Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, misitu; (kwa nini ni muhimu kuwa na Chuo cha Misitu Mufindi) Pamoja na mchango huu, naomba kuwasilisha nakala ya kwa nini tuwe na Chuo kama Tawi la Chuo cha Misitu cha Olmotonyi. Nakala yangu imejieleza vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, mgao wa malighafi, ninashukuru Wakala wa Misitu kwa kuitikia kilio changu cha kukutana na wadau wa mazao ya misitu kabla ya msimu kuanza. Hata hivyo kama sehemu ya maoni ya wadau tulipokea tarehe 30 Aprili, 2018 mgao uzingatie pia kiwango cha uwekezaji na hivyo kwa waliowekeza mitaji mikubwa wepewe mikataba ya malighafi, mfano watu kama kina CF (Makambako), Hongwei International just mention some few ukiacha MPM na Sao Hill (ambao kiasi fulani wameyumba) kuna watu wanapewa kwa mkataba wakati wao hawavuni, hawana viwanda isipokuwa wanauza malighafi zao kwa wenzao, sio haki kabisa.

Ninashauri timu inayopita kukagua, itende haki na itoe maoni ya wanaostahili kupewa mikataba ya malighafi. Ikiwa mtu anatoa ajira direct employment ya watu 200 na kuendelea kwa nini asipewe mkataba? Mgao wa cubic meter 90,000 za Sao Hill ambao wameyumba mngefanya review ili walau one third ya mgao huo uende kwa wavunaji wadogo waliowekeza.

Mheshimiwa Spika, ushauri, ili kupunguza malumbano na mivutano isiyo na sababu Wizara itoe maelekezo kuwa na chama kimoja tu ambacho kitafanya kazi na Serikali pasipo mivutano maana mwisho wa siku wote ni wadau hivyo kuwa na chama kimoja ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, napongeza uongozi wa shamba la Sao Hill kwa ushirikiano na Mafinga Town Council.

Mheshimiwa Spika, why a need for a forestry college in the Southern Highlands of Tanzania and preferably in Mufindi District?

Mheshimiwa Spika, historia/background, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania imejaaliwa kuwa na hali ya hewa nzuri na udongo wenye rutuba, vyote kwa pamoja ni muhimu kwa kilimo cha miti ya misindano na mikaratusi. Wananchi wanaoishi katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa na Katavi wanajishughulisha kwa kiasi kikubwa na upandaji miti. Wilaya ya Mufindi iliyoyo katika Mkoa wa Iringa inaongoza kwa upandaji miti kitaifa. Wilaya hii pia ni nyumbani (is a home of) misitu ya Sao-Hill, msitu mkubwa wa pili Barani Afrika na wa kwanza nchini Tanzania. Ukubwa wa msitu huu ni zaidi ya nusu ya misitu yote inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania iliyopo sehemu mbalimbali kama Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Tabora, Mbeya na kwingineko. Msitu una eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 135,903. Msitu huu umesambaa katika tarafa nne kati ya tano za Wilaya ya Mufindi. Umesambaa katika tarafa za Kibengu, Ifwagi, Kasanga na Malangali.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1937 Waingereza walianzisha Chuo cha Misitu Mkoani Arusha kiitwacho Olmotonyi. Chuo hiki kililenga kuzalisha wataalam wa misitu katika fani mbalimbali. Wakati Chuo cha Olmotonyi kikifunguliwa msitu wa Sao-Hill ulikuwa katika hatua ya majaribio. Kuanzishwa chuo mikoa ya Kaskazini ilikuwa ni muhimu kwa sababu tayari kulikuwa na misitu kadhaa iliyokuwa imepandwa na Wajerumani na Waingereza kwa nyakati tofauti. Chuo hiki kiliwapa fursa Watanzania toka sehemu mbalimbali ya nchi kupata elimu ya misitu na hivyo kuajiriwa katika mashamba mbalimbali ya Serikali na katika Wizara ya Maliasili. Hata hivyo, kwa kuwa Serikali ya kikoloni ilikuwa inaona shida kuwagharamia watu wa mbali usafiri, kipaumbele kikubwa ilikuwa ni kuwasomesha watu wa Kaskazini ambao walikuwa karibu na chuo. Hivyo, tangu kipindi cha ukoloni Watanzania wengi wanaoishi mbali na Chuo cha Olmotonyi walikosa fursa ya kupata elimu ya misitu.

Mheshimiwa Spika, baada ya uhuru Serikali ilirithi chuo hicho na kukiendeleza ikiwa ni pamoja na kuanzisha elimu ya misitu Sokoine University of Agriculture (SUA). Baada ya Serikali kupanua shughuli za upandaji miti katika msitu wa Sao-Hill baada ya uhuru ilitambua kwamba haikuwa na maafisa misitu wa kutosha hasa wazawa.

