Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, naomba kufanya mabadiliko ya usajili wa kijiji cha Sibwesa kwenye karatasi yangu niliyochangia kwa maandishi badala ya kusajiliwa mwaka 1967 sahihi ni kuwa Kijiji cha Sibwesa kilisajiliwa mwaka 1975 na hati ya usajili wa kijiji hicho kusainiwa tarehe 20/5/1976 hivyo mgogoro huu una zaidi ya miaka 31.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri, nawapongeza watendaji wote wa Wizara hii naunga mkono hoja. Pia nampongeza Waziri na Naibu Waziri wake kwa jinsi wanavyoweza kushuka na kupokea ushauri na maoni wanayopewa na wadau wa maliasili na utalii mfano kundi la uhamasishaji wa utalii wa ndani uitwao Utalii 255.
Mheshimiwa Spika, Waziri na Naibu Waziri kwa wakati mbalimbali walipata fursa ya kuzungumza na wadau hao.
Katika suala zima la uwindaji, nashauri muda wa kuwinda unapofika taarifa itolewe kwa uwazi kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Taarifa hiyo ieleze muda wa kuwinda, gharama zinazotakiwa kulipwa, aina ya silaha zinazoruhusiwa kutumika na kadhalika. Kwa sasa taarifa hizo hazipo wazi kwa wananchi ambao wangependa kupata kitoweo chenye ladha tofauti kinachopatikana nchini.
Mheshimiwa Spika, katika nchi jirani ya Kenya kuna ukumbi wa burudani mjini Nairobi unajulikana kwa jina la Carnival, kuna aina tofauti za nyama choma kutoka mbugani mfano nyati, nyumbu, swala, mbuni na kadhalika. Huku kwetu jambo hilo halipo hivyo Tanzania tunafanya utalii na kuwatunza lakini wenzetu wanatafuna!
Mheshimiwa Spika, suala la maeneo ya hifadhi na changamoto zake, kazi za ulinzi katika maeneo hayo inafanyika vizuri sana. Naomba ubinadamu ufanyike, kuna tofauti kubwa ya majangili na wananchi wanaoingia katika hifadhi kupata dawa, kupata miti ya kuni au kutengeneza mipini ya majembe na mashoka. Ukweli wananchi hao wanapokutwa huko adhabu wanayoipata ni kubwa kuliko kosa walilolifanya. Wengine wamepata vilema hata kupoteza maisha. Naomba elimu itolewe zaidi kwa wananchi ili kuwaepushia na adhabu hizo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu uanzishwaji wa vituo vya utalii wa ndani katika mikoa mbalimbali nchini, vituo hivyo vitasaidia kuleta hamasa na ushindani baina ya Mkoa na Mkoa, utasaidia wananchi kusafiri umbali mdogo ili kufikia vituo. Kama malipo yatawekwa kidogo itasaidia wananchi wengi kutembea na kuingiza mapato kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika uhamasishaji wa utalii wa ndani, kuwe na utaratibu wa kuwazoesha watoto na wanafunzi kutembelea vivutio mbalimbali na kuelezewa umuhimu wa kutunza tunu zetu na kuwa wazalendo, watoto hao na wanafunzi wataendeleza tabia nzuri ambayo itasaidia kuondoa au kupunguza mambo ya ujangili na uvunjaji wa sheria na kuisadia katika kulinda tunu zenu.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara hii kwa kuitangaza nchi yetu ndani na nje ya nchi. Naipongeza kwa kuingizia Serikali mapato kupitia vivutio mbalimbali, nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante.