Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbeya Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza naomba niwashukuru sana Wanambeya wenzangu kwa kusimama na mimi nilipofungwa kisiasa kwenye Gereza Kuu la Luanda, Mbeya, pia nawapa pole kwa wao kufungwa kisaikolojia. Nawashukuru pia Watanzania wote ndani na nje ya Tanzania kwa kulaani kufungwa kwangu kiholela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Wabunge wote hasa wa Upinzani, kwa support kubwa waliyotoa, lakini pia hata upande wa CCM, japo kuwa mliogopa kuja kuniangalia lakini salamu zenu nilizipata; na source ya hofu yenu wote tunaelewa, lakini nimshukuru mzee, Profesa Mark Mwandosya, aliwawakilisha upande wa CCM kwa kuja kunitembelea jela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niwapongeze Mheshimiwa Stephen Masele na Mheshimiwa Mboni Mhita kwa nafasi walizochaguliwa kwenye Bunge la Afrika. Bunge letu limejiunga kwenye Vyama vya Kibunge vya kimataifa kama CPA, PAP, ACPEU, IPU na kadhalika, lakini wote tunafahamu ni kwamba hatushiriki vyema na tatizo sijajua ni nini. Hata hivyo, kama hatujui umuhimu mbona tunafurahia matunda ya ushindi wa Mheshimiwa Masele na Mheshimiwa Mboni Mhita wakati wote tunajua hata kwenda huko walijigharamia wenyewe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja, na nitaanza na masuala ya sera za mambo ya nje (foreign policy). Mheshimiwa Waziri wakati anaanza kuchangia alisisitiza sana kwamba mwelekeo wetu wa foreign policy hatutakubali kuingiliwa wala kuchaguliwa marafiki. Naomba nimhakikishie na kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, najua ana weledi katika nyanja za kimataifa, kwamba sisi kama Tanzania hatujawahi kuburuzwa wala kuchaguliwa marafiki tangu enzi ya Mwalimu Nyerere na ndiyo maana tulikuwa member wa nchi zisizofungamana na upande wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ile Non-Aligned Organization (movement) sisi tulikuwa ni member muhimu sana na tulitambulika kimataifa. Tanzania ilikuwa inaheshimika kimataifa kwa mambo kadhaa. Kwanza na muhimu tulikuwa na sera ya kutetea wanaokandamizwa duniani; mfano South Africa, Mozambique, tuliwasaidia sana mpaka kufikia kujiondoa katika makucha ya apartheid na wale Mozambique kupata uhuru wao kutoka kwa Wareno.
Mheshimiwa Naibu Spika, sera hizo hizo tulizokuwa nazo dhidi ya South Afrika na Mozambique ndizo tulisimamia Sera yetu ya Mambo ya Nje kwa Palestina na Sahara ya Magharibi. Mwalimu Nyerere alifuta uhusiano wa kibalozi na Israel kwa ku-support struggle ya Wapalestina kudai uhuru. Sasa tujiulize leo hii tunaenda kufungua Ubalozi Israel, je, ile course ya Mwalimu ku-support uhuru wa Palestina imefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu ukiangalia ni kwamba hali imezidi kuwa mbaya Wapalestina ndani ya Gaza na maeneo mengine yanayokaliwa kimabavu wanazidi kuuawa kila siku kadri Israel inavyoongeza uwezo wake wa kijeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika Mwalimu Nyerere na sisi kama Taifa tulifuta uhusiano na Morocco kwa ku-support kudai haki kwa Sahara ya Magharibi chini ya POLISARIO. Sasa leo tumeacha sera zetu dhidi ya Morocco kwa ahadi ya kujengewa uwanja wa mpira stadium, tunajivunjia heshima kwa ahadi ya kujengewa uwanja wa mpira ambao Mheshimiwa Mkapa amejenga pale Dar es Salam uwanja wa mpira kwa support ya Wachina bila kuuza nchi wala bila kukiuka misimamo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika Mheshimiwa Waziri na Bunge hili Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa huko alikolala kaburini Mwitongo anageuka geuka kwa jinsi Taifa hili linavyokwenda sasa hivi katika sera ya mambo ya nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, diaspora; naomba sana Mheshimiwa Waziri tuache siasa kwenye maisha ya Watanzania wenzetu. Ni lini Serikali itatambua Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora)? tuache kutoa ahadi kila tena nasikia mwakilishi yuko hapa, I hope amekuja ile straight hakuja kisiasa kwa sababu wenzake anaowawakilisha wanalia sana kule, sisi tumekaa kule, tuna mawasiliano kule, tunajua kilio chao, hata hapa kwenye simu nina mawasiliano ya kutoka diaspora baada ya wao kujua kwamba leo kinaenda kuzungumzwa nini, wametoa nao changamoto zao wanataka tuzizungumze humu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanachotaka watu wa diaspora ni kuruhusiwa uraia pacha, kama ambavyo uraia pacha uko katika nchi nyingine. Wapewe uraia pacha ili waweze kushiriki kujenga uchumi na si tu makongamano mara kuwaalika Zanzibar, mara kuwaalika wapi. Wakati umefika turuhusu sasa uraia pacha ili watu hawa waweze kushiriki