Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini pia ninampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo kwa kuendelea kulisaidia Taifa hili kwa kupitia taaluma yake na uzoefu wake ndani ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba hata kuna baadhi ya Wabunge hawajui majukumu ya Kamati ya Sheria Ndogo na hata kutamka hili neno unakuta mtu anasema sheria ndogo ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge linatunga sheria, lakini sheria inapotungwa na Bunge haiwezi kwenda kutumika bila kutungwa kanuni. Kanuni hizo zimekasimishwa kwenye taasisi kuanzia kwenye Halmashauri hasa kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tunapotunga sheria, sheria nyingine zinakuja zinapitishwa kwa haraka sana lakini kanuni zinachelewa zaidi na pamoja na kuchelewa zinakuja na makosa mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kanuni zikitungwa zikawa kinyume na sheria mama na tunaamini sheria mama ndiyo dira yetu ndiyo katiba tunayoitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilichangia hapa kuhusu suala la sheria ndogo kwenda kinyume na sheria mama na nikaomba Wizara ya TAMISEMI ambayo iko chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiyo inayoongoza kwa makosa na madudu mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa sehemu wamefanyia kazi lakini ningependa wajue kwamba tunapozungumza haya mambo tumefanya utafiti. Yawezekana suala la kubana matumizi limepelekea hasara kubwa sana. Hawa watu hawapewi semina elekezi na inapotokea sheria hizi zikawa zimeshaanza kutumika ndiyo tunakuja kugundua Kamati ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo sisi sio watunzi wa sheria, lakini makosa yanayokuja yanaanzia kwenye utunzi wa kanuni yenyewe na inakuwa tayari imeshaanza kutumika. Makosa haya mengine yanafanyika kwa makusudi na hili jambo limeongezeka zaidi kwenye awamu ya tano kwenye suala la ukusanyaji wa mapato, ile tamaa ya kukusanya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanatunga kanuni mpaka wanakwenda kinyume na sheria mama. Sasa ningependa kuishauri Serikali, ni vyema, hasa Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Fedha waende kufanya utafiti upya. Aidha, wanasheria wetu uwezo wao ni mdogo au kuna watu wanawaendesha ina maana wanaacha taaluma zao wanafuata maagizo ya kutunga hizi kanuni ambazo zinakwenda kuwaathiri Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo kuwa na makosa ya kiundishi hii Sheria Ndogo mpaka ije ipite inakuwa imepitia kwenye hatua mbalimbali, hatuamini kwamba mpaka inaanza kutumika hawa watu wote hawajaona. Tungeomba Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali ifuatilie kwa kina, aidha, kuna kuna upungufu mkubwa wa waandishi wa sheria au hatuna kabisa au hakuna vigezo sahihi mnavyovitumia kuwapata hao waandishi wa sheria. Kama na huko mtaingiza siasa ndiyo hali inakuwa ngumu zaidi kwa sababu hizi sheria zinakwenda kuwaathiri Watanzania wa chini kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo kutorejea kanuni sahihi; bado wanarudia makosa yale yale, kwa sababu mpaka ianze kutumika imepita hatua kadhaa; hawa watu wako wapi? Mbona hatujaona hatua kadhaa zikichukuliwa kama watu wengine wanavyochukuliwa makosa ambayo yanakuwa yanafanyika ni ya kawaida kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutorejea jedwali sahihi, yaani hawa watu, inapita kwa mtu wa kwanza, mtu wa pili mpaka inaanza kutumika jedwali tu kwamba anarejea jedwali ambalo si sahihi na kile kitu anachokizungumzia. Hivi ni suala la kuja kujadili ndani ya Bunge, hayo ni mambo ambayo tunayafanya Sheria Ndogo sisi tunajeuka kuwa waandishi wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijasoma law nimesoma Community Development inabidi utumie akili nyingi kufikiri. Sasa Mwanasheria Mkuu utuambie, aidha na wewe umeshindwa kutimiza wajibu wako au ofisi yako inapwaya. Kwa sababu hizi sheria tunaposema hatuzungumzii kwa sababu Waziri kama sheria imepita hapa ndani ya Bunge yeye ana mamlaka ya kutunga kanuni; unatunga kanuni ambayo inakupa mamlaka zaidi na mpaka inaanza kutumika ina makosa mpaka tunarudi ndani ya Bunge tunazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri ni vema sasa kwa kuwa Bunge limekasimu mamlaka yake kwenye Kamati, kabla sheria hizi hazijaanza kutumika, hazijawa gazetted, sheria ikishatungwa kanuni ziletwe hapa mara moja baada ya kwamba sheria zimepita ili tuweze kupitia kanuni hizo kama zina usahihi na baadae ndiyo ziwe gazetted zianze kutumika kwa Watanzania kwa sababu zimewathiri Watanzania wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kama kuna uharaka kiasi hicho, yaani manaleta tayari zimeshaathiri watu, kwa hiyo tunataka ziletwe kabla hazijaanza kutumika tuziangalie kama zimekwenda sawa sawa na sheria mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kanuni la Baraza la Sanaa la Taifa. Mheshimiwa Mwakyembe nafikiri hili jambo uliangalie vizuri. Hawa wasanii mnakuja kuwaangalia wakiwa wameshatumia nyingi ndiyo mnatunga kanuni ambazo wala hazieleweki. Wakati mwingine hili jambo linakuwa gumu kwa sababu ushirikishwaji wa wadau unakuwa mdogo na mkiwashirikisha mnawatafuta wale makada makada wale ambao wakija wanapitisha tu halafu baadae zikianza kuwaathiri ndiyo wanaanza kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu msanii ili afahamike kwamba ni msanii anatumia nguvu zake za ziada sana na hakuna mkakati wowote ambao wizara mmeuweka wasanii wale wa chini, ila ninyi kazi yenu ni kuandaa kanuni ambazo zinawafanya ninyi mkusanye pesa. Ni jinsi gani mnawasaidia hamna utaratibu wala mkakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara ya Habari kama nia yao ni kuinua vipaji na michezo vya watanzania, wasijikite kwenye kukusanya pesa na kuweka adhabu ambazo zitawazuia wao kukuza na kuondoa vipaji vyao kwa sababu kuna wakati mwingine tumeshuhudia huyu Diamond ni msanii mkubwa, kuna kanuni nyingine mnatunga kwamba anavyoenda kwenye tangazo alipie milioni tano. Kuna msanii wa hali ya chini kabisa, hiyo milioni tano anaitoa wapi ina maana mnamzuia yeye mnakwenda kumtafuta mtu ambaye tayari ameshafahamika na hao ndiyo watakuwa wanaendelea kukua kila siku, wale wa chini kabisa ni vigumu sana kuweza kuonesha vipaji vyao kwamba wao wanafahamika wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tena Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumieni ofisi yenu vizuri. Kama shida ni fedha za kuwapa semina elekezi watendaji wenu huko chini, hali ilivyo kwenye Halmashauri ni mbaya sana. Kama Rais alikuja kuzungumza ndani ya Bunge kuhusu tozo, zile tozo kama hamjui tunawaambia tena kanuni zilizotungwa huko chini zinakwenda kinyume kabisa na yale aliyozungumza hapa ndani na wanaoathirika ni watanzania wa hali ya chini kabisa. Kwa hiyo, ni vyema mkafuatilia yale mnayoyazungumza na siyo kuzungumza kwa ajili ya kujiridhisha wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.