Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, namimi nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia hoja hii ambayo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, hoja hii ni muhimu kwa sababu Wizara ya Fedha ndiyo Wizara ambayo inategemewa kwa mambo mengi na Wizara hii inatakiwa ijikite na ijiweke sawasawa kwenye mambo mbalimbali. Mipango ambayo inatakiwa ifanywe na Wizara hii kwa ajili ya shughuli za maendeleo hapa nchini ni muhimu sana. Na ni muhimu kwa sababu ni mipango ya kimkakati ya maendeleo ambayo inaweza kutufanya kuinua uchumi wetu.
Sasa ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Tume ya Mipango ambayo imeanzishwa kisheria chini ya Sheria ya Mipango ikiwa kwenye Fungu 66 Tume hiyo imeondolewa sasa hivi, imeingizwa moja kwa moja kwenye Fungu 50 la Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, sasa nchi yoyote suala la mipango, suala la research, suala la plan ni muhimu sana. Sasa unapoondoa Tume ya Mipango unaiondoa unaiweka chini ya Wizara yaani ile mipango bwana mipango naye anatungenezea mipango aripoti kwa Waziri au kwa Katibu Mkuu, si atatengeneza mipango ambayo anaitaka. (Makofi)
Sasa hili ni suala moja na ambao Kamati ya bajeti imependekeza huo mpango kuondoa hili suala la Tume ya Mipango lirudi mara moja. Tunashauri sana ni muhimu sana, kwa sababu bila mipango hatuwezi kuwa na uchumi mzuri, hatuwezi kusema kwamba tunaendelea na mipango mizuri, uchumi unakua Tume ya Mipango lazima iwe independent na miaka yote imekuwa chini ya Ofisi ya Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni lazima hii irudi chini ya Ofisi ya Rais maana yake baadaye tutakuja kuisema CAG nayo iende chini ya Wizara haitakuwa independent, kutakuwa na check and balance za aina gani. Kwa hiyo, hilo ni wazo moja ambalo nashauri na Wizara iweze kulichukua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili ni suala la utoaji wa fedha za mifuko ring fence, hapa tumeona fedha mbalimbali ambazo zimewekwa kwa kisheria kabisa kwamba fedha hizi ziende kwenye mambo ya maji, fedha hizi ziende kwenye mambo ya reli, kwenye mfuko wa reli, fedha hizi ziende kwenye labda korosho, fedha hizo zinakwenda badala zinachukuliwa zinakaa palepale BOT. Sasa inakuwa ni muda mrefu kuna kitu kinaitwa letters of credits, letter credits (LCs), Benki Kuu inafungua tangu lini? LCs zinatakiwa zifunguliwe kwenye matawi kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tumeona hapa ucheleweshaji wa fedha za REA ambao baada ya Kamati kuingilia ndiyo haya mambo yameanza kuingiliwa. Sasa tumeona ucheleweshaji pia wa Mfuko wa Reli na baada ya Kamati kuingilia mambo hayo yameanza kutekelezwa. Sasa huu urasimu tunataka Wizara iuondoe na tufuate sheria, hizi fedha zinatajwa hizo zitakatwa kwa kufuata sheria. Kwa hiyo, tunaomba fedha hizi ziende kwa misingi ya sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni suala la michezo hii ya kubahatisha, hili suala la michezo ya kubahatisha sasa hivi limechukua kasi sana na ni nzuri sana kwa sababu Serikali inapata kodi. Lakini tatizo moja kubwa ni watoto ambao ni chini ya miaka 18. Sasa hivi wamekuwa wanachukua hela za wazao wao kuingia kwenye hii michezo. Sasa ni lazima Wizara iangalie namna gani inaweza kudhibiti hawa watoto wasiweze kuingia kwenye hii suala la kuingia kwenye michezo ya kubahatisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo namuomba Waziri alitolee ufafanuzi ni suala la shilingi milioni 50 za kila kijiji. Hili limeleta matatizo sana village empowerment, sasa suala hili katika bajeti ya mwaka 2016/2017 limetengewa shilingi bilioni 60, bajeti ya mwaka 2017/2018 shilingi bilioni 60. Lakini hakuna hata senti moja imetoka, sasa ni vizuri Waziri akikaa pale jioni atuambie kwamba kweli hizi fedha zipo au huu mpango upo kwa sababu ni kazi kubwa kwenye 2020.
Mheshimiwa Spika, mifuko ya PSPF, jana Naibu Waziri alijibu swali la askari wa magereza kwamba wamelipwa. Lakini ukweli na malalamiko mengi ya askari polisi ambao bado wako kambini hawajalipwa mafao yao kuanzia mwaka 2016/17 na 2017/2018. Juzi tu wiki iliyopita wakati naweka mafuta hapa mjini askari mmoja akanifuata afande mimi ni fulani fulani akaniambia; “mimi nimestaafu tangu mwaka jana ambapo ilikuwa ni mwaka 2016/2017 hatujalipwa” na wako kambini. Sasa wako Kambini ina maana kwamba wanasema hawawezi kutoka kwenye kambi kama hawajalipwa hizi hela zao vinginevyo hatapata kabisa. Sasa niliomba Mheshimiwa Waziri suala hili ulifuatulie kwa makini sana kwasababu haya malalamiko yao na hizi PSPF hawajalipa hizi fedha kwa kipindi cha miaka miwili, hawa askari walipwe hela zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la rufani za kodi, pamekuwa na mashauri mengi, report zinaonesha karibu mashauri 320 lakini katika mashauri hayo ni asilimia 31 tu ambayo mashauri haya yamesikilizwa. Sasa mashauri ya kodi, rufaa kwenye Baraza la Kodi yanakuwa ni mengi na hayasikilizwi kwa wakati, sasa ni vizuri Waziri aangalie utaratibu gani ambao utafanyika hizi kesi ziweze kusikilizwa na kwanini rufaa za kodi zinakuwa ni nyingi.
Mheshimiwa Spika, ningeshauri kwamba ni vizuri kuanzia kwenye utaratibu wa negotiations badala ya kuanza kukimbilia kwenye Mabaraza ya Kodi au kwenye makesi kwa sababu hawa ni walipa kodi ambao wanatakiwa waangaliwe kwa uangalifu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Msajili wa Hazina; pale tumeona kwamba kwenye report changamoto ambazo zimekuwepo ni baadhi ya wawekezaji ambao walikabidhiwa, walinunua mali za ubinafsishaji, bado mali zile zipo tu. Pamoja na juhudi kubwa na kelele nyingi za Serikali lakini hawa watu bado hizi mali wanazo na hakuna utaratibu wowote wa kuwanyang’anya, kama wamenyang’anywa basi ni kidogo sana. Ufanyike utaratibu, Msajili wa Hazina apewe madaraka, Msajili wa Hazina hata ukiangalia kwenye mafungu ambayo amepewa, amepewa hela ndogo sana. Sasa suala hilo Msajili wa Hazina akaangaliwa na kuweza kupewa hela ambazo zinatosheleza.
Mheshimiwa Spika, na suala la mwisho ni suala la ubia (PPP). Hiki kitengo ambacho kipo pale cha PPP hakijapewa umuhimu kwa sababu kitengo hiki kina maandiko mengi ambayo yanafanywa lakini mpaka sasa hivi pamoja na miradi mingi mikubwa ambayo inaonekana kufanyika hapa nchini lakini hiki kitengo ukiangalia fedha ambazo kimepewa ni kidogo sana na ni kitengo ambacho kinatakiwa kipewe nguvu, kipewe hela, kiweze kuingia kufanya lobbying na watu kiweze kuhakikisha kwamba tunaingia miradi mikubwa mikubwa hii kwa njia ya PPP.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja.