Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, hili la Stieglers’ Gorge halihitaji wala akili nyingi, ukifananisha eneo la UDOM na Dar es Salaam kwamba kulikuwa na wanyama pori na kwenyewe na hili eneo la Stieglers’ Gorge ambalo ni Selous, haihitaji kusoma hata kidogo kujua kwamba kule hakuna wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wafugaji wa nchi hii kwa muda mrefu wameonewa sana. Mwaka 1968 Mwalimu Nyerere alipokuwa Rais wa nchi yetu, alipotembelea eneo la Indumiet kule Longido, ambayo kwa sasa ni Siha aliwaambia Serikali kwamba wafugaji watengewe ekari 5,500 kwa ajili ya kufuga, mwaka 1968. Mwaka 1973 Bunge hili likatunga sheria na kuiagiza Serikali mwezi wa tatu, mwaka 1973 kwamba wafugaji wapewe eneo hilo. Serikali kupitia GN Na. 59 mwaka huohuo wakatenga ekari 5,500 kwa ajili ya wafugaji, lakini TANAPA kwa kukaidi maagizo ya Mheshimiwa Rais Nyerere, Marehemu, Baba wa Taifa, waliwanyang’anya wananchi wale ile ardhi wakairudisha Kilimanjaro National Park. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka 1998 Mahakama ya Rufani chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu Nyalali iliiagiza Serikali ya Tanzania kuwapatia wafugaji wa Mkomazi eneo lingine mbadala la kufugia. Mpaka leo miaka 20 tayari kamili wafugaji wale wanahangaika wako pale juu, wanahangaika hawana eneo la kufugia.

Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi, juzi mwezi Februari, 2018 Mheshimiwa Kigwangalla alienda Wilayani Simanjiro, Kijiji cha Kimotorop, najua unafahamu kwa sababu, ulitembelea muda mrefu sana, Kijiji cha Kimotorop. Amekuta vigingi wanyama pori wamepiga kuanzia pale zahanati, shule ya msingi na kuchukua kaya 3,000 akatoa tamko kama Waziri kwamba wafugaji wale wote wafukuzwe na waondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike mahali sasa mnajiuliza kwa nini Tanzania tunashika nafasi ya 110 duniani kati ya nchi 133 kiutalii, mnajiuliza ni kwa nini pamoja na vivutio vikubwa ambavyo tunavyo. Jibu ni dogo, laana na vilio vya wafugaji nchi hii na wananchi wanaolia kwa sababu ya kuonewa kwa muda mrefu sasa. Ifike mahali wananchi hawa wasikilizwe, watu wanaumia kwelikweli, naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi saidiana na Wizara hii maana mliambiwa, Bunge lilitoa tamko la Wizara tano mkae kwa ajili ya kusaidia wananchi, mpaka leo hamjakaa, mmeweka vigingi wenyewe, wananchi waaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine, kuna dada yangu kutoka Arusha aliongelea kuhusu Loliondo, mgogoro wa Loliondo miaka 26 leo halina majibu Bunge, Serikali haina majibu, Loliondo wananchi wanaumia sana. Ifike mahali niungane na Mheshimiwa Mbunge aliyesema unda kamati malum kama ambavyo umeunda ia Tanzanite, ya madini mengine, ili tusaidie nchi hii kuwanusuru wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale juu kuna mfugaji mmoja anaitwa Julius Tisho amepoteza ng’ombe 240 ambao wameswagwa na wahifadhi kwenye Mbuga ya Selous, wakalipia risiti, hizi hapa kwa ajili ya faini, lakini mwisho wa siku pamoja na kulipa risiti hizo ng’ombe wale walipigwa risasi na wahifadhi, CD ninayo hapa nitakukabidhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua Wasukuma wameonewa, najua Wagogo wameonewa ambao ni wafugaji, Wamasai wameonewa ambao ni wafugaji, Wabarbaig, lakini wengine na Wakurya, itafika mahali tutaweka tamko na ninyi Chama cha Wafugaji mko hapa ndani, tufike mahali tuseme kwa sababu utalii unaathiri maisha yetu tufike huko Ulaya na Marekani, twendeni China na mahali popote duniani tuwambie kwamba tunawaombeni msije Tanzania kwa sababu mnapokuja Tanzania maisha yetu yanaathirika, tutaweza. Tukaeni pamoja, tuunganishe pamoja na sisi Wabunge tuko tayari kuitangaza Tanzania kwamba utalii huu unaathiri maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado hatujafikia hapo, lakini tutafikia mahali fulani tunaumia sana, inauma sana. Naombeni Serikali hii isikie kwa mara ya kwanza. Bahati mbaya kule Loliondo ambako 2015 ndilo Jimbo pekee Arusha ambalo mmechagua CCM watu wanaumia sana. Wafugaji nchi hii naomba sasa ifike mahali wasikilizwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru.
Ahsante sana.