Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa na mimi kuchangia Wizara hii na kwa haraka kabisa napenda kuipongeza Wizara kuanzia Mheshimiwa Waziri, Naibu, Makatibu Wakuu pamoja na Mabalozi ambao ni Wakurugenzi wanaoongoza idara mbalimbali katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi hizi haziwezi kwenda tu hivi hivi zitaendana na ukurasa wa 25 ambao unaelezea misamaha ya madeni ya nje. Hii yote ni jitihada za kazi nzuri ambao Wizara pamoja na Wakurugenzi na Mabalozi kote waliko wanaifanya na ndiyo maana tumeweza kusamehewa baadhi ya madeni katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia na mimi nichukue nafasi hii kuwapongeza wenzangu Mheshimiwa Masele na Mheshimiwa Mboni Mhita kwa nafasi walizochaguliwa. Hii inaendelea kuthibitisha kwamba Taifa bado linaendelea ku- maintain heshima yake katika nyanja za kidiplomasia Afrika na dunia kwa ujumla. Kwa hiyo tuendelee kusonga mbele na kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa sababu si haba niseme kidogo, sina nia ya kumjibu ndugu yangu Mheshimiwa Mbilinyi lakini niseme tu kwamba, katika nyanja za kidiplomasia nchi kama Algeria nitawapa mfano ndiye supporter mkubwa wa POLISARIO Chama cha Ukombozi wa Sahara. Hata hivyo, Algeria hii ambao POLISALIO Makao yake Makuu yako Algeria ina mahusiano (bilateral) na Morocco. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kum-support mtu fulani haikuzuii wewe kufanya mahusiano na yule mtu mwingine as far as you have interest in that particular mahusiano. Kwa hiyo si jambo geni, hata South Afrika ni supporter mkubwa wa POLISARIO, ndio wanao finance POLISARIO, lakini wana mahusiano bilateraly na Morocco. Kwa hiyo, unaangalia wewe una interest gani na misimamo yako inabaki vile vile; niliona ni muhimu kulisema hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nipende pia kupongeza kwa kufunguliwa hizi balozi zetu nyingine, sita na Mheshimiwa Waziri amesema mabalozi wamesha kwenda. Pia kama ambavyo Kamati ilikuwa imeshauri kuwa na umuhimu wa kufungua zile tunaita General Consulate katika Miji ya Lubumbashi na Guangzhou. Nimeona kwamba Serikali imezingatia ushauri wa Kamati na Wabunge kwa ujumla na kwamba sasa tunakwenda kufungua General Consulate katika hiyo miji ambayo iko strategically kibiashara kwa Taifa letu, kama hiyo Lubumbashi na Guangzhou.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo ambayo ya kupongeza na yanaonesha kwamba Serikali inachukua mawazo yetu Wabunge na kuyafanyia kazi. Kwa hiyo niwasihi tu kama Serikali twende kwa haraka katika kulitekeleza kwa vitendo jambo hili ambalo mmelichukua kutokana na ushauri wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie; Mheshimiwa Waziri amekuwa kwenye nyanja hii ya diplomasia, atakuwa anafahamu kwamba sasa hivi kuna reform inaendelea UN Security Council, kwamba na sisi kama Afrika tungependa tupate nafasi katika sehemu ile ya zile kura tano za veto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Taifa nimwombe Mheshimiwa Waziri tujipange vizuri na hatua mojawapo ya kujipanga ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunapeleka maafisa katika vituo vyetu vya ubalozi. Tukiwa na maafisa wa kutosha maana yake ni kwamba ushiriki wetu utakuwa ni madhubuti. Kuna vituo ambavyo ni multilateral stations, Mheshimiwa Waziri anafahamu, kama New York, anafahamu pale kuna Kamati sita ambazo kila Kamati inapaswa iwe na afisa kwa ajili ya kutetea maslahi mbalimbali ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano wa Kamati ya tano, Mheshimiwa Waziri anafahamu kabisa kwamba baada ya kufunga ICTR tuko kwenye transition kupitia ile Mechanism For International Criminal Tribunala. Katika bajeti ya 2018/2019 mapendekezo yalikuwa kwamba tupate nadhani dola milioni mia mbili kumi na tano. Hata hivyo, kutokana na kukosa ushawishi wa kutosha, Waziri anafahamu mataifa makubwa yamepunguza tumepata dola milioni 88.