Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, kuhusu Wizara ya Fedha kutekeleza majukumu yake, fedha ndiyo msingi mkuu wa utekelezaji wenye ufanisi wa shughuli zote za Serikali. Shughuli zote za Serikali zilizopangwa kutekelezwa katika sekta mbalimbali kwa mwaka fedha 2018/2019 hazitaweza kutekelezwa ikiwa hakuna rasilimali fedha. Hivyo sekta ya fedha ikiratibiwa na kusimamiwa vizuri matokeo yake ni utekelezaji mzuri wa shughuli za Serikali ambao hatimaye utapelekea ukuaji wa uchumi na ustawi katika Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka kadhaa sasa Wizara hii imeonekana kushindwa kuratibu baadhi ya mambo ambayo yapo chini ya madaraka yake, jambo ambalo limepelekea ukuaji wa sekta mbalimbali kuyumba. Ni vizuri Wizara ya Fedha ikasimamia jukumu la Deni la Taifa kwani Wizara inaonesha udhaifu mkubwa katika kusimamia Deni la Taifa, kwani deni hili linaendelea kuwa kubwa kila mwaka, jambo hili limekuwa na athari kubwa katika bajeti ya Serikali na hivyo kuathiri uchumi wetu na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mashirika mengi ya fedha duniani yamejitolea kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa nchi yetu, kwa kuwa hakuna uhakika kuwa mikopo hiyo itaweza kurejeshwa, matokeo ya jambo hilo Serikali imekosa namna nyingine ya kumudu gharama za kuendesha nchi badala yake imekimbilia kwenye mikopo ya masharti ya kibiashara jambo ambalo linaendelea kudidimiza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utendaji wa TRA na kero kwa wafanyabiashara; Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni chombo ambacho kipo chini ya Wizara ya Fedha. Kwa muda mrefu chombo hiki kimekuwa kikilalamikiwa na walipa kodi kutokana na kutumia mabavu kuwanyanyasa na kuwadhalilisha walipa kodi wakati wa zoezi la kukusanya kodi. Vilevile ushuru wa forodha wakati mwingine unakuwa mkubwa kuliko thamani ya bidhaa, jambo linalowafanya wananchi kushindwa kununua bidhaa.
Mheshimiwa Spika, ni vizuri TRA kuwaelimisha walipa kodi ili watambue umuhimu wao katika kulipa kodi na siyo kuwavizia kwa kuwategeshea makosa ili wawatoze faini, kitendo hiki ni cha kihuni na kamwe hakiwezi kuwa njia bora ya kukusanya mapato ya kodi. Pia kunakuwa na usumbufu kwenye ushuru wa bandari hasa kwa upande wa Zanzibar kwani wananchi wanalipa kodi mara mbili, unalipia bandari ya Zanzibar na bandari ya Dar es Salaam. Ni gharama kubwa sana hadi wafanyabishara wanalalamika na kushindwa kuuza bidhaa kwa wingi kutokana na kodi kuwa kubwa, hii imekuwa ni kero kubwa kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kuhusu malipo ya mafao kwa wastaafu, Wizara hii ya Fedha pia ina jukumu la kusimamia malipo ya mafao kwa wastaafu. Mafao ya wastaafu katika nchi hii yameendelea kuzua migogoro mbalimbali katika jamii. Kuna makundi mengi yana malalamiko kuanzia wanajeshi waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wastaafu waliokuwa watumishi wa umma ambao wamebaguliwa na Sheria ya Mafao kwa Watumishi wa Umma, pia kwa sasa asilimia kubwa ya watumishi wanalipwa mafao yasiyoendana na hali halisi ya maisha.
