Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza kabisa, nianze kwa kusema yapo mambo katika Taifa letu ambayo kiukweli yanatia kichefuchefu sana. Kama Taifa na Bunge endapo mambo haya hayatachukuliwa hatua yoyote sisi Wabunge humu ndani tunakosa sababu ya kuendelea kuwa humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie picha halisi ya ufisadi mkubwa unaofanyika kwenye mradi wa Songas. Kwenye mradi wa Songas kuna ufisadi mkubwa sana. Ukiangalia investment ya mradi wa Songas kwenye upande wa capital structure, Songas wali-invest karibu Euro milioni 392. Katika Euro 392, Serikali ilitoa Euro milioni 285 ambayo ni sawasawa na asilimia 73 na Songas wenyewe walitoa karibia asilimia 27 peke yake, shikilia hapo kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shareholding structure umiliki kwenye mradi wa Songas, Serikali inamiliki only 46 percent na Songas inamiliki 54 percent ya mradi mzima. Swali kwa Serikali ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri anapokuja kesho ku-wind up hapa aseme. Kama Serikali kwenye capital structure ime-invest kwa asilimia 73 kwa nini kwenye shareholding structure inamiliki asilimia 46 peke yake? Serikali kwenye shareholding structure inakuwa minority wakati kwenye investment imekuwa majority kwa ku-invest 73 percent. Swali la kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kila mwezi TANESCO inalipa Dola milioni tano kwenye mradi wa Songas kama capacity charges. Capacity charges ni kitu gani? Capacity charges ni fidia anayopewa mwekezaji kufidia gharama alizowekeza na lengo kubwa ni kutaka baada ya mkataba kuisha ile mali inakuwa chini ya Serikali. Sasa Serikali kupitia TANESCO inalipa Songas Dola milioni tano kila mwezi kila mwezi, katika Dola milioni tano kila mwezi wanaacha kutoa Dola milioni 3.6 kwa ajili ya Serikali kama Serikali ambayo imetoa 73 percent kwenye uwekezekaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipiga mahesabu ya toka mradi huu ulipoanzishwa mwaka 2004 mpaka sasa ni 14 years, Dola milioni 3.6 kwa miaka 14 tumepoteza zaidi ya trilioni 1.3. Mkataba huu wa Songas ni wa miaka 20, tafsiri yake ni kwamba huu mkataba unakwenda mpaka mwaka 2024, kama mtapuuza tunakwenda kupoteza zaidi ya trilioni mbili kwenye mradi mmoja peke yake wa Songas. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo Serikali kuna wakati lazima msikilize na mtii. Mamlaka kubwa kama Bunge inaposhauri ni lazima msikilize, mamlaka kubwa kama CAG inaposhauri lazima msikilize. Suala hili la ufisadi kwenye Songas limezungumzwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge mwaka 2005, ninayo hapa na mwaka 2006 chini ya Mwenyekiti wake, kipindi hicho alikuwa Mheshimiwa William Shelukindo, katika ukurasa wa 8, anaeleza namna ambavyo mkataba huu una ubadhirifu mkubwa na Serikali inaibiwa pesa nyingi sana, lakini Serikali ikauchuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG akaja mwaka 2009 ninayo hapa taarifa, akaelezea vizuri kupitia ukurasa wa 135 namna ambavyo Serikali inapoteza pesa na mkataba ulivyokuwa umekaa kijizi-jizi. CAG ameeleza vizuri sana, kwa sababu ya muda nashindwa kusoma, lakini Waheshimiwa Wabunge wakipata nafasi wapitie hii ripoti ya CAG ya mwaka 2009, ameeleza vizuri sana. Ufisadi huu Ndugu Ludovick Utouh ameupambanua vizuri sana na huyu ni CAG mwingine tofauti na wa sasa hivi lakini mpaka hapo Serikali bado ikaendelea kuuchuna. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akaja CAG mwingine Profesa Mussa Assad mwaka 2018 na ninyi mnajua ni juzi tu hapa. Ukiangalia ukurasa wa 131 ameeleza vizuri namna gani na amechambua kwa mahesabu, tunapoteza fedha kiasi gani kwenye mkataba wa kijizi ambao tumeingia mwaka 2004, lakini mpaka sasa Serikali hii bado mnauchuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naongea hapa, hasira za Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwenye mkataba wa IPTL nategemea kuziona kwenye mkataba wa Songas kwa sababu hawa ni Kulwa na Doto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Bunge lako Tukufu liunde Kamati. Kama hili jambo limekuwa likipigwa danadana toka mwaka 2004 mpaka sasa na tumeshapoteza trillions of money, naomba Kamati iundwe iweze kuchunguza jambo hili. Tetesi zilizopo ni kwamba suala hili limefunikwa na kigogo mkubwa ambaye hagusiki kwa namna yoyote ile na ndiyo maana Serikali inakuwa inasuasua katika kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kauli ya Serikali itakuwa haijanyooka vizuri, naahidi kuleta Hoja Binafsi humu ndani, mbivu na mbichi zijulikane. Haiwezekani tukaendelea kuibiwa namna hii. Naomba nitangaze rasmi, mwenye masikio asikie, mradi wa Songas ni mali ya Serikali, Songas ni mali ya wananchi na Songas ni mali ya Taifa. Naongea kwa ujasiri huu kwa sababu naamini kwamba Serikali ili-invest pesa nyingi sana kwenye mradi huu lakini haipokei chochote kutokana na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tabia hizo hizo za kuendelea kupuuza hivyo hivyo, kuna mambo ambayo niliyazungumza hapa mwaka 2016/2017 lakini mpaka leo Serikali haijachukua hatua yoyote. Hizi sheria tumezitunga wenyewe, tumezipitisha wenyewe, pale ambapo tunaona sheria zinavunjwa ni vema hatua ikachukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye transfer of shares ambayo hata kwenye Kamati Mheshimiwa Waziri nilihoji lakini majibu hamkunipa, nikahoji FTC majibu hawakunipa, nikamfuata Mkurugenzi wa TPDC personally majibu hakunipa, alikuwa anababaika tu. Kulikuwa kuna transfer of shares kutoka vitalu vya gesi kutoka Kampuni ya BG kwenda Kampuni ya Shell. Utaratibu uliopo ni kwamba, kama kuna transfer of shares yoyote, ukiangalia Financial Act ya mwaka 2012, kipengele cha 29 kinaeleza kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda za mzungumzaji)