Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninashukuru kwa kuweza kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii jioni ya leo. Kabla sijaendelea niseme kwamba naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili namshukuru Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wengine wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya na sote tunaiona kazi hiyo. Jambo moja ambalo Waziri inabidi alifahamu ni kwamba kuna hadithi ya uyoga wa porini, ukienda porini ukikuta uyoga haujaguswa hata na ndege ujue huo uyoga ni sumu, kama uyoga umeparuliwa paruliwa ujue basi huo uyoga unaliwa. Sasa mishale anayopata maana yake kwamba anafanya kazi kubwa na watu wanaona kazi hiyo. Wengine tumeshakwenda naye mguu kwa mguu mpaka Majimboni kwetu kwa hiyo tunatambua ufanyaji kazi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo naiona kwenye Wizara hii, yawezekana wewe speed ya Waziri ni kubwa kuliko hao anaofanya nao kazi. Kwa sababu Waziri akitoa maagizo TANESCO wenyewe wanapumzika wanasubiri tena Waziri aende, sasa tunataka mfumo ufanye kazi. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana Wizara isimamie mfumo kufanya kazi. Ndiyo maana watu wanasema TANESCO inabidi iangaliwe upya, pia TANESCO inatakiwe liwe Shirika vibrant na liwe customer focused. TANESCO ikifanya kazi kwa mfumo huo tutapiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo katika Jimbo la Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla ni kwamba REA II na REA III ilikuwa haijaanza. Kwenye ukurasa wa 55 tumeambiwa kwamba mkandarasi anaanza, sasa tunaomba mkandarasi afike na afanye kazi kwa ukamilifu. Jambo hili ni muhimu sana kwa sababu kuna maeneo umeme umewaka na maeneo mengine umeme haujawaka na wananchi wanasubiri umeme. Kauli mbiu yetu kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tunasema umeme utawaka vijiji vyote, hata mimi nikienda nawaambia umeme utawaka vijiji vyote. Sasa kama ndiyo kauli mbiu yetu basi umeme unatakiwa uwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba nguzo zinapelekwa kidogo sana. Pale Ibaga umeme umewaka lakini maeneo mengi hayajapata umeme, kwa hiyo pale manung’uniko mengine yamezaliwa ingawaje kazi kubwa ya kuwasha umeme imefanyika. Ukienda Iyambi, Gumanga, Nkalakala, Kinyangiri, Iguguno umeme umewaka lakini vitongoji vyake au maeneo ya karibu kabisa hayana umeme. Scope hiyo inabidi iangaliwe ili watu wengi waweze kupata umeme lakini pia umeme ni biashara TANESCO waweze kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba Serikali inatoa pesa nyingi kujenga vituo vya afya. Wizara ya Afya na TAMISEMI wametoa shilingi milioni 400 kujenga vituo vya afya lakini havina umeme. Nafikiri sasa ni wakati muafaka Waziri atakapo-wind up atoe tu agizo kwamba vituo vyote vya afya vilivyojengwa umeme upelekwe, kwa sababu upasuaji na vipimo vitafanyikaje? Jambo hilo naona limesahaulika halafu tunaanza kupeleka maombi TANESCO inakuwa ni changamoto. Kama majengo yanakabidhiwa kwamba yamekamilika basi na umeme unatakiwa uwe umefika. Jambo hili pia tutazungumza na Waziri wa Maji ili na maji pia yaweze kufika kwenye vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuja na energy mix, kwa kuleta vyanzo vya umeme kwenye Grid ya Taifa kwa mifumo mbalimbali.
Umeme ulipokuwa unakatika tulikuwa tunalalamika kila siku sasa umekatika na siku hizi tuna mitandao wanasema sasa umeme umekatika, lakini katika kutekeleza azma hiyo huu mradi wa Stiggler’s Gorge nafikiri umeleta matatizo kidogo kwa baadhi ya watu. Umeleta matatizo kwa sababu tu ya kuwa na fikra mgando kwa sababu ni lazima utumie rasilimali uliyonayo ili uweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya rasilimali tuliyonayo ni hilo bonde na umeme wake unahitajika na kama study zimeshafanyika tangu mwaka 1950 na 1960 hakuna jambo jipya ambalo tunafanya sasa hivi. Kwa hiyo, jambo jema ni kushauri mradi huo utekelezwe vipi na hapa tunawashauri wataalam wetu wa mazingira waweze kusimamia kikamilifu jambo hili na mradi utekelezwe lakini tuupokee mradi badala ya kuanza kuuzuia kwamba usiweze kutekelezeka. After all Serikali imeshaamua kutekeleza nani anatakayezuia tena, kwa hiyo, mradi unaenda kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga. Bomba hilo litapita katika Mkoa wa Singida na katika Wilaya ya Mkalama ambako mimi ndiye Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki. Tunaiomba Serikali iangalie na isimamie kwa ukamilifu suala la fidia, pia suala la watu watakaofanya kazi katika bomba hilo katika Wilaya hizo au Mikoa husika waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivi kwa sababu mara nyingi maandiko huwa yanakuwa mazuri sana, tunapokutana kwenye presentation, tunapotaka kuanza mradi mambo yanayozungumzwa yanakuwa roses, yote yanakuwa ni maua mazuri lakini mradi unapoanza ndipo changamoto zinakuja. Kwa hiyo, tujifunze kutokana na makosa, hatutarajii kwamba mradi huu utaleta malumbano na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kutakuwa na quarters za wafanyakazi, kwa maana kwamba Wilaya hii au Mkoa huu utaleta wafanyakazi kadhaa na wafanyakazi hao waandaliwe, ikiwepo hata Mama Ntilie maana yake watapeleka vyakula katika maeneo hayo. Kwa hiyo, jambo hilo tukiliratibu vizuri nafikiri tutapiga hatua kubwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni hili bomba la gesi wanasema linatumika kwa asilimia sita tu. Naona watu wengi tunasimama tunalaumu tu, lakini hayo ndiyo maendeleo na bomba lingekuwa limetumika asilimia 100 ingekuwa lime-fail. Sasa hivi tumeona gesi ya majumbani imeanza kutumika na viwanda vinatumia gesi. Kwa hiyo, tunatumai kwamba hili bomba sasa litatumika kikamilifu kulingana na capacity level. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi zaidi ni kwamba Mawaziri tunawahimiza kutembelea maeneo ya vijijini. Mkitembelea maeneo ya vijijini...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.