Mheshimiwa Spika, wastaafu wako kwenye hali ngumu ya udhalilishwaji na umaskini uliopindukia. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na aibu kwa Taifa. Ni vizuri Serikali ifanye mabadiliko ya sheria zote zinazohusu mafao kwa wafanyakazi katika sekta zote za ajira nchini na kipaumbele kiwekwe kwenye marekebisho ya Sheria ya Pensheni. Vilevile Serikali iwe inawahisha mafao kwa wastaafu pindi wanapostaafu, kwa kuwa sasa hivi kuna malalamiko mengi miongoni mwa wastaafu kutokana na kucheleweshwa kwa mafao hayo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgao wa fedha za maendeleo katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; licha ya Wizara hii ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kufanyiwa upendeleo na Serikali kwa kutengewa fedha nyingi, huku Wizara nyingine zikitaabika kwa kutopelekewa fedha za maendeleo kwani kuna maslahi gani makubwa ya msingi katika sekta ya ujenzi na uchukuzi kuliko miradi ya maji ambayo kutotekelezwa kwa hayo kunagharimu maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgao wa fedha katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi; hakuna hata shilingi moja ambayo ilikuwa imepokelewa kutoka Hazina kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya mifugo. Pia ukiangalia trend ya uwekezaji wa Serikali kwenye sekta ya mifugo ni dhahiri kwamba sekta hii japokuwa inahudumia takribani asilimia 50 ya kaya zetu lakini inapewa umuhimu mdogo sana.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayoikabili tasnia ya mifugo ni namna ya kufikia viwango vya ubora wa mifugo vitakavyokidhi mahitaji ya soko la kitaifa, kikanda na kimataifa. Je, tunatokaje katika changamoto hizo wakati ambapo Serikali haiwekezi katika tasnia hii. Hata ukiangalia rekodi ya miaka ya nyuma mifugo na uvuvi siyo kipaumbale cha Serikali hii ingawa ndiyo sekta inayotegemewa na takribani asilimia 50 ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgao wa fedha za maendeleo katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; kumekuwa na uwiano kinzani kati ya bajeti ya matumizi ya kawaida na bajeti ya maendeleo katika sekta ya elimu. Bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikiongezeka katika sekta hii, bajeti ya maendeleo imekuwa ikipungua. Bajeti hafifu ya maendeleo ya sekta ina athari kubwa kwenye elimu ya msingi. Kwa kipindi kirefu utekelezaji wa bajeti ya maendeleo umekuwa hafifu.
Mheshimiwa Spika, ubora wa elimu unategemea sana utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu ambayo imejikita zaidi katika kuboresha sekta hiyo. Ikiwa miradi haitekelezwi ipasavyo, tusitegemee muujiza wa kupandisha viwango vya ubora vya elimu hapa nchini, bali tunazidi kushusha viwango vya ubora na hatimaye kudumaza sekta nzima ya elimu. Ni kwa nini bajeti ya maendeleo katika sekta ya elimu inapungua?
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgao wa fedha za maendeleo katika Wizara ya Kilimo, bahati mbaya sana kwamba hakuna uwekezaji wa maana uliofanywa katika sekta ya kilimo hapa nchini kwani inatakiwa kutenga angalau asilimia kumi ya bajeti ya Taifa na kuielekeza kwenye sekta ya kilimo ili kusaidia ukuaji wa sekta hiyo. Je, ni muujiza gani utatendeka ili kilimo kiweze kusukuma uchumi wa viwanda ikiwa Serikali haitengi fedha za kutosha katika sekta hiyo?
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana sekta ya kilimo imekuwa haipewi umuhimu kama ule iliyonao katika uchumi wa nchi kwani kilimo siyo kipaumbele kwa Serikali.
Ni vizuri kuzingatia uwekezaji katika sekta muhimu za uzalishaji kama kilimo ili sekta hizo ziweze kuzalisha fedha ambazo zitatumika kulipa madeni mbalimbali, ni vizuri Serikali ikajenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mgawanyo wa fedha kwenye Wizara mbalimbali; Wizara ya Fedha kupitia Hazina ya Mfuko Mkuu wa Serikali ina jukumu la kupeleka fedha katika Wizara mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya utendaji wa siku hadi siku wa shughuli za Serikali. Pia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya Wizara husika. Siyo vizuri Serikali ikichelewa kupeleka fedha kwenye Wizara na Idara mbalimbali za Serikali au kutoa fedha pungufu au kutokutoa fedha kabisa. Ni vizuri Serikali kuandaa makisio yake ya mwaka yanayoshabihiana na makusanyo ya mapato, kwa kufanya hivyo, shughuli zilizopangwa zitatekelezwa kama zilivyopangwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kesi za kodi kutosikilizwa; kuna malalamiko ya muda mrefu ya kuwepo kwa kesi za kodi za muda mrefu katika Bodi ya Rufaa za Kodi, suala ambalo limekuwa ni kikwazo kikubwa kwa upande wa wafanyabiashara (walipa kodi). Pia kuna tatizo kubwa la ufinyu wa bajeti, hivyo kuathiri kufanyika vikao vya kutosha na kusikiliza kesi kama inavyotakiwa na sheria. Kutokana na hilo baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu wanatumia mwanya huu kuchelewesha malipo ya kodi kisheria kwa kupeleka kesi zao kwenye taasisi hizo wakijua itachukua muda mrefu kusikilizwa.