Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, nipende kupongeza uwasilishaji wa Wizara na Kamati ya Bajeti. Napenda kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu Deni la Taifa, nipende kuishauri Serikali kuangalia juu ya madeni haya ambayo yamesababisha mpaka vifo vya Watanzania wenzetu waliotoa huduma kwa Serikali kwa sababu ya kuchelewa kulipwa hivyo kushindwa kulipa mikopo na mabenki kuchukua mali zao. Ningependa kushauri Serikali kukopa mikopo yenye riba nafuu na kuwekeza kwenye miradi yenye kurudisha faida haraka ili mzunguko wa fedha hizo kuwa mizuri na kulipia madeni kwa wakati ili kuepuka riba kubwa.
Mheshimiwa Spika, wakandarasi wengi wanapata hasara kwani Serikali haiwalipi riba kwa pesa ambayo inacheleweshwa katika malipo ukizingatia wakandarasi hawa wanakopa kwenye mabenki hayo na wakichelewesha wanatozwa penalty.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vipaumbele kuwa vingi, ningeshauri Serikali kuwa na vipaumbele vichache ili kuweza kuvitekeleza kwa wakati hivyo kuokoa fedha badala ya kuwa na vipaumbele vingi ambavyo havitekelezwi kwa wakati. Mfano, tuna ujenzi wa Bwawa la Rufiji, reli, viwanja vya ndege, flyovers huku kuna huduma za jamii zinabaki zikisua sua.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mikopo mabenki ya ndani, niishauri Serikali kukopa mikopo nje badala ya sasa ambapo Serikali inanyang’anyana na sekta binafsi mikopo katika benki hizo hivyo sekta binafsi kukosa mikopo na kushindwa kujiendesha na kufunga biashara nyingi hivyo Serikali kukosa kodi ya kuendesa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kodi ya mapato, nashauri Serikali kuangalia upya juu ya kodi hizo kwani zimekuwa sababu ya wafanyabiashara wengi kuhama na kuhamia nchi jirani kama wafanyabiashara wa Tunduma waliomua kuhamia Zambia kutokana na kodi zilizo msururu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mashine za EFD, nipende kuishauri Serikali kuliangalia kwani mashine hizi nyingi ni mbovu, lakini pia upatikanaji wake ni wa shida, unalipia kisha unasubiri muda mrefu sana mpaka kupata. Pia bei zake ziko juu kiasi ambacho wenye mitaji midogo ni ngumu kulipa kwa mara moja. Serikali ingeanzisha ulipiaji mashine hizi kidogo kidogo.
Mheshimiwa Spika, kodi kabla ya biashara, niishauri Serikali kuondoa mpango wa Serikali wa kuwatoza kodi wateja wapya kabla ya biashara na kuwa-charge kwenye mitaji badala ya kuwa-charge katika faida ya biashara.
Mheshimiwa Spika, wawekezaji kutoka nje wamepewa muda wa matazamio, baada ya hapo ndiyo wanatozwa tofauti na sisi wazawa tunatozwa kabla ya biashara.