Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi si Tanzania ya Nyerere, ni Tanzania mpya, Tanzania mbaya inayokalia kimya mauaji ya kinyama ya Wapalestina na kuunga mkono waonevu.

(i) Msimamo wa Tanzania kuhusu Palestine (aya 18 ya Hotuba ya Waziri), maelezo ya Serikali hayaendani na matendo. Tanzania imewatupa mkono wanyonge wa Palestine.

(ii) Msimamo wa Tanzania kuhusu Sahara Magharibi (aya 19 ya Hotuba ya Waziri), kuna dalili zote kuwa Serikali inataka kuwafukuza POLISARIO baada ya kuikumbatia Morocco.

(iii) Unafanyaje diplomasia bila wanadiplomasia? Vituo vingi nje havina FSOs.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo wa Tanzania kuhusu mgogoro wa Israel na Palestina unaelezwa vizuri sana na nukuu hii ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1967 na ndiyo umekuwa msingi wa Sera yetu ya Mambo ya Nje kwa miaka mingi kabla ya utawala wa sasa wa CCM mpya.

“….Tanzania’s position. We recognize Israel and wish to be friendly with her as well as with the Arab Nations. But we cannot condone aggression on any pretext, nor accept victory in war as a justification for the exploitation of other lands, or Government over other peoples.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba Tanzania inaitambua Israel na inapenda kuwa na urafiki nayo pamoja na urafiki na mataifa mengine ya kiarabu, lakini hatuwezi kukalia kimya uvamizi kwa namna yoyote ile, pia ushindi vitani hauhalalishi unyonyaji dhidi ya ardhi ya wengine au dhidi ya Serikali za watu wengine. Msingi huu unaendana kabisa na dhamira ya sasa ya Sera ya Mambo ya Nje. Hata hivyo, hali ni tofauti kabisa. Mambo tunayoyayafanya kwenye Sera yetu ya Mambo ya Nje yanamfanya Mwalimu Nyerere ageuke huko kaburini kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaeleza kwa mifano, 26 Oktoba, 2016 kulikuwa na kikao cha Wajumbe wa Nchi 21 zinazounda ‘Kamati ya Urithi wa Dunia’ ya UNESCO-Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni kupiga kura ya kupitisha makubaliano ya kuridhia kuupa hadhi ya urithi wa Dunia Mji wa Jerusalemu pamoja na moja ya majengo ya Mji huo (Temple Mount) na kufungamanishwa na uasili wake na si hali ya sasa inayotokana na uvamizi wa Israel juu ya eneo hilo lililoko Jerusalemu Mashariki (lililovamiwa mwaka 1967 na mpaka leo kutambuliwa na UN kama eneo la Palestina, ambao wanauona ndiyo Mji Mkuu wa nchi ya Palestina iwapo makubaliano ya ‘Two States Solution’ yatafikiwa).

Mheshimiwa Naibu Spika, ACT Wazalendo tulihoji juu ya jambo hili linalokwenda kinyume na Sera ya Nje ya nchi yetu. Msimamo wa Tanzania ni kukubaliana na UN kupinga uvamizi wa eneo hilo uliofanywa na Israel. Serikali ilitoa majibu mepesi tu, tena pembeni kuwa upigaji wa kura ule haukuwa msimamo rasmi wa nchi yetu ni ukiukwaji wa sera yetu ya Mambo ya Nje na kuwa ni jambo ambalo Afisa wetu kwenye mkutano ule wa UNESCO alilifanya kwa makosa na hivyo hatua zingechukuliwa dhidi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri hayo yalikuwa ni ghiliba tu, matukio ya karibuni yameonesha kwa uwazi sura mpya ya Taifa letu pamoja na msimamo mpya wa Sera yetu ya Mambo ya Nje. Kwenye diplomasia matendo ya nchi huwa na maana zaidi kuliko maneno ya wanadiplomasia wake, matendo yetu yafuatayo ya karibuni yameonesha kuwa Tanzania hatuiungi mkono tena Palestina.

