Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza niwashukuru tu watendaji wa Wizara tukianza na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kasoro wale tu wanaodhulumu ng’ombe hao siwezi kuwashukuru hao ambao wanadhulumu ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, naliona jambo moja muhimu sana ambalo unaweza ukalifanya wewe kwa ujasiri wako. Wizara tulipokuja hapa Bunge hili tulikuwa tunataka kushughulikia masuala ya wafugaji na ardhi ya migogoro ya mipaka. Zikawekwa Wizara tano kushughulika matatizo hayo, zimeshindwa, zimeshindwa kushughulika matatizo ya wananchi katika mipaka na mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nakuomba wewe sasa ama uunde Kamati Maalum ya Bunge kushughulikia migogoro hiyo au ukiona hilo ni gumu utuachie Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii washughulikie hiyo migogoro. Kwa maana sasa watendaji wa Maliasili wanaoshughulika na mapori ya akiba na hifadhi wanachokifanya ni kile ambacho umekizungumza sasa hizi hapa wanakwenda na ramani, hata kama hiyo ramani mipaka yake ya asili ilikuwa Bahi, lakini ramani yao inaonesha wamekuja vigingi UDOM, watafika UDOM halafu wanamwambia mwanakijiji vigingi vyetu vipo hapa kwa hiyo tuamue hapa. Haliwezi kuisha, hauwezi kuachia mgogoro wa mtu aliyeweka mwenye mali halafu aamue mgogoro wake, haiwezekani.

Kwa hiyo, tukubali sasa ile Wizara ya Ardhi na zile Tume zilizounda zimefeli. Sasa ni jukumu lako uunde Tume au uwaambie watu wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii waendelee ku-solve hiyo migogoro uwape mamlaka hayo, nilikuwa nafikiri kwamba hilo ni la maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Stiegler’s Gorge nilikuwa naliona kwangu kwa mawazo yangu, kwa sababu wafadhili hawawezi kujenga ule mradi, kama Serikali yetu ina uwezo wa kujenga huo mradi na wana fedha za kujenga huo Mradi wajenge na kama fedha hizo za mradi huo zitahujumu maeneo mengine ya miradi kwa mfano kwenye kilimo, ardhi, viwanda kama fedha zetu hazitoshi kujenga Stiegler’s Gorge kwa maana kwamba tuna mambo mengine yanagusa wananchi tuangalie upya juu ya mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake isije ikawa tukachukua fedha zote kama hatuna ufadhili tukazipeleka kwenye Stiegler’s Gorge halafu maeneo mengine ya nchi yakaathirika na mradi huo. Lakini kama ni mazingira, mimi mwenyewe nimesoma mazingira, mazingira yapo kwa ajili ya binadamu na binadamu yupo kwa ajili ya mazingira. Habari ya kukata miti milioni ngapi hiyo sawa, lakini miti mingapi tunakata kwenye nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuangalie kama tuna fedha ya kujenga hiyo ndo muhimu ili maeneo mengine haya tusije tukamalizia fedha. Kwa sababu wafadhili hawapo tayari kufanya ule mradi, nimeusoma muda mrefu wafadhili wamekuwa wakitukataza mambo mengi tu hata barabara ya Loliondo, hata maeneo ya kujenga viwanja vya ndege hata nini hawajengi viwanja hivyo. Kwa hiyo, suala ni moja tu tukubali tu Wabunge watuambie na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ituambie ina fedha za kujenga? Je, fedha hizi hazitaathiri maeneo mengine ya uchumi wetu? Basi hilo ndiyo jambo muhimu la kufanya kwenye mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumza kwenye maeneo yangu ya Bunda kwamba niwashukuru Wizara wamekuwa wanafanya maendeleo kwenye maeneo yanayozunguka vijiji vinavyozunguka mbuga za wanyama, niwashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kunijengea Kituo cha Afya Kunyali, wanafanya maendeleo, niwashukuru Wizara kwa kuleta barabara zile za kuvuka vijiji 15 vya kwangu havina uwezo wa kwenda porini kwenye eneo la Serengeti wamesema watafungua barabara ya kutoka Mgeta kwenda kule. Nimshukuru Mtu wa TANAPA, ndugu yangu Kijazi kwa kuona hili kwamba sasa mnaenda kufanya maendeleo kwenye maeneovijiji vinavyozunguka maeneo yanayotuzunguka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru kwa mpango wenu wa kupima vijiji vinavyozunguka maeneo haya ili vipate hati waweze kufanya biashara na mambo mengine na vijiji vyangu 15 mmsema vitakuwemo katika vijiji hivyo Unyali, Mgeta, Maliwanda, Kihumbu na maeneo mengine ambayo amezunguka maeneo haya. Niwashukuru sana kwa mpango huo ambao mtaufanya kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna zile vitu vya buffer zone, sasa buffer zone nashangaa buffer zone za National Park au Hifadhi ya Taifa kwa maana Mapori ya Akiba, TAWA na TANAPA zinakwenda kuweka kwenye maeneo ya vijiji mpaka ambao siyo wao, wao wanaweka mipaka kwa nini sasa? Kwa nini buffer zone isiende kwenye upande wako wewe? Nadhani kwa kuunda hiyo Kamati ambayo tumeisema tutashughulikia matatizo kama haya nadhani yanaenda kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla niseme jamani timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga vizuri. Kigangwalla wanaweza wakakutafsiri kwa maana umekaa kimya upo hivi, lakini una uwezo wa kufanya kazi, Naibu wako anauwezo wa kufanya kazi, Makatibu wana uwezo wa kufanya kazi kwa hiyo tuwashukuru waendelee kufanya kazi.