwa nini hatufanyi maamuzi? Kwa nini hatukubari kwamba Tanzania yetu hii Mwenyezi Mungu alivyotujaalia Tanzania hii ilivyo nzuri, kwa mfano pale kwetu, ninakotokea, Jimbo la Vunjo, lango kuu la kuingia Mlima Kilimanjaro, kwa miaka kumi yale mapato ambayo yamepatikana pale, ukiangalia vile vijiji viko hoi bin taabani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna chuki imejengeka kati ya askari wa kulinda mbuga na raia. Kwa mfano vijiji vya Mshiri, Kijiji cha lyasongoro, vijiji vyote ambavyo vinazunguka, Kirie kote huku wanaonekana kama ni adui badala ya kuwa ni rafiki; na haya ni matatizo ya chuki tuu zinazojengwa. Sasa tujenge mahusiano yaliyo mema na yawe mema kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, tulikwenda huko na Naibu Waziri wa Utalii kabla hajabadilishwa akaona matukio ya utesaji wa hali ya juu. Sasa naamini TANAPA, General ni mtu makini sana lakini nadhani kuna vurugu zinaingilia katikati ambazo si nzuri. Tutumie lugha iliyo nzuri ili tuhakikishe haya yote tuliyonayo ni kwa maslai mapana ya mama Tanzania ambayo ni yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupanga ni kuchagua, wenzetu wa Kenya ukiangalia walivyowekeza, ukisoma hata kwenye website, nilikuwa nasoma leo asubuhi, kwa miaka mitano ijayo utaona wanataka wafikie wapi kwenye utalii utaona hapa kwetu tunasuasua, ni blaa blaa tu tunafanya.

Mheshimiwa Spika, tuiwezeshe Wizara kwa mfano, Wizara imeomba bajeti hapa shilingi bilioni 115, lakini ukiangalia mapato tuu yanayotokana haya maduhuli yanayotiokana Wizara inayochangia ni shilingi bilioni 623.5.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, Mwenyezi Mungu akubariki sana.