Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu ahsante sana kwa kunipa dakika tano, ili nipate kuchangia. Ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwenye hii hotuba ya Waziri wa Maliasili nimeenda kwenye ukurasa wa 62, aya ya 5.4.5.2, kuhusu Idara ya Wanyamapori, akasema kwamba mradi na usimamizi endelevu wa ikolojia ya ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero na Mto Rufiji.

Sasa nimesimama hapa na kwa kukuomba sana ili kuzungumzia hilo suala kidogo ambapo kwenye kitabu chake ameongea kitu kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri nimealikwa kwenye vikao mbalimbali vya nishati na madini kwenda na wataalam wanaoshughulikia suala la Stieglers’ Gorge kule Rufiji, kuhusu kutuelimisha namna tutakavyopata umeme. Lakini wakiwa wametujumuisha watu wa Mkoa wa Morogoro, hususan Bonde la Kilombero kwa sababu wanasema kuna asilimia karibu 60 na zaidi za maji zinategemewa kutoka Kilombero kwenda kwenye lile bwawa la umeme. Pamoja na mpango huo, lakini Wizara hii pamoja na Wizara ya Nishati haizungumzii athari za wananchi zitakazotokana na uwekezaji huo mkubwa ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitiririke sasa moja kwa moja, mradi huu ndani ya Jimbo la Mlimba kuna kata zipatazo nane na vijiji vipatavyo 18 vinaenda kuathirika moja kwa moja na mradi huu, lakini mradi huu hauzungumzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo katika hizo kata na hivyo vijiji vipatavyo 18 kuna kilometa 359 inachukuliwa kwenye Kijiji cha Ngombo, chote kinaondolewa kwa ajili ya kutunza maji ili yaende Rufiji, Kata za Mlimba hizo. Katika Kata ya Mofu, Kijiji cha Idandu wanachukua ekari moja na Mwawala Kata wanachukua kilometa moja, Kata ya Idete wanachukua kilometa tatu Kijiji cha Miwangani, Kata ya Mofu wanachukua Kijiji cha Miomboni kilometa 13, Kata ya Kalenga Kijiji cha Mofu wanachukua kilometa 23, Kata ya Mofu wanachukua kilometa 31, Kata ya Ikwambi, Kijiji cha Ikwambi wanachukua kilometa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mchombe, Kijiji cha Lukolongo wanachukua kilometa mbili, Kata ya Mngeta wanachukua kilometa moja, Kata ya Chita, Chita JKT, wanachukua kilometa 74, Kata ya Melela wanachukua kilometa 27, Kata ya Kalenga Kero wanachukua kilometa 19, Kata ya Ching’anda Kijiji cha Udagaji wanachukua kilometa 37, Kata ya Chisano wanachukua kilometa sita, jumla ni Jimbo la Mlimba, ni kilometa 37. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule wanakochukua huko ndio tunakotegemea kulima, ndio tunakotegemea wafugaji wameingia wengi, wanafuga huko, tutakwenda wapi? Hawatuambii hawa watu wanakwenda wapi? Hiyo ni hatari ndani ya Jimbo la Mlimba, ni maumivu makubwa. Mradi huu hauzungumzii chochote kuhusu athari ya maeneo haya, hawa watu takribani karibuni 30,000 wanakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba majibu ya Serikali, hiyo ni hatari, eti kwa sababu tu kwa Stieglers’ Gorge, jamani hata mradi mzuri angalieni athari za wananchi wanazopata. Hiyo nimesema Jimbo moja tu, kuna Jimbo la Kilombero lenyewe, kuna Jimbo la Ulanga na Jimbo la Malinyi kote wanaenda kuathirika, si kazi yangu kusemea, watasema Wabunge wao.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni hatari. Watuambie Serikali sisi wanatupeleka wapi? Wafugaji wamejaa kule mnawapeleka wapi? Wakulima watalima wapi? Tutaishi vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mbinu mbadala ya kutusaidia sisi, naongea hivi kwa machungu makubwa, yaani sipati jibu, hali ni hatari, sijui tutaenda wapi sisi wananchi wa Mlimba? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kusema sana kwa sababu moyoni naumia sana pamoja mnacheka lakini sisi tunaenda kuathirika na sisi ni Watanzania hatuna barabara, umeme wenyewe hatuna, maji hatuna, hivi mnatufanyia nini sisi, tumewakosea nini nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ni mbaya ndani ya Jimbo la Mlimba, Serikali hebu hamieni kule mkaone watu wanavyoenda kuathirika na huo mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru sana.