(1) Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwaangusha Wapalestina kule Paris kwenye Mkutano wa UNESCO, Serikali iliahidi kuwa ingemchukulia hatua Afisa yule wa Wizara ya Mambo ya Nje aliyekwenda kinyume na Sera yetu ya Mambo ya Nje, hatujafanya hilo zaidi tumempandisha cheo na kumteua kuwa Balozi Elizabeth Kiondo apige kura namna ile kule UNESCO na sasa tumempa cheo zaidi kwa kazi njema aliyoifanya. Jambo hili linaonesha kuwa kwa sasa tunawaunga mkono Waisrael na hatuko tena na Wapalestina.

(2) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tumeamua kufungua Ubalozi wetu Israel, Tel Aviv, kuongeza uchungu kwenye kidonda, tukachagua wakati huu wa maadhimisho ya miaka 70 ya uvamizi wa Israel ardhi ya Taifa la Palestina kuzindua ubalozi wetu huo. Jambo hili linafanyika kukiwa na tuhuma kuwa hata huo ubalozi unagharamiwa na Israel yenyewe, ndiyo maana tumepangiwa hata kipindi cha kuufungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kidiplomasia kuufungua ubalozi wetu katika wakati huu ni kuadhimisha uvamizi wa Israel katika ardhi ya Palestina. Maana tulikuwa na uwezo wa kuchagua wakati mwingine wowote kufanya uzinduzi wa ubalozi wetu, lakini kwa kuwa aliyegharamia uwepo wa Ubalozi huo (Israel) alitaka tuufungue wakati huu wa maadhimisho ya miaka 70 ya uvamizi wa Israel kwa Palestina, ilitubidi tufanye hivyo. Jambo hili limeonesha kuwa kwa sasa hatuungi mkono tena utu (Palestina) bali tunamtumikia kila mwenye kitu (Israel).

(3) Mheshimiwa Naibu Spika, wakati akiwa ziarani Israel, Balozi Dkt. Mahinga alifika sehemu ya miji inayokaliwa kimabavu na Israel ambayo inapakana na ukanda wa Gaza, na baadaye alihojiwa na Televisheni ya Taifa ya Israel ambako alionesha tu masikitiko yake kwa Waisrael wanaokaa maeneo hayo kwa kusumbuliwa na mashambulizi ya Hamas, lakini hakulaani kabisa uendelezaji wa Israel kujenga makazi kwenye maeneo hayo ya uvamizi kama wanadiplomasia wengine wa nchi zenye msimamo wa ‘Two States Solution’ kama sisi wanavyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Balozi Dkt. Mahinga mwanadiplomasia mzoefu na mbobezi, kutokulaani kwake makazi yale haramu ni jambo la makusudi kabisa, si bahati mbaya. Ni kitendo cha kutuma salamu kwa Wapalestina kuwa tunaunga mkono uendelezaji makazi wa Israel katika maeneo hayo iliyoyavamia.

(4) Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imetajwa na vituo mbalimbali vya habari vya Kimataifa kuwa ni katika nchi 33 ambazo zilihudhuria ufunguzi wa Ubalozi wa Marekani Mjini Jerusalemu, Mei 14 kilele cha maadhimisho ya miaka 70 tangu uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina. Chanzo cha taarifa ya Tanzania kuhudhuria ni Serikali ya Israel, ikitaja nchi ilizozialika na zilizohudhuria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu inasema inapinga uwepo wa Ubalozi wa Marekani Mjini Jerusalem, lakini hapo hapo inatajwa kuhudhuria uzinduzi huo. Picha tunayoitoa hapa kwa Wapalestina ni kuwa tunaunga mkono jambo hili la ufunguzi wa Ubalozi wa Marekani Mjini Jerusalem.

(5) Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya uzinduzi huo wa ubalozi wa nchi ya Marekani Mjini Jerusalemu, Jeshi la Israel liliwaua kwa risasi zaidi ya watu 54 wa Palestina, wakiwemo wanawake, watoto, walemavu na hata wanahabari. Nchi mbalimbali duniani zimelaani mauaji hayo. Nchi ya Afrika ya Kusini imekwenda mbali zaidi kwa kumrudisha nyumbani Balozi wake aliyeko Israel. Tanzania tuliyoikomboa Afrika ya Kusini tumekaa kimya, tumeshindwa hata kutoa kauli ya kulaani mauaji hayo. Kuhudhuria kwetu ufunguzi wa ubalozi na kukaa kimya juu ya mauaji hayo kunaonesha tumewaacha rasmi Wapalestina.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo hayo matano yanaonesha kuwa sisi si tena ile Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere, sisi kwa sasa ni Tanzania mpya (kama yasemavyo matangazo ya Ikulu yetu) – Tanzania mpya inayosimama na waonevu wa dunia, wauaji na wavunja haki za wanyonge. Sisi si tena Tanzania ya kusimama na wanyonge, bali ni Tanzania ya kusimama na wanyongaji kwa sababu ya maslahi ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, si ile Tanzania iliyongoza ukombozi wa Bara la Afrika kutoka kwenye makucha ya ukoloni, bali ni Tanzania mpya inayounga mkono na kushabikia ukoloni na uvamizi. Sisi si ile Tanzania yenye msimamo mkali tuliopinga Taifa kubwa la Marekani dhidi ya
uvamizi wake kwa wanyonge wa Taifa la Vietnam, bali sasa ni Tanzania mpya ya kuunga mkono uvamizi wa Taifa onevu la Israel kule Palestina.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi si Tanzania ile iliyoitetea China ipate nafasi na Kiti chake stahili kule UN, bali sasa sisi ni Tanzania mpya inayowaacha watu wa Palestina bila utetezi wa hadhi, kiti na nafasi yake stahili kule UNESCO.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi si ile Tanzania huru tena ya Mwalimu Nyerere, iliyowaheshimu watu na Mataifa kwa sababu ya utu wao na kuamini kwamba binadamu wote ni sawa. Sasa sisi ni Tanzania mpya, inayowapa heshima watu kwa sababu ya kitu inachotuhonga, tukiuza usuli wa Utaifa wetu kwa maslahi machache ya kifedha au kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwashi tena Mwenge na kuuweka Mlimani Kilimanjaro, hatumuliki tena nje ya mipaka yetu, hatuleti tena matumaini pale pasipo na matumaini, hatupeleki tena upendo kule kuliko na chuki na hatuleti heshima pale palipojaa dharau. Sisi si Tanzania ya Mwalimu Nyerere, sisi sasa ni Tanzania mpya, Tanzania mbaya, Taifa lililokiuka misingi yake, Taifa linalowaacha Wapalestina wakiuawa kinyama na sasa linalosapoti waonevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kujengewa uwanja wa mpira na msikiti visiifanye Tanzania likumbatie Morocco na kuacha kuiunga mkono Sahara Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado niko kwenye Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi yetu, si hii ya Tanzania mpya bali ile Tanzania ya tangu wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya kusimama na wanyonge. Wakati tulipoamua kufuata ‘Diplomasia ya Uchumi’ bado msingi wetu huu wa kusimama na wanyonge ulibaki palepale. Ndiyo maana wakati wa Rais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete bado tulibaki kuwa ni sauti ya Mataifa yanayoonewa kama Cuba (tukipinga vikwazo vya Marekani dhidi yao), Palestina na Sahara Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi huo wa kusimama na wanyonge ni muhimu zaidi kwa Chama chetu cha ACT Wazalendo, ndiyo maana tulipinga ujio wa Mfalme wa Morocco hapa nchini tarehe 23 - 25 Oktoba, 2016. Kwa kuwa Taifa hilo bado linaikalia kimabavu ardhi ya wanyonge wa Sahara Magharibi, ndiyo msingi pia wa kutangaza wazi mahusiano yetu rasmi na Chama cha Siasa na Ukombozi wa Taifa hilo cha POLISARIO kinachopigania uhuru wa nchi ya Sahara Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Umoja wa Afrika (AU) uliamua kukubali ombi la Morocco kurudi bila masharti kwenye Jumuiya hiyo. Ikumbukwe kuwa kwa zaidi ya miaka 33 Morocco haikuwa na mahusiano na Jumuiya hiyo (tangu OAU mpaka sasa AU) baada ya kujitoa kwa kupinga OAU kuitambua Sahara Magharibi kama Taifa huru na kupewa Kiti rasmi ndani ya OA mwaka 1984.

Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi wa OAU wa kuiruhusu Sahara Magharibi kuwa mwanachama wa umoja huo ulitokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court of Justice-ICJ) ya mwaka 1975 iliyopinga madai ya Morocco kuwa ina mahusiano ya kihistoria na kisheria na Sahara Magharibi (na hivyo kuitawala kinguvu) na kutoa haki ya kujitawala kwa Taifa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaheshimu maamuzi yale ya mkutano wa AU uliofanyika Januari, 2017 ulioirudisha Morocco kwenye AU, lakini tabia za Taifa hilo onevu bado hazijabadilika, hivyo ni muhimu tulieleze Bunge hili Tukufu masuala yafuatayo ili liweke msimamo wake kwa Serikali juu ya kuminywa kwa watu wa Sahara Magharibi:-

(1) Kikao cha AU cha tarehe 28 - 29Januari, 2018 kiliazimia kuwa Morocco iruhusu Kamati Maalum ya Uangalizi ya AU iende kwenye maeneo ya Sahara Magharibi ambayo inayakalia kimabavu ili kuja kuijulisha AU hali ya mambo ilivyo.

(2) Tarehe 29 Machi, 2018 Morocco iliwajulisha UN juu ya kutoruhusu waangalizi wowote wa AU kwenda kwenye maeneo yote ya Sahara Magharibi inayokalia.

(3) Tangu mwaka 1991 Morocco imetumia mbinu, hila na uzandiki ili kuzuia Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kura ya maoni ya uhuru wa Sahara Magharibi (MINURSO) kufanya kazi yake kwenye maeneo inayoyakalia kimabavu ya Sahara Magharibi. Siku za karibuni Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha Azimio Na. 2414 (2018) la kuongeza muda wa mamlaka, uhai na madaraka ya MINURSO kwa miezi sita, Morocco imepinga jambo hilo na kutishia kufanya mashambulizi ya kijeshi kwenye maeneo ya Sahara Magharibi ambayo yameshakombolewa (Liberated Zones).

(4) Bado Morocco inaendeleza uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu kwa watu wote wa Sahara Magharibi wanaodai uhuru wao.

(5) Kurudishwa kwa Morocco kwenye AU kulienda pamoja na Taifa hilo kuridhia ‘AU Constitutive Act’ inayotaka Mataifa ya Afrika kuheshimu Maazimio ya AU na hata yale ya UN yanatolewa kwa ushirikiano na AU. Hata hivyo, kwa matendo yake tuliyoyaainisha hapo juu ni dhahiri kuwa Morocco haitaki usuluhishi na Sahara Magharibi, bado inataka kuitawala na kuikalia kimabavu, ndiyo maana imekataa hata kumpa ushirikiano msuluhishi wa mgogoro huu, Ndugu Horst Kohler Rais wa zamani wa Ujerumani.