katika uchumi wa nchi. Hawa watu wa diaspora sasa wanaanzisha kitu kinachoitwa Tanzania Global Diaspora Council (TGDC). Sasa tusije sisi na mawazo yetu tunataka kuwasaidia vipi sijui kuwashirikisha vipi, wale wana exposure wamefunguka, wanajua wanachokitaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa itakiwa tutambue na Serikali iniambie imejipangaje kufanya kazi hiki chombo cha diaspora cha Tanzania Global Diaspora Council ambacho kinaenda kuanzishwa na hawa Watanzania wenzetu katika kusaidia kuji-integrate kwenye masuala ya nchi yao ambayo wanaipenda. Kwa sababu, otherwise mtu kama ameshapata uraia wa wapi anaweza akaamua kuendelea na maisha na kusaidia kuleta maendeleo kwenye yale maeneo wakati tungewapa fursa wangeweza kafanya hivyo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna ajenda ya pamoja kwa diaspora. Mheshimiwa Mzee Kikwete alipokuwa anaenda nje aliwashawishi experts wa Tanzania huko nje warudi kujenga nchi yao; lakini utawala huu uliofuata ukawageuka na kuanza kuwanyanyasa mfano ni yule mama Julieth Kairuki wa TIC. Mheshimiwa Dkt. Kikwete alikwenda kumshawishi South Afrika ameacha kazi yake nzuri, ameacha kila kitu kilicho kizuri kinachoendana na weledi wake amekuja nyumbani kusaidia kujenga nchi, lakini leo unamwambia kwamba hatuwezi kukulipa huo mshahara mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi alikuja kwa makubaliano gani kutoka South Afrika anakuja hapa tunakuja tunawageuka? Wengine waliambiwa warudi kujenga nyumbani na kuwekeza wakaanza kurudi kwa wingi wakajenga majumba, wakafungua biashara. Leo hii Waziri wa Ardhi hawa si raia halali, kwa hiyo mali zao zitataifishwa tunawatia woga Watanzania wezetu hawa wakati walikuwa wangeweza kushiriki vizuri sana katika masuala yetu ya uchumi na kujenga nchi.
T A A R I F A . . .
MHE. JOSEPH. O MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ilifaa kabisa kubakisha ubalozi wetu pale Cairo, Egypt, kwa sababu ule ubalozi ulikuwa neutral na ulikuwa unaweza ku-harmonize pande zote yaani Palestina na Israel mpaka mambo yao yatakapokaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ni top diplomat wa nchi, suala la kusafiri bado ni muhimu, labda kama ana tatizo la kiafya. Tena anapokwenda nje anaweza kutumia lugha ya Kiswahili kwa sababu Rais wa Xi Jinping wa China kila anakokwenda anaongea Kichina japokuwa ni msomi aliyesomea Marekani. Yeye amesomea chuo kikuu na elimu zake za juu Marekani anazungumza Kiingereza vizuri, lakini kila anapokwenda anazungumza lugha ya Kichina; kwa hiyo tena tutakuwa tunaitangaza na lugha yetu ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama tatizo ni gharama mbona anatuma delegations? Mara Makamu wa Rais, mara Waziri Mkuu nao wanatumia gharama kwa sababu hawaendi kule kwa miguu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hatuendi UN, hatuendi Davos, hatuendi Common Wealth. Common Wealth ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi (Head of States), lakini sisi tunatuma wawakilishi wakati kule kuna fursa za kiuchumi na biashara. Rais Uhuru Kenyatta ametumia vizuri sana fursa za kiuchumi na kibiashara kwa nchi alipokwenda Common Wealth, hali kadhalika Rais Ramaphosa wa South Afrika pia alitumia huo kukutana na investors wa kutosha aka-archive miradi ya takribani Rand trilioni 1.2 kwa ajili ya nchi yake; ndizo faida ya majukwaa haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Rais kusafiri haiepukiki, ni muhimu na kama alivyonukuliwa mzee Kikwete Rais aliyepita kwamba kusafiri kulimsaidia sana, mkaa bure si sawasawa na mtembea bure; hii alisema wazi. Kwa hiyo kusafiri ni muhimu sana, kwa sababu Mabalozi tunaowachagua huko hawatusaidii kwa sababu tunachagua Mabalozi wetu kisiasa bila kuangalia weledi. Aidha, tunawapa ubalozi watu kama zawadi au kuwa- control.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Slaa tumempa zawadi kwa kazi aliyoifanya 2015 katika uchaguzi, tumempa ubalozi, lakini Dkt. Emmanuel Nchimbi tumempa ubalozi Brazil kum- control ili awe mbali kudhibiti ushawishi wake ndani ya Chama cha Mapinduzi. Haya ni mambo ambayo yako wazi na yanaeleweka kabisa. Sasa hawa ni shida sana kusimamia diplomasia ya uchumi, watakuwa wanaleta siasa pekeyake na iko hiviā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisimamishwa kidogo. Diplomasia ya uchumi bila stability ni shida. Tunawatisha wawekezaji, tunapiga risasi Wabunge, tunafunga ovyo Wabunge. Wawekezaji wa nje walifuatilia haya mambo. Wakifuatilia haya mambo inakuwa wanasita sasa kuja kuwekeza kwa sababu hakuna mwekezaji anayetaka kuweka kwenye nchi ambayo haiko stable, haina amani na usalama.