Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia hoja hii ya Maliasili na Utalii ambayo ni muhimu sana. Kwa sababu ya muda nitakwenda moja kwa moja kwa utalii na vivutio vya utalii ambavyo viko jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwanza Mawaziri wote Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wameweza kuja katika Jimbo la Muheza na kuweza kuona vivutio vya utalii ambavyo viko maeneo ya Amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Amani kama walivyoona ni kwamba kuna mambo mengi sana ya vivutio vya utalii, acha pamoja na mambo ya kuwa na miti mirefu hapa duniani, pamoja na kuwa na majoka makubwa hapa duniani na mambo mengine mengi, lakini kitu kimoja ambacho Mawaziri hawa wameweza kukiona kule ni namna ya wananchi wa Fanusi maeneo ya Amani ambapo wanachuma/wanavuna vipepeo. Vipepeo ambavyo vinawaletea hela nyingi na kukuza uchumi sio Muheza tu na hata Mkoa mzima wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tatizo ambalo lilitokea kwenye uvunaji wa hawa vipepeo ni kwamba waliingia kwenye kundi la kuzuiwa kusafirisha vipepeo hivi nje ya nchi. Ni kwamba Serikali ilipiga marufuku kusafirisha wanyama pori hai nje ya nchi basi wakachukua na vipepeo. Lakini sidhani kama lengo la Serikali lilikuwa ni kuzuia vipepeo hawa kuzuia vipepeo hawa kusafirishwa nje ya nchi. Naamini kabisa Serikali ilikuwa na nia ya kuzuia wanyama wakubwa faru na wanyama wengine kwenda nchi za nje, lakini sio vipepeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wote wawili mliahidi mtalishughulikia suala hili, lakini siku zinavyozidi kwenda na wale wavunaji na wenyewe wanakata tamaa. Naomba suala hili Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-wind up jioni ulitolee maelekezo kwa sababu ni suala muhimu sana katika maendelezo ya uchumi pale Muheza, kwa sababu linaingiza fedha nyingi sana na pia uliahidi kuboresha yale maeneo kuwaboreshea wale wavunaji yale maeneo bado suala hilo bado Wakala wa Misitu hajalishughulika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo ni mgogoro wa muda mrefu pale Derema. Kuna wakulima ambao walikuwa kwenye hifadhi karibu 1,028 mgogoro huu ni wa muda mrefu tangu miaka kumi umeukuta na wote mlipokuja mliwaona wale wananchi walivyokuwa wanalalamika. Sasa hivi Muheza tumeanza kuwagawia viwanja kuwatoa pale wameshaondoka lakini tunawagaia viwanja eneo la Kibaranga ili waweze kuondoka vizuri. Lakini kuna fidia ambazo mapungufu ambayo wanadai na ni muda mrefu sana, sasa naomba suala hili pia Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-wind up jioni naomba ulishughulikie ili ulielezee/ulitolee tamko kwa sababu hata wiki iliyopita tu walikuwa hapa Dodoma hawakupata nafasi tu ya kuwaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni suala la tiki, sisi tunalima tiki, tunalima tiki katika Afrika tunaongoza, tiki yetu iliyoko pale ni the best in Africa. Sasa suala hili Serikali inaelewa kabisa, kulikuwa na mpango ambao ulikuwepo ambao wakulima wa tiki ilikuwa inagaiwa kwenye vitalu. Sasa vitalu ilikuwa inawawezesha wafanyabiashara ya Muheza au kutoka nje kununua vile vitalu na kuweka viwanda pale Muheza. Sasa baadae mmeanzisha mtindo wa mnada, mnada ambao anakuja tajiri mmoja ananunua vitalu vyote kiasi kwamba ilisababisha viwanda karibu 10/12 vyote vya wilaya ya Muheza kufungwa.

Sasa mlipokuja mliwaona na Mheshimiwa Waziri uliahidi kabisa kwamba suala hilo unalirekebisha na wananchi wa Muheza watafaidika sasa kuanza kununua vile vitalu. Naomba hiyo ahadi yako itekelezwe ili tuweze kuweka viwanda ambavyo ni viwanda vingi kwa ajili ya uchumi wa Muheza.

Mheshimiwa Spika, na mwisho ni suala la Maafisa Misitu. Maafisa Misitu kupewa madaraka ya kukata au kutoa vibali vya misitu katika hizi Halmashauri. Suala hili limetokea hapa juzi Muheza ambapo Afisa Misitu wa Muheza ameamuru karibu misitu mia na ushee kukatwa. Sasa suala hili ni kubwa sana ambalo Baraza la Madiwani liliamua kabisa kupendekeza hawa watu wasimamishwe kazi.

Sasa ni vizuri hawa Maafisa Misitu ili kuweza ku-protect misiti yetu na wenyewe wawe answerable moja kwa moja kwa Katibu Mkuu. Kama vile Rais alivyoamuru maafisa/ wahandisi wa maji na watu wa ardhi wote waripoti moja kwa moja kwa Waziri Mkuu nafikiri Mheshimiwa Rais amesahau hii kitengo cha misitu na wao waende moja kwa moja wawajibike ili waweze kushughulikiwa kwa haraka pale panapotokea matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu muda ni mdogo ningeomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana.