Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, kwanza kabisa naunga mkono maoni ya Kamati na niwapongeze sana kwa kufanya kazi nzuri sana ambayo kimsingi imekuja wakati muafaka jinsi ambavyo tunaona watu wengi wanaoumia huku chini ni wananchi wanyonge ambao Serikali ya Awamu ya Tano imesema inashughulika nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ipo kwa ajili ya kumfanya binadamu awe bora, haipo kwa ajili ya kumkandamiza binadamu. Ukiangalia hizi sheria nyingi, hata kwenye Halmashauri zetu ni sheria ambazo zimekuwa kandamizi na zinazidi kuleta ugumu kwenye maisha ya huyu Mtanzania. Kwa hiyo, niseme Mheshimiwa Chenge pamoja na Kamati yako nikushukuru sana kwa kazi kubwa mliyofanya ya uchambuzi ambayo tukienda kwa kina kama wabunge tutaweza kuwasaidia watu wetu wasiteseke sana huko chini ambako kimsingi ndiko wanakoumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia sheria mama kwa mfano ya BASATA ambayo ilisainiwa na Baba yetu wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere mwaka 1985, kifungu cha pili kimeorodhesha kabisa ni nini sanaa, imefafanua nini ni sanaa, lakini kwenye kanuni alizotuletea Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe hapa ukisoma ukurasa wa 59 ameingiza pamoja na ukumbi nayo ni sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unashangaa ukumbi unakuaje nao ni sanaa, hata ukimuuliza mtoto wa darasa la pili; nina mtoto wangu anaitwa Simon, mtoto wa darasa la pili, ukisema taja kitu ambacho hakihusiani na sanaa azungushie pale, nadhani ukumbi ukiweka miongoni mwake atasema hakipo, sasa sielewi Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe amewekaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia sasa kwenye mambo aliyoyataja yanayohusiana na ukumbi. Anasema gharama za kibali kwa kumbi za maonesho sanaa na burudani zenye ukubwa wa kukaa watu wasiozidi 350 yaani unapokwenda kufanya maonesho hayo ukalipe shilingi 350,000 unapeleka BASATA, siyo unalipia ukumbi, unapeleka BASATA, bado ukumbi hujalipia, watu 350 unalipa shilingi 550,000 unapeleka BASATA. Ukumbi unahusianaje na sanaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikizingalia hizi kanuni za Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe zinakwenda kinyume kabisa na hii sheria mama ambayo Baba wa Taifa aliisaini. Hii inaonesha jinsi ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano iko desperate, inatafuta hela kwa gharama yoyote ambazo hazihusiani kabisa na masuala ya sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kumbi zenye ukubwa wa watu 750 na kuendelea mtu analipa 1,050,000 kupeleka BASATA, what is this? Hapo bado hujalipia ukumbi. Sasa hizi ni sheria kandamizi ndiyo maana narudia tena kwamba niwapongeze sana Kamati, mmefanya kazi kubwa kuangalia sheria kama hizi. Bado kuna kodi mbalimbali na siyo ukumbi tu, sasa haya ni mambo ya kuwanyonya na kuwakatisha tamaa hawa wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kwamba Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe ame-withdraw hiki kitu, lakini bado nasema hii sheria tungetoa maamuzi kwamba isifanye kazi, isimame kwanza kwa sababu ina mapungufu mengi, BASATA bado wanaitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ni sheria hii hii ilimzuia msanii ambaye amejaribu kuiweka Tanzania kwenye ramani, Diamond, wamemzuia anataka kwenda nje, vijana hawa wako talented, wanajaribu kutafuta pesa lakini kwa sheria mbovu kama hii tumemzuia asiende kutafuta pesa. Bado hata wasanii wadogo ambao wanajitahidi wanaambiwa wanapotaka kwenda kwenye matangazo watoe shilingi milioni tano, huku ni kuwakandamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maelezo yenu yote mmesema mnataka mkuze vipaji, tutakuzaje vipaji kwa kanuni kama hizi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba sheria kama hizi zinakandamiza wananchi, zinaonea wananchi, ni wakati muafaka kwamba tufafanue kwa pamoja na ni vizuri sheria kama hizi zisiwe zinaanza kufanya kazi kabla hazijaja tukazipitia humu na wataalam vizuri ili ziwe zinafanya kazi, itasaidia kupunguza matatizo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linaendana na hili, kuna wakati mwingine kuna sheria hizi ndogo ambazo zimeainishwa kabisa kwa mujibu wa sheria. Kwa mfano tuna sheria za Serikali za Mitaa, nikichukulia mfano wa kesi ya Mheshimiwa Haonga. Mheshimiwa Haonga alifanya makosa kwenye kikao cha Halmashauri kwa mujibu wa mashtaka aliyopelekewa Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati mbaya Maafisa wa Mahakama wamekwenda kumshtaki kwa sheria nyingine tofauti na mahakama ambayo mpaka hakimu anasema mmemleta kwenye mashtaka haya wakati huyu makosa yake alitakiwa ahukumiwe na sheria ndogo ya ndani ya Manispaa. Kwa hiyo, maafisa wanapotosha, badala ya kuisadia mahakama kufafanua vizuri hizi sheria ndogo zinavyotumika, wanajikuta wanapotosha umma, wanatumia sheria nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawa na hapa Bungeni. Hapa tukikoseana kwa makosa ya kimaadili hauwezi kuchukuliwa hapa ukapelekwa mahakamani kule, ndiyo maana kuna Kamati ya Maadili hapa inakuita inakuonya. Lakini matokeo yake huko mitaani kwenye Halmashauri zetu watu wakifanya makosa ya kimaadili utakuta watu wanatumia madaraka yao vibaya wanawapeleka mahakamani kwa sheria zile mnaita criminal procedure, si ndiyo? Sheria za Makosa ya Jinai, wakati watu wamekosea. Kwa hiyo, hata hizo sheria ndogo zipo haziheshimiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wale maafisa wa Serikali tusaidiane tuwaelimishe wananchi, tusaidiane kuelimisha mahakama tuiongoze mahakama vizuri kwa sababu wao ni Maafisa wa Mahakama.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Chenge na Kamati yako nikupongeze sana kwa kazi nzuri ambayo kwa pamoja tutakwenda kuwasaidia wananchi wetu.