Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni nchi ya kilimo. Asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania wanategemea kilimo. Ili kupunguza umasikini na kuondoa utegemezi wa nchi wahisani, ni lazima tuwekeze kwa kiasi kikubwa katika kilimo na tuwe na mikakati thabiti ya kukiboresha kilimo chetu. Hivyo basi, hatuna budi kilimo chetu sasa kijielekeze katika kuongeza uzalishaji kwa ekari moja na kuachana kabisa na ukulima wa jembe la mkono. Kwa mfano, nchi kama China wamefanikiwa sana katika kilimo cha uzalishaji kwa ekari moja. Ukilinganisha ukulima wao na wetu, wakulima wetu wanalima ekari tatu mpaka nne lakini wanapata mazao ya ekari moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida kijiografia ni mkoa wenye hali ya ukame ambao unapata mvua kwa msimu mmoja na unakabiliwa na changamoto nyingi katika Sekta ya Kilimo. Kwa hiyo, kuna haja ya Serikali kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Singida waweze kulima na kunufaika na kilimo cha matone kwenye maeneo yenye chemchemi na maeneo ambayo hayana chemchemi, basi Serikali iwasaidie kuchimba mabwawa ya maji ili waweze kulima na kuvuna kwa misimu yote ya mwaka. Maeneo ambayo yamenufaika na kilimo cha matone Mkoani Singida ni Isana, Mkiwa, Uhamaka na Kisasida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida pia unakabiliwa na uhaba wa Maafisa Ugani pamoja na mashamba darasa. Naomba Serikali iunge mkono jitihada za uanzishwaji wa mashamba darasa kwani yana mchango mkubwa wa maendeleo ya kilimo, siyo tu kwa kuwafundisha wakulima kwa niaba ya Maafisa Ugani, bali pia husaidia kutoa utaalam wa kuzalisha mbegu bora za daraja linalokubaliwa, yaani QDS.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni mkoa unaosifika kwa kilimo cha alizeti, mahindi, mtama, uwele, karanga na vitunguu, lakini bado wakulima wake hawajanufaika na ukulima huo na hii ni kutokana na ukosefu wa soko la kudumu au vituo maalum vya kuuzia mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ya Awamu ya Tano kuona umuhimu wa kujenga soko kubwa la kisasa la mazao kwenye Manispaa ya Singida, kwani uwepo wake utatoa nafasi kwa wakulima wengi kunufaika na bei za mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida unakabiliwa pia na ukosefu wa vituo vya utafiti ikiwemo maabara ya matumizi ya udongo na hii hupelekea wakulima wengi wasiweze kujua hali ya ardhi yao na hivyo kusababisha uzalishaji duni. Naomba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kulitazama kwa kina na kuona ni namna gani wataweza kuwasaidia wakulima wetu katika kutambua matumizi bora ya ardhi ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mifugo, Singida ni hodari wa ufugaji wa ng‟ombe, mbuzi na kondoo lakini bado zipo changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya mifugo Mkoani Singida. Changamoto hizo ni uhaba wa majosho, uhaba wa maeneo ya malisho na magonjwa ambayo kwa asilimia 70 yanachangiwa na mdudu kupe. Hivyo basi, naiomba Serikali yangu sikivu kuongeza majosho ya kutosha, kutenga maeneo ya malisho na maji na kuleta dawa za chanjo na dawa hizo zifike kwa wakati.