Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb), Naibu Waziri Mheshimiwa Hasunga na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha hotuba yao ya bajeti ili tuweze kuijadili. Nimpongeze Waziri kwa kuongeza pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia tano, hongera sana.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa ujenzi wa viwanja vya ndege nchini kikiwamo Kiwanja cha Ndege cha Nduli, Mkoa wa Iringa. Pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inakwenda katika Hifadhi ya Ruaha. Tunaamini kabisa miundombinu itakapokamilika Mkoa wa Iringa utakuwa kitovu cha utalii, pia Nyanda za Juu Kusini kutafunguka kiutalii na pato la mkoa na nchi litaongezeka.

Mheshimiwa Spika, kuvibaini vivutio zaidi vya utalii vilivyoko nchini na kuviendeleza, nilikuwa naomba Serikali itueleze mpango maalum walioupanga kwa ajili ya kuvibaini vivutio vilivyopo katika nchi yetu kwa ajili ya kuiendeleza na kuvitangaza ili viwe na tija na visaidie kuongeza pato la Taifa. Katika Mkoa wetu wa Iringa kuna vivutio vingi sana vya utalii ambavyo bado havijapewa kipaumbele katika kuvitangaza kama vile Fuvu la Kichwa cha Mkwawa, Jiwe la Hangilongo (jiwe lililokuwa linaongea), sehemu waliyokuwa wananyongwa watumwa (vitani), sehemu waliyopigania uhuru alipokuwa anaishi Mandela, Lugalo sehemu lilipo kaburi la Nyundo na vingine vingi sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu elimu ya utalii, nilikuwa pia nataka kujua mpango mkakakti wa kuwapatia elimu wananchi wa Mkoa wa Iringa. Tunaipongeza Serikali kwa uzinduzi wa utalii katika mkoa wetu kama kitovu cha utalii wa Nyanda za Juu Kusini. Ni imani yangu kabisa kupitia utalii wananchi wetu watajiajiri. Kama wataandaliwa katika utalii kuna ajira nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa ununuzi wa ndege ambazo nina imani utaongeza utalii katika mikoa yetu na nchi yetu. Tulikuwa tunaomba huu mradi wa Regrow unaokuja kukuza utalii Nyanda za Juu Kusini uendelee kusaidia utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa hii ya Kusini. Mradi huu uendelee ku-support maonesho haya yaliyozinduliwa Iringa ya Karibu Kusini ambapo imefanyika kwa miaka miwili kwa Mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Katavi, Ruvuma na Rulewa.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru mradi huu utajenga jengo kama Kituo cha Utalii eneo la uliokuwa Msitu wa Kihesa, Kilolo Iringa. Nilikuwa naomba watakapojibu watujulishe makao makuu ya mradi huu ni wapi? Kwa kuwa mradi wa Spanest unaishia mwezi wa sita, je, utaongezewa muda tena? Kwa kuwa sasa mkoa wetu utakuwa kitovu cha utalii, je, Serikali imejiandaaje kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi ili waweze kujiajiri kupitia utalii?

Mheshimiwa Spika, Mkoa wetu wa Iringa una eneo la uwekezaji lililopo katika Msitu wa Kihesa, Kilolo ekari 640 za eneo zima, lakini ekari 230 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilipatiwa kuendeleza katika utalii. Tunaomba Serikali ilete rasilimali fedha na rasiliamali watu ili kusaidia kuutunza msitu huo kwa eneo lililobaki.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Iringa katika Halmashauri zote kuna vivutio vya utalii, pamoja na kuwa Afisa Wanyapori, Dada Hawa Mwechaga anafanya kazi nzuri sana za utalii pia Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Amina Masenza anahamasisha sana utalii, tunaomba Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikiane na Wizara ya TAMISEMI ili kuhakikisha Halmashauri inakuwa na Afisa Utalii ili vivutio vilivyomo katika Halmashauri zetu vitumike kama vyanzo vya mapato. Niendelee kumpongeza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mito yenye mamba, niendelee kumpongeza, naomba kujua Serikali inasaidiaje mito yenye mamba hasa katika Mkoa wa Iringa? Wanasaidiwe kuvuta maji ili wananchi wasiendelee kuuawa na kupata ulemavu?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.