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jitihada za baadhi ya mataifa kuhakikisha kwamba hata ikiwezekana ile iliyokuwa ICTR ifungwe ihamie The Hague. Sasa jambo hili likifanyika ni hasara kwa Taifa letu kwa sababu, imagine kama mahakama ile inapangiwa dola milioni 215 maana yake ni kwamba hata kiuchumi zitaongoza mzunguko katika Taifa letu, siyo tu pale Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Nanibu Spika, pia jitihada hizi inabidi tujipange kikamilifu kuweka kukabiliana nazo; kwa nini; kwa sababu wa uwepo wa ICTR pale Arusha ni legacy kubwa kwa Taifa letu katika dunia. Sasa jitihada hizi kama hatutahakikisha tunapeleka watumishi wa kutosha katika balozi zetu, maana yake ni kwamba hata ushiriki wetu katika vyombo mbalimbali especial hizi Kamati utakuwa ni minimum. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri tu speed up hii process ya kupeleka maafisa kwani umuhimu wake uko wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama vile haitoshi, kwa nini mimi nasema nasema masuala haya, watu wengi tunapozungumza masuala ya peace keeping wanazungumzia chapter six na chapter seven; lakini ukweli UN imeendelea kupunguza fedha za kulinda amani katika maeneo ya migogoro Afrika. Hii ni kwa sababu ama tunapunguziwa ushawishi kutoka labda na understaffing.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimwmbe Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ni nguli katika nyanja hii, katika hii reform inayoendelea ya UN Security Council hebu sisi kama watu ambao tunaaminika kiplomasia na kimataifa, kwamba tuna ushawishi mkubwa Kusini mwa Afrika, tuna ushawishi mkubwa katika bara la Afrika, tuna ushawishi mpaka katika South East Asia, hebu tu-play role yetu ili kusudi ushawishi kama Taifa katika Umoja wa Mataifa uendelee kuwa mkubwa ili kusudi hata yanapokuja masuala ya bajeti kwa mfano za peace keeping tuweze kushawishi pesa itengwe ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu madhara yake ni nini, tumeona tumepoteza wanajeshi pale Congo. Ingekuwa UN inapeleka bajeti ya kutosha ya peace keeping; maana tumeambiwa mapigano yalidumu masaa 14, maana kama vingekuwa vifaa vya kisasa, tuna ndege za rescure maana yake tungeweza kuokoa wanajeshi wetu wale. Haya yote hayafanyiki kwa sababu ndani ya mfumo wa UN wakubwa wa dunia wanajitahidi kuhakikisha ile keki inapelekwa katika mambo ambayo wao wanaona yatakuwa yanawasaidia lakini sisi hayatusaidii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niishauri Serikali kwamba tuendelee kuthibitisha kwa vitendo kwamba sisi ni taifa kubwa katika ushawishi wa diplomasia kimataifa Afrika na duniani kwa ujumla; na ushiriki huu utathibishwa kwa sisi kuendelea kuwa na staff wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia sitakuwa nimetenda haki kama sitawashukuru Wizara katika ujumla wake. Nimeona hapa wametuletea kijitabu kinasema find about us; ndani yake kina anuani za Balozi zetu. Maana yake ni kwamba sisi hapa ama tuna ndugu zetu ama tuna watu wanaenda katika matibabu au watu wanaenda kutafuta fursa za kibiashara au kuna wanafunzi. Sasa kijitabu hiki kitarahisisha yale mawasiliano ya kidiplomasia kujua nchi gani balozi ni nani na anuani yake ni ipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi wametupa pia kijitabu ambacho kinaonesha anuani za Balozi za nje ambazo ziko hapa nchini. Vile vile wametupa kijitabu hiki kinachoonesha diplomasia ya Tanzania ambapo ndani yake wametuonesha picha, wameandika na caption ya utekelezaji mbalimbali wa Diplomasia Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niwashukuru sana na naamini Mheshimiwa Masoud, Mzee wangu wa Matambile pale atakuwa leo amefurahi na atacheka mpaka jino la mwisho kwa sababu ni kitu ambacho tumekuwa pia tukizungumza katika Kamati na Serikali imeweza kuthibitisha. Niongeze tu wakati ujao wanaweza kutuboreshea pia kwa kutuletea kijitabu ambacho kinaeleza kila nchi ina fursa gani na watu wanaweza kuzipata fursa zile kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, napende kushukuru na naunga mkono hoja. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. Ahsante sana.