Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja kwa njia ya maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tatizo la GN kutokutambulika katika hifadhi nyingi nchini inaongeza migogoro isiyo ya lazima kati ya wananchi na hifadhi, utatuzi wa haraka unahitajika. Wahifadhi/askari wanyamapori wanatumia GN kama fursa ya kuwaumiza wananchi kwa kigezo kwamba wameingia kwenye hifadhi na kuwalipisha faini zilizo onevu.

Mheshimiwa Spika, bado Wizara haijaweka dhamira ya dhati kwa kuimarisha utalii wa fukwe hapa nchini kama ilivyo nchi za Mauritania/Morocco na nchi nyingine. Hapa nchini fukwe zetu kama Coco Beach ambazo zinatumika kuuza mihogo kwa nini Wizara isiziboreshe kwa kujenga hoteli za kitalii, beach za kisasa, hasa watalii wanapotua Dar es Salaam wakati wakisubiri kwenda kwenye hifadhi wakapumzika beach, wakaongeza mapato badala ya ilivyo sasa kwamba wanabaki hotelini wakisoma vitabu huku wakisubiri kwenda kwenye hifadhi?

Mheshimiwa Spika, malipo kwa wananchi wanaouawa na tembo au wanyama wengine ni kidogo, ipo haja Sheria ya Fidia kuletwa Bungeni ibadilishwe. Kwa sasa kifuta jasho ni kati ya shilingi 100,000 ni kidogo ikilinganishwa na thamani ya utu/mwanadamu. Tembo akigongwa na gari faini ya USD 1500 zaidi ya shilingi milioni 30 kwa tembo mmoja, lakini ukilinganisha mtu akiuawa na tembo eti kifuta jasho shilingi 100,000 sio sawa kabisa.

Mheshimiwa Spika, Wami Mbiki ni potential kwa hifadhi, wanyama wapo wa kutosha, Sweden imewahi kusaidia hifadhi ile na Mwenyekiti wake ni Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Kwa nini Wizara isiendeleze hifadhi hii ambayo ina rasimali za wanyama za kutosheleza? Sasa hivi wananchi wameingia kwenye hifadhi wanalima, wanawinda wanyama na wanakata miti, sasa badala ya hifadhi imegeuka mashamba. Wanyama wanavamia makazi ya wananchi kula mazao kwa sababu hifadhi inakosa sifa. Tunaitaka Serikali kurudisha hifadhi hii kwenye hadhi yake ili kuongeza kipato kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika Hifadhi ya Mikumi wanyama wanaendelea kuuawa kwa kugongwa na magari. Ulikuwepo mpango wa barabara ya Morogoro – Mikumi ku-divert Kilosa mpaka Mji wa Mikumi. Kwa nini mpango huu hautekelezeki?

Mheshimiwa Spika, kuzibwa kwa shoroba; Hifadhi ya Saadani kupitia Wami Mbiki kwenda Mikumi hadi Selous kuna wanyama wanatembea kwa mfano tembo wanatoka Saadani hadi Selous, lakini shoroba zimezibwa. Mbaya zaidi Serikali imejenga majengo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, wameziba shoroba. Vilevile Serikali hiyo imevunja nyumba za wananchi Mtaa wa CCT Mkundi kwa madai kuziba shoroba wakati majengo ya Serikali Wilaya ya Mvomero yapo, hayajavunjwa.