Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, sambamba na kutoa pongezi lakini kuna tatizo kubwa la TFS na Jeshi la Wanyamapori. Wilaya ya Uvinza ina Hifadhi za Ilunde, Mahale pamoja na Ipuguru. Vilevile ina Msitu wa Pakunda Pachambi na Msitu wa Masanza.

Mheshimiwa Spika, nianze na Hifadhi ya Mahale, hifadhi hii imepakana na vijiji viwili, Kijiji cha Simbwesa na Kijiji cha Kalilani. Kijiji cha Kalilani kilisajiliwa tangu mwaka 1995 kwa Namba 244 na Kijiji cha Simbwesa kimesajiliwa kisheria tangu mwaka 1967.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tatizo kubwa na DC wa Uvinza kwa kushirikiana na mhifadhi pamoja na watumishi wa Hifadhi ya Mahale. Mheshimiwa DC alienda Kalilani na kuwafokea wazee kama watoto wadogo. Naye Mheshimiwa DC wa Kigoma Mjini Ndugu Hanga alikwenda Kijiji cha Simbwesa akawatukana wanakijiji na kuwatishia kuwa Serikali hii ya Awamu ya Tano haitaki mchezo na mtu na kutoa amri kwa askari na askari wa hifadhi kuwa waweka vigingi ndani ya Kijiji cha Simbwesa na kuwatishia kuwaweka Serikali ya kijiji ndani.

Mheshimiwa Spika, ninavyoona mimi kama mwakilishi wa wananchi hawa wa Vijiji vya Kalilani na Simbwesa sina mahusiano kabisa na Hifadhi ya Mahale kwa kuwa hata wakiwa na suala na vijiji hivi wanatakiwa kunishirikisha mimi, mimi kama mwakilishi wa wananchi badala yake wanatoa hongo kwa viongozi wa Wilaya. Niwe wazi Mheshimiwa DC Mwanamvua Mlindoko ni kero, kero, kero kubwa kwenye suala la utatuzi wa migogoro.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijiji hivi viwili vya Kalilani na Simbwesa vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria, kwa nini hifadhi walazimishe kuweka vigingi ndani ya eneo la vijiji? Nimuombe Mheshimiwa Waziri watoe vigingi ndani ya vijiji hivi ili wananchi waweze kupata maeneo ya kulima na kufanya shughuli zao za kimaendeleo. Kwa kuwa kuna Kamati ya Waziri Mkuu hivi vijiji vya Kalilani na Simbwesa vimo niombe basi kauli ya Serikali itolewe kuwaachia wananchi maeneo yao. Mgogoro huu una zaidi ya miaka 46.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Msitu wa Masito, tunao msitu huu ambao umekwisha kabisa na hauna wanyama wala miti. Tulipata fedha za ujenzi wa barabara ya Basanza – Lugofu Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.

Tangu tupewe fedha za ujenzi wa barabara hii inayopita ndani ya Msitu wa Masito ni miezi 12 sasa tunashindwa kuijenga barabara hii kwa kigezo cha kuzuiliwa na Mkuu wa TFS wa Uvinza.

Mheshimiwa Spika, ni barabara ngapi zinapita ndani ya hifadhi za Selous, Ngorongoro Serengeti na kadhalika? Kwa nini sisi Uvinza tusiruhusiwe kuijenga hii barabara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Kata ya Basanza? Niombe Mheshimiwa Waziri tupewe kibali kabla pesa hazijarudi Hazina.

Mheshimiwa Spika, Msitu wa Pakunda Pachambi, msitu huu uko chini ya Halmashauri ya Wilaya, lakini changamoto tuliyonayo ni watu wa maliasili kuweka vigingi hadi kwenye vyoo vya wananchi na kusababisha wananchi wa Kata ya Nguruka, Kitongoji cha Humula na Kitongoji cha Reli Mpya kukosa maeneo ya kulima, kujenga zahanati pamoja na kujenga taasisi muhimu za Serikali. Tuombe pia kibali cha kugaiwa ekari kadhaa kwa vitongoji hivi pamoja na Vijiji vya Chagu, Mganza nan Nyangabo ili wapate maeneo ya kulima na kujenga mahitaji yao muhimu.

Mheshimiwa Spika, tuiombe Serikali itupe pesa za kujenga barabara ya kutoka Rukoma hadi Kalilani ili kukuza utalii. Watalii wanapata shida sana ya kutumia boti wakati wa upepo mkali. Tuna vita Rukuga, ni lazima barabara hii ijengwe na TANAPA. Tunaishukuru TANAPA kwa kujenga madaraja mawili, lakini madaraja haya hayana tija kama barabara haitojengwa.

Mheshimiwa Spika, mwisho nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Waziri kwa kutupa Msitu wa Masito – Ugala kwani kwa kupata msitu huu Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza itaongeza mapato. Pia niombe Mheshimiwa Waziri atusaidie gari kwa ajili ya Idara ya Maliasili kwa ajili ya kuijengea ufanisi idara hii. Baada ya kuchangia haya niendelee kumpongeza Waziri na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.