(6) Matendo ya Serikali yetu kwa sasa yanaonesha hatuna msimamo kwenye mambo ya msingi ya kidiplomasia, namna tulivyoenenda kwenye mahusiano yetu na wanyonge wa Palestina ni mfano hai, sasa tukijali vitu kuliko utu kama ilivyo zamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, nataka kulishawishi Bunge lako litoe mwongozo kwa Serikali juu ya kuenenda kwenye hili jambo la Morocco na Sahara Magharibi ili kuzuia ahadi ya kujengewa uwanja na msikiti na Serikali ya Morocco. Vitu visitufanye tuwaache ndugu zetu wanyonge wa Sahara Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ni kimbilio la nchi ya Sahara, Serikali yetu chini ya Mwalimu Nyerere ililitambua Taifa la Sahara Magharibi tangu siku za mwanzo kabisa za harakati zao, ndiyo maana wanao Ubalozi hapa nchini. Kumuenzi Baba wa Taifa na kulinda misingi ya Taifa letu ni lazima tusimame na watu wa Sahara Magharibi na tusiwatupe kama tulivyofanya kwa watu wa Palestina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naliomba Bunge liibane Serikali ili itoe ahadi hiyo hapa Bungeni, pamoja na kuitaka Serikali kutumia ushawishi wake kule AU na UN kuibana Morocco iruhusu kura ya maoni ya kuamua mustakabali wa watu wa Sahara Magharibi kama ilivyoridhiwa kwenye Azimio la UN. Viva Sahara Magharibi, Viva POLISARIO, Mungu Ibariki Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Diplomasia bila wanadiplomasia, tuna uhaba mkubwa wa Watumishi kwenye Balozi zetu. Msingi wa tano wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania unatutaka tushirikiane kikamilifu na nchi, Mashirika pamoja na Taasisi mbalimbali katika nyanja za Diplomasia, siasa, uchumi, utaalam na teknolojia. Wizara hii ina jukumu la kubuni na kusimamia utekelezaji wa misingi yote ya sera yetu ya mambo ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wizara hii pia ina jukumu la kusimamia na kuratibu mahusiano kati ya Tanzania na nchi pamoja na mashirika mbalimbali. Utimizaji wa jambo hilo unafanyika kupitia Balozi zetu zilizotapakaa kwenye nchi mbalimbali ulimwenguni. Kwa sasa ufanisi wetu si mkubwa kwa sababu ya uhaba wa Watumishi kwenye Balozi zetu mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wastani ukimwondoa Balozi, kila kituo cha Ubalozi wetu nje ya nchi kinapaswa kuwa na Mhasibu, mtu wa TISS pamoja na mwanadiplomasia (FSO). Vituo vingi vya Balozi zetu havina kabisa Maafisa wa Diplomasia (FSO’s), wale wachache waliokuwepo awali walirudishwa nchini kwa sababu mbalimbali (ikiwemo kumaliza muda wao wa Utumishi Nje ya Nchi). Tumerudisha watu bila kupeleka mbadala wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Balozi zetu mbalimbali Watendaji hasa wa kazi za Kibalozi na Kidiplomasia ni hawa Maafisa wa Diplomasia (FSO’s). Sasa kwa uhaba huu tunawezaje kufanya diplomasia ya nchi yetu? Hiyo Diplomasia ya Uchumi tunafanyaje bila kuwa na hao wanadiplomasia?

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa tu mfano wa Balozi zetu chache ulimwenguni, China nchi ambayo ni mshirika wetu mkubwa kidiplomasia na kiuchumi, hatuna kabisa FSO huko, labda ndiyo sababu mauzo yetu kwenda China yameshuka mno, maana biashara ya nje ni diplomasia. Sasa wakati unamtaka ndugu yangu Charles Mwijage asafiri ni nani atakayemuandalia hiyo mikutano ya kupata wawekezaji huko China kama hatuna FSO hata mmoja? Wenzetu Uganda wana FSO’s nane huko China, Kenya na Sudani wao wanao tisa kila mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingine ambayo hatuna FSO ni Ethiopia-Makao Makuu ya AU, utaona tunavyodharau nafasi yetu katika Afrika. Pia hatuna FSO Afrika Kusini, nchi rafiki na moja ya zenye uchumi mkubwa Afrika, hatuna kabisa FSO Ujerumani, nchi kubwa zaidi kiuchumi katika Umoja wa Ulaya (EU). Hata India ambako tangu Bunge lianze Wabunge tunalalamikia kukosa soko la mbaazi kutoka huko nako hatuna FSO hata mmoja. Tumeufanya kuwa ubalozi wa kupokea wagonjwa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za BRICS (ukiondoa China, India na Afrika Kusini ambazo hatuna kabisa FSO’s) zilizobaki, Brazili na Urusi tuna FSO mmoja mmoja tu. Hata DRC Congo nchi ambayo zaidi ya theluthi moja ya mizigo ya transit inapita kwenye bandari ya Dar es Salaam inatoka, nayo tuna FSO mmoja tu tofauti na watatu ilivyozoeleka.

Kenya nchi ya Afrika Mashariki tunayofanya nayo biashara zaidi nayo ina FSO mmoja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali iko hivyo karibu katika Balozi zetu nyingi ulimwenguni, FSO’s ndiyo Maafisa hasa waliyofundwa na kupikwa kutekeleza sera yetu ya Mambo ya Nje. Foreign Service Officers (FSO’s) ndiyo diplomats (wanadiploma wetu). Kama hawapo vituoni na hatuwatumii maana yake hatufanyi diplomasia na kwa kuangalia mbali tunaua diplomasia yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitapitisha bajeti hii mpaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itakaponihakikishia kuwa itapeleka Maafisa wa Diplomasia (FSO’s) katika vituo ambavyo hatuna kabisa na pia kuwaongeza katika vile vituo ambavyo wako wachache.