Mheshimiwa Spika, miaka ya 1980 ikaanzisha chuo cha kutoa mafunzo ya elimu ya misitu ya muda mfupi katika makao makuu ya Sao-Hill (majengo bado yapo hadi leo) (Sao-Hill Forestry College). Kwa sababu ambazo hata hazifahamiki chuo kilihudumu kwa muda wa miaka saba tu hivyo hakikuendelea kutoa tena mafunzo. Kutoendelea kwa chuo hicho kimewanyima wananchi wengi wa maeneo yanayozunguka misitu na Mkoa ya jirani ya nyanda za juu kujipatia elimu ya misitu na hivyo kuwafanya wategemezi kwa NGOs chache zinazotoa huduma hiyo. Pia vijana wengi wa nyanda za juu wamekosa exposure ya elimu ya misitu na hivyo kuishia kufanya unskilled jobs ambao zinawafanya kulipwa ujira mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tuwe na Chuo cha Misitu Mufindi (Mufindi/Sao-Hill Forestry College, a Constituent College of Olmotonyi Forestry College). Tayari kuna majengo (madarasa, ofisi za walimu na mabweni) pale makao makuu ya Sao-Hill ambayo yalijengwa tangu miaka ya 1980 hivyo haitatumika gharama kubwa ya kuanzisha chuo kwa kuwa majengo ya kuanzia yapo. Kwa sasa majengo hayo wanaishi wafanyakazi na mengine wanafugia tu kuku na kuhifadhia mahindi.

Natambua jitihada za Serikali katika kuyafufua majengo hayo kwa msaada wa watu wa Finland ili yatumike kutoa mafunzo kwa wakulima wa miti wadogo wadogo. Hata hivyo, hii haizuii majengo hayo kutumika kama chuo kishiriki cha Chuo cha Misitu cha Olmotonyi kwa sababu wananchi wanaopata mafunzo yatakuwa yanatolewa kwa muda mfupi tu (kwa uelewa wangu). Hivyo, kuwa na chuo kitakuwa ni msaada mkubwa hasa kwa vijana wengi wanaotoka maeneo yanayozunguka msitu na hata nyanda za juu katika mikoa tajwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi tarafa zake nne kati ya tano zimezungukwa na misitu na hivyo hii ndio shughuli yao kubwa ya kiuchumi kwa sasa. Kuwa na chuo kitavutia vijana wengi kusoma ili kupata elimu ya misitu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi ina wawekezaji wengi wakubwa kwa wadogo waliowekeza katika kilimo cha miti. Wawekezaji hawa wanatakiwa kuajiri watu wenye weledi katika mashamba yao. Pia wanahitaji wavunaji wenye elimu ya kuvuna misitu kitaalamu zaidi. Kuwa na chuo Mufindi kutafungua fursa mpya za ajira kwa vijana wengi ambao watapata mafunzo kwa ngazi mbalimbali za cheti na diploma.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi ndio mwenyeji wa msitu mkubwa zaidi nchini na wa pili Afrika. Eneo kubwa la ardhi ya wananchi lilichukuliwa ili kupisha uwekezaji huu. Kuwa na chuo Mufindi ni njia mojawapo ya Serikali kutoa fadhila na kudumisha mahusiano mema kati ya wananchi wa Mufundi na Sao-Hill/Serikali kwa kuwa vijana wao watapata elimu ya misitu inatakayoinufaisha jamii nzima inayozunguka mradi na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, vijana wengi wa Mufindi hawaajiriki katika mashamba ya miti na viwanda vya kupasua mbao. Wengi wao wanaajiriwa katika kazi ambazo sio za kutumia utaalam kama kusukuma magogo, kuzima moto, kupanda miti na kusafisha mashamba. Hii imejenga matabaka kati ya wenyeji wengine na hivyo kujiona kama hawathaminiwi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, ni moja ya ahadi zilizowahi kuahidiwa tangu kipindi cha mkoloni wa kiingereza na kurudiwa tena na Serikali yetu baada ya uhuru. Wakati wanawashawishi wananchi kuhama ili kupisha mradi wa Sao- Hill wananchi waliahidiwa vitu vingi ikiwa ni pamoja na ajira, chuo cha misitu na mengine. Ahadi hiyo ilianza kutekelezwa miaka ya 1980 baada ya kuanzisha chuo pale Sao-Hill lakini hakikudumu hadi leo hii yamebaki majengo tu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mufindi ina eneo la kutosha na hali ya hewa nzuri. Vilevile uwepo wa msitu mkubwa, viwanda vya kuchakata magogo vikubwa na vidogo pamoja na kiwanda cha karatasi vinaifanya Wilaya kuwa sehemu nzuri hasa kwa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, relevance ya kuwa na chuo eneo tofauti na Mufindi kama ilivyo sasa Arusha kwa sasa haipo kwa kuwa hakuna viwanda vya karatasi, wala viwanda vya kutosha kwa mafunzo ya vitendo na pia eneo hilo sio rafiki kwa kilimo cha miti kwa sasa kwa kuwa hawana ardhi ya kutosha hivyo manufaa yake kwa jamii inayokizunguka chuo ni ndogo ukilinganisha na manufaa ambayo wanaweza kuyapata wakulima wa miti wa Mufindi pamoja na wa Nyanda za Juu kwa ujumla ambao ndio wadau wakubwa wa misitu kwa sasa.