Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukupongeza kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Naitwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa namna kilivyoiandaa Ilani yake. Ilani yake ni Ilani nzuri ambayo imetengeneza mpango mzuri wa mwelekeo wa Taifa ambako linatakiwa kwenda. Katika chaguzi zetu tuliinadi Ilani na wananchi wakatuchagua. Kwa hiyo, napenda kukipongeza chama. Hawa wanaotoka sasa ni kwa sababu hoja zao nyingi zinapwaya, hawana kitu cha kukizungumzia zaidi ya kutengeneza vijembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kujikita katika hotuba ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake katika ukurasa wa 12 ameizungumzia reli toka Mtwara – Songea – Mbamba Bay mpaka Liganga. Mimi napenda kumshukuru kwa hilo na tulipokuwa tunaizungumzia hiyo reli ya kutoka Mtwara mpaka Liganga ni kwa maana tunazungumzia suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga limekuwa ni suala la muda mrefu. Nadhani sasa ni kipindi cha miaka 50 limekuwa likizungumziwa na halina utekelezaji wowote. Nimshukuru Waziri Profesa Muhongo, tarehe 4 na 5 alifika kwenye makaa ya mawe Mchuchuma na vilevile alifika pale chuma – Liganga; alijionea type ya wawekezaji ambao tunao na namna gani wanaweza wakaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisikitike, wana wa Ludewa wana masikitiko makubwa. Wameachia ardhi yao miaka ipatayo 10, ardhi ile haitumiki, hawaitumii kwa maana yao na hakuna utaratibu wowote wa matumaini wa kulipwa fidia katika maeneo ambayo wao wameyaachia.
Sasa nipende kuliambia Bunge lako, wananchi wanataka fidia ya maeneo waliyoyaacha na kibaya zaidi hata ule mpango wa kimkakati wa huyu mwekezaji bado hauonekani!
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Waziri Muhongo tarehe 5 Mchuchuma, pale Nkoma Ng‟ombe na vilevile tulikuwa Liganga pale Mndindi; Serikali imekuwa ikiwakilishwa na NDC na wawekezaji ni Wachina, lakini katika majadiliano na maongezi yao wana contradiction kubwa. Ile miradi ni mikubwa, kuna mamilioni ya tani za makaa ya mawe, leo nchi inazungumza kwamba haina umeme! Lakini tunaamini mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma ukianza umeme katika Taifa hili inaweza ikawa ni historia.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme utakaozalishwa Liganga una uwezo wa ku-supply ndani ya nchi hii katika miaka isiyopungua 150, lakini leo Taifa bado halijachukua hatua madhubuti. Ni miaka mingi, sisi wengine toka tunasoma, kabla hatujazaliwa tunaambiwa kuna makaa ya mawe – Mchuchuma, tunaambiwa kuna chuma – Liganga! Mwekezaji aliyepo ameonesha incompetence kubwa mbele ya Waziri Profesa Muhongo! Hakuna maandalizi ya kutosha ya hiyo miradi kuanza!
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nipende tu kushukuru na kumshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, aliwaeleza wananchi wetu ukweli kwamba Taifa tunapoamua kuingia mikataba hii iwe ni ya wazi na kusiwepo na uficho wowote.
Mimi ninaamini Waziri usingekuja Ludewa, usingekuja pale Nkoma Ng‟ombe – Mchuchuma, usingekuja Liganga bado wananchi wetu wangekuwa wanaendelea tu kudanganywa danganywa na tusingejua fate yoyote ambayo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nipende kuchukua fursa hii kwamba, tupate wawekezaji ambao ni serious. Tupate wawekezaji ambao wana uhakika, ili mwisho wa siku watu wetu tuwajengee matumaini, ili nchi iweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukizungumza sana Bungeni kwa nini nchi haiendi, wakati tuna madini ya kutosha, tuna mazao ya kutosha, lakini hatuchukui hatua. Huyu mwekezaji amekuwa akikumbatiwa! Haoneshi dalili yoyote ya namna gani tunaweza kwenda! Fidia hataki kulipa, anaulizwa kama hizo hela anazo anasema hela hana anasubiri kukopa nje ya nchi! What type of mwekezaji is? Sasa investor wa namna hii kweli tunakaa na kumkumbatia namna hii? Mimi nadhani siyo sawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Ludewa wanaisubiria Liganga ianze mara moja kwa sababu, imeshakuwa ni hadithi za muda mrefu. Liganga aanze, Mchuchuma aanze, tuachane na hii biashara kwamba hatuna umeme, hatuna umeme, hatuna umeme! Hii inatakiwa kubaki kuwa ni historia. Lakini mimi ninamuamini Waziri Muhongo atalishughulikia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ya Itoni – Njombe kuelekea Manda; barabara hii Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba iwekwe lami, lakini nashukuru TANROADS juzi imetangaza kipande cha kilometa 50 kutoka Lusitu kuelekea Mawengi kwamba kitawekwa lami. Kwa hiyo, tunaomba hili lizingatiwe na lifanyiwe kazi haraka vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna barabara kutoka Mkiu kwenda Madaba na yenyewe Mheshimiwa Rais ameizungumzia kwa kiwango cha lami. Tunaomba lami hiyo iwekwe na wananchi wana matumaini, wana mazao yao mashambani, ila usafiri umekuwa ni shida, pindi hizi lami zikiwa tayari naamini kabisa mazao yatafika kwenye maeneo ya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna suala la miundombinu ya mawasiliano ya simu. Leo hii Tarafa nzima ya Mwambao, Ukisi kule Ziwa Nyasa tunapakana na Malawi, vijiji 15 havina mawasiliano ya simu kabisa! Sasa sijajua Serikali inajipangaje na inawaonaje hawa watu? Hawa watu wako mpakani! Huku tunapakana na Kyela na Dkt. Mwakyembe! Huku tunapakana na Nyasa na Engineer Manyanya! Hapa katikati pamekuwa hamna mawasiliano ya aina yoyote! Wananchi wale wameniambia wataanza wao kutafuta hayo mawasiliano. Hatuna mawasiliano ya barabara, hatuna mawasiliano ya simu! Kwenye upande wa barabara wanasema wao wataanza na jembe la mkono. Na ninaiomba Serikali sasa ituunge mkono, ili tuweze kuviunganisha hivi vijiji na waonekane na wao wapo ni sehemu ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiahidiwa muda mrefu juu ya daraja la Mto Ruhuhu unaounganisha Wilaya ya Ludewa na Wilaya ya Nyasa. Wananchi wanapata shida na kivuko kile na kivuko kimekuwa hakifanyi kazi. Dada yangu Injinia Manyanya unalifahamu hilo. Tunaomba Serikali ilichukue hilo na ilifanyie kazi, ili mwisho wa siku tuweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi sisi wana wa Ludewa. Mheshimiwa Rais alipokuja Ludewa alitoa ahadi ya kipande kidogo cha lami cha kilometa 25 kutoka Ludewa mpaka Lupingu. Kwa hiyo, tungeomba ahadi hizo zitekelezwe.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umeisha!
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)