Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kwa juhudi kubwa ambazo Wizara yako imezichukua katika kuhakikisha kuwa tembo wa nchi hii wanalindwa na kubaki salama. Ombi langu kwako tafadhali naomba juhudi hizo za kupambana na ujangili zisiendeshwe kwa kukiuka haki za binadamu na dhuluma dhidi ya mali za wananchi kama vile ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, nimesikitishwa sana na kitendo cha kuacha hata kulitambua na kutaja mabaki ya mijusi yaliyopo Ujerumani ambayo yalichukuliwa jimboni kwangu. Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 6, 7, 8, 9, 10 na 11 wa kitabu chako, umezungumzia namna ya uendelezaji wa Mali Kale. Mheshimiwa Waziri imekuwaje uache hata kutambua tu kwamba kuna hayo mabaki yalichukuliwa na kupelekwa katika makumbusho ya Mali Kale kule Ujerumani. Kutokana na hali hiyo nimejiuliza maswali matano yafuatayo ambayo nimekosa majibu hivyo naomba majibu kutoka kwako:-

(a) Je, suala la mjusi huyo haulitambui?

(b) Serikali imeshindwa kabisa kulipatia muafaka suala hili?

(c) Serikali haina utashi wa kisiasa kurudisha na kutunza rasilimali hiyo ya kale?

(d) Majibu ambayo Serikali imekuwa ikiyatoa hapa Bungeni mara kwa mara kuhusu mijusi yote ni ya uongo?

(e) Serikali haitaki kuliendeleza eneo lile ambalo taarifa zinaonesha kuwa yapo mabaki mengine chini ya ardhi?

Mheshimiwa Spika, kama kuna suala ambalo Serikali ya CCM inaonesha udhaifu mkubwa katika kulinda rasilimali na maliasili ya nchi zetu ni huku kufeli kwenu kwa kushindwa kurudisha nchini mabaki yale, kushindwa kuliendeleza suala lile na au hata namna ambavyo nchi haipati kitu chochote kutokana na mabaki yale ya mijusi. Jambo hili linafedhehesha sana na kukianika Chama cha Mapinduzi kwani ni dhaifu katika kulinda, kutetea na kuhifadhi rasilimnali na maliasili za nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nakuomba basi uutangazie umma wa Tanzania kwamba Serikali imeshindwa kulipigania suala hili. Mnashindwa hata kuchonga barabara inayokwenda katika lile bonde ambalo watalii wamekuwa wakienda mara kwa mara kila mwaka. Shame to you guys.

Mheshimiwa Spika, kutokana na longo longo ya Serikali katika jambo hili, wananchi wa Mchinga tunaona ni dhana ile ile ya vitendo vya makusudi ya Serikali kudharau, kutothamini na kutojali vitu vya thamani vilivyopo Kusini hususan Mkoa wa Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Spika, ninaandika haya kwa uchungu mkubwa nikiwiwa na namna ambavyo Serikali inaacha kutumia mali kale hii katika ku-promote eneo husika, kukosa pesa za kigeni lakini pia kushindwa kujivunia rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Ahsante.