Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Deni la Taifa, Wizara hii ndiyo yenye jukumu la kusimamia Deni la Taifa. Mwaka 2017/2018 limezidi kuongezeka kwa dola za Kimarekani milioni 1,054.6 sawa na shilingi 2,320,120,000,000 kutoka USD milioni 19,957.6 sawa na 43,906,720,000,000 mwaka 2016. Hii
inatokana na taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania. Deni hili kubwa husababisha Serikali kulipa riba kubwa na kurudisha shughuli za maendeleo nyuma na kudumisha uchumi wa nchi. Deni hilo sio himilivu tena kwa sababu linaelekea kufikia nusu ya Pato la Taifa. Serikali ije na kutueleza ina mikakati gani ya kupunguza deni hilo badala ya kuendelea kukopa mikopo ya kibiashara yenye riba nafuu na kuendeleza kuongeza Deni la Taifa?
Mheshimiwa Spika, kuhusu utendaji wa TRA, ni vizuri wafanyakazi wa TRA wakatoa elimu kwa wafanyabiashara jinsi ya kulipa kodi badala ya kufanya kama wanakomoa wafanyabiashara. Je, ni kwa nini walimbikize mahesabu kwa zaidi ya miaka kumi ndiyo wafanye auditing? Halafu wanatoa fine za hali ya juu wakati biashara pengine haina hata mtaji wa kutosha na kusababisha biashara nyingi kufungwa kwa kukosa fedha. Kwa hiyo, hayo malimbikizo ya kodi hayana afya kwa wafanyabiashara na ieleweke wafanyabiashara hawakwepi wala hawakatai kulipa kodi, wapewe elimu, kitendo cha kuviziana na kuvamiana kwenye biashara ndicho huwasababisha baadhi ya wafanyabiashara kufikiria wananyanyaswa na kuonewa.
Mheshimiwa Spika, ni wakati sasa Serikali kuangalia haya matumizi ya EFD machine yanatumika vizuri na ziwe zinafanya kazi. Zaidi ya siku kumi mashine hizi nchi nzima zilikuwa hazifanyi kazi na kusababisha wafanyabiashara kushindwa kutoa receipt. Si hilo tu pia receipt hizi huwa zinafutika. Ni kwa nini kusiwe na mashine zinazoweza kudumu? Pia mashine hizo bei yake ni ghali sana kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wadogo, shilingi 700,000 hadi 650,000 ni nyingi sana. Ili Serikali iweze kupata mapato kwa kila mfanyabiashara ni vizuri Serikali ikagharamia mashine hizo ili kila mtu aweze kulipa kodi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini, fedha yetu ya Tanzania shilingi kama nchi tunachangia kwa thamani yetu kushuka. Je, ni kwa nini taasisi za Serikali zinapokea malipo kwa dola za Kimarekani? Mfano, malipo yote ya hifadhi mfano, Kilimanjaro, Serengeti na kadhalika lazima kulipia kwa dola. Nchi jirani zote na zingine duniani ni lazima kubadilisha fedha hizo kwenye maduka ya fedha na kulipa kwa thamani ya fedha ya nchi husika. Lakini hapa kwetu ni tofauti kabisa. Je, ni lini sasa Serikali itaziagiza taasisi hizi kuanza kupokea Tanzanian Shillings? Tusipothamini fedha zetu nani atazithamini?