Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtemi Chenge, ahsante sana kwa fursa hii. Nimesimama hapa nikiungana na Waheshimiwa Wabunge walio wengi kuipongeza sana Serikali. Kwa kuanza kabisa, naunga mkono hoja ya Serikali iliyoko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utangulizi wetu kwenye hotuba hii ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi inasema namna ambavyo hotuba hii imeandaliwa, lakini moja ya mambo yaliyozingatiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hapa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, nikiwawakilisha pia Watanzania kwa ujumla wake kwamba, hivi karibuni tumesikia taarifa zilizoenea kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, kwamba ule utengenezaji wa kivuko cha pale Kigongo Busisi, eneo ambalo linaunganisha Wilaya ya Misungwi kwa Mheshimiwa Charles Kitwanga pamoja na Busisi upande wa Sengerema sasa uko hatua za mwisho kabisa na kile kivuko kimeshaanza majaribio kwa sababu, kimeshashushwa ziwani tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 hadi mwaka 2020. Kwa hiyo, kwa dhati kabisa naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, natumia fursa hii kuishukuru sana Serikali na nitataja baadhi ya Mawaziri kwa mambo ambayo wameiwezesha hivi karibuni kwa taarifa nilizonazo. Kwanza ni Mheshimiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo. Wanakatunguru pale Jimboni Sengerema kwenye Kituo chetu cha Afya, mjiandae tumepata fedha za maboresho shilingi milioni 400 zinakuja. Sengerema Sekondari tumepata zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya maboresho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia utekelezaji wa miradi ya maji Sengerema na Taifa kwa ujumla, nasi hujatusahau, maelekezo yake yanaendelea kusimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri, Mheshimiwa Kakunda ufuatiliaji wa malipo ya fedha zile, ziara yake imezaa matunda, tumeshapata fedha kwa ajili ya Mkandarasi wa mradi wa maji Buyagu, Kangalala, Bichocho na utaratibu wa ukamilishaji unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy kwa msaada wake ambao ametupa. Nataja hawa wachache kwa niaba ya Serikali nzima kwa sababu muda hauruhusu kutaja wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizamia kwenye hotuba yetu iliyoko mbele yetu na hasa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Taarifa za Kiserikali pamoja na Kamati; naipongeza sana Serikali, lakini pia Kamati ya Bunge ya Bajeti pamoja na Kamati ya Uongozi kwa ujumla wake kwa maelekezo ya Mheshimiwa Spika, kwa namna ambavyo walizitumia zile siku sita kushauriana. Wameshauriana mambo mengi. Yale mazuri tumeshayasema sana na yapo wazi, lakini katika Taarifa ya Kamati ya Bajeti, pia zipo changamoto ambazo ziliainishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie changamoto inayohusu sera za matumizi, kama ambavyo imeainishwa katika Taarifa ya Kamati ya Bajeti na hasa katika ukurasa wa 32, wakati nafanya mapitio na kupitia taarifa hiyo kuhusu Mpango wa Fedha na Matumizi kwa mwaka huu wa fedha mpya unaokuja mwaka 2018/2019. Moja ya jambo kubwa lililojitokeza ni kwamba kwa miaka kadhaa sasa kama nchi tumekuwa na changamoto ya kutokidhi matarajio ama maoteo ya bajeti tunazozipanga hapa, aidha kwa kutotimiza malengo kutokana na vyanzo vya ndani, lakini pia kwa kutopata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameshauri hapa kwamba, kwa mujibu wa kanuni na ni jukumu la kikanuni, lakini pia inatokana na Katiba, kama Bunge tuna wajibu wa kuishauri Serikali; wameshauri kwamba suluhu ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ambayo Serikali inafanya sasa hivi, natambua ujenzi wa reli ya kisasa, Stiegler’s Gorge, lakini ununuzi wa ndege na miradi mikubwa kwa mfano kule Mkulazi pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iridhie ushauri wa Bunge lako kupitia Kamati ya Bajeti na michango ya Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa sasa kwa mazingira tuliyonayo na uwezekano wa kukusanya vyanzo vya mapato ambavyo tumeviainisha kwenye bajeti kwa asilimia 100 ni mdogo, tunaiomba Serikali na naamini kwamba Mheshimiwa Rais anafuatilia mjadala huu, tukakope kwa masharti nafuu. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri ametuthibitishia kwanza kukopa siyo dhambi, lakini sisi kama Taifa kwa mahesabu yetu bado tunakopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali itafakari jambo hili. Najua kuna kipindi fulani ilionekana kwamba pengine kukopa kungetuongezea madeni (liability), Deni la Taifa, lakini kwa nchi kama yetu, kama nchi tajiri zinakopa kwa nini sisi tujivunge kukopa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali ikakope kwa mikopo yenye masharti nafuu ya muda mrefu, tujipe muda kwa vyanzo vyetu vya mapato vilivyopo ndani, tupumue, lakini tuweze kutekeleza miradi inayogusa wananchi moja kwa moja, miradi inayohusu Sekta za Kilimo, ambacho ndiyo kipaumbele, kinabeba wananchi zaidi ya asilimia 66, lakini mchango wake tunaona kwenye pato la Taifa ni 4% tu. Hili ni jambo ambalo tunahitaji kuliongezea muda wa kulifanyia kazi vizuri. Kwa hiyo, tukakope, lakini tuishirikishe sekta binafsi na pia tufanye miradi kupitia utaratibu wa ubia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalizo lake, nchi zote duniani zinapoelekea kwenye chaguzi na hasa miaka ya uchaguzi, bajeti zake huwa zinaathiriwa kwa sababu ya suala la uchaguzi. Sisi Tanzania mwaka kesho tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka 2020 tuna Uchaguzi Mkuu; vyovyote itakavyokuwa hatuwezi kukwepa kwamba kuna rasilimali fedha nyingi na hasa ya ndani itakwenda kwenye uchaguzi. Kwa sababu hiyo ndiyo msingi katika mustakabali wa Taifa letu. Tutafanyaje kama hatutakuwa na mikopo yenye masharti nafuu ya kutusaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunaomba sana Serikali izingatie ushauri huu, tufungue milango, tukakope kwa masharti nafuu, tuendeleze nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchambuzi, lipo jambo nimeliona nikasema niliseme tu niishauri Serikali. Kwa namna ambavyo lipo kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti ni kama linaashiria hivi, kuna taratibu ambazo tumeziweka kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu ni kama kuna viashiria hivi tunaelekea kuvikiuka. Hatujafikia hatua hiyo, kwa sababu Hotuba ya Bajeti na Mheshimiwa Spika, alielezea vizuri sana siku ile wakati Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alivyowasilisha kwamba haya mapendekezo tunayoyajadili sasa hivi, sisi ndio tunatengeneza bajeti ya nchi. Nashauri kwa yale maeneo ambayo Kamati yenu mliyabaini Serikali isikilize ushauri, kwa sababu viashiria vyake sio vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza inaonekana kuna viashiria vya kukiuka sheria kuhusu matumizi ya fedha ambazo zimetengwa kwa maeneo maalum na hasa Mifuko mbalimbali ambayo imeanzishwa kisheria. Halijafikia pabaya kwa sababu, sisi ndiyo tunaamua, hebu tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine inaonekana Kamati imebaini kwamba Wizara ya Fedha na Mipango inaanzisha utaratibu wa kubadili matumizi ya fedha zilizotengwa kisheria kwa ajili ya matumizi maalum. Sasa hili siyo jambo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili la kupendekeza kuanzisha Akaunti Maalum ama Akaunti Jumuifu ya Hazina. Sasa ukisoma ukurasa wa 40 mpaka wa 41 tumeelezwa kwamba hii imetokana na makubaliano ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; lakini Kamati ya Bajeti ilipozamia kule imebaini kwamba kumbe sisi kama nchi tuna fursa ya kuliangalia jambo hili kwa namna yake; na madhara yake ni kwamba kama itaanzishwa hii single account maana yake ni kwamba hata ile Mifuko ambayo tumeanzisha kisheria tukatenga fedha, kama suala la umeme, masuala ya barabara, reli na masuala ya korosho na mengine, miradi ya maji, nazo zitahitajika kwenda kwanza Mfuko Mkuu wa Hazina halafu ndio zije. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa ushauri wangu ni kwamba jambo hili linahitaji mjadala mpana zaidi, ni zaidi ya kupitia kwenye bajeti hii, kwa sababu, tulianzisha sheria maalum na mpaka sasa ukiangalia ni kama hatujaathirika, matokeo yake naona mifuko ile imekuwa ikitekelezwa kwa utaratibu ambapo matokeo yake ukiyapima ni chanya zaidi kuliko hasi. Sasa labda tujipe muda zaidi tuangalie, tuendelee na utaratibu, twendenao kwa sasa, lakini kama kuna haja ya kufanya hivi, basi tufanye mjadala mpana zaidi kuliko ilivyo sasa kupitia utaratibu wa bajeti kwa sababu, tukifanya vile tunaweza kuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti tumeyabaini kwa mfano, makusanyo ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania, ziko fedha zaidi ya 1.5 trillion. Sizungumzii lile suala la CAG, zimesemwa hapa kutokana na masuala ya kodi kulikuwa na mabishano na makampuni fulani, hazijakusanywa kwa sababu ambazo hazijaeleweka. Sasa kama Serikali yenyewe kuna mambo haijayaweka sawa, tunashauri kwamba tusiongeze tena mzigo wa fedha zote kwenda kule. Tujipe muda kidogo, nadhani tunaweza kufanikiwa, lakini wazo inawezekana limekuja kwa nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naona kama kiashiria chake siyo kizuri, tunasema tukisoma Katiba yetu ya nchi, Ibara ya 145 na Ibara ya 146, zimeanzisha utaratibu wa Serikali za Mitaa maalum kabisa na zikatambuliwa. Hili jambo nilivyokuwa nalisoma kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti, ni kama vile Kamati inasema: “Kwa namna ambavyo baadhi ya hatua zinazochukuliwa za Serikali Kuu ni kama vile zinakwenda kuathiri uhalali na umuhimu wa kuwepo kwa hizi Mamlaka za Serikali za Mitaa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa siyo jambo zuri sana, kwa sababu, ile Decentralization By Devolution tuliyoanzisha miaka ile kwa mujibu wa Katiba, lakini pia mwaka 1998 kulikuwa kuna Tamko la Kisera na tunafahamu manufaa ambayo tumeyapata; na kwa sababu, kuanzisha utaratibu ule ilitokana na uzoefu ambao tuliona kwamba kuendesha nchi kwa msingi wa kutoka Serikali Kuu peke yake ni mgumu sana duniani na utaratibu huo umekwaza baadhi ya nchi nyingi tu duniani na ndiyo maana sisi tuka-opt kwenda kwenye hiyo route ya kusema tuwe na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za Mitaa ni Serikali kamili kabisa. Kwa hiyo, nashauri kwamba tupunguze uwezekano wa kiashiria hiki kushamiri kwa sababu bado tuna muda na jambo halijaharibika na Waheshimiwa Wabunge tulitazame Kitaifa zaidi, tusiangalie kwamba kwa kufanya hivi tutakuwa tunakwaza kitu gani, hapana. Ni kwa faida yetu, nami naamini kwamba utaratibu ule haujatuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunafahamu kwenye ngazi ya Halmashauri, wapo Madiwani, zipo Halmashauri zimeshindwa kufanya vikao vyake kabisa na hawajalipwa stahiki zao kwa sababu hakuna fedha. Ni kwa sababu tunazi- cripple. Nashauri kwamba, hili jambo tuliangalie tena na naamini kwamba bado tuna fursa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Deni la Taifa, napendekeza solution tu. Mengi yamesemwa, lakini nataka nirejee miaka ya 1990 ilivyokuwa. Serikali ilikuwa na utaratibu wa kununua dhahabu, baadaye baadhi ya Watendaji hawakufanya vizuri sana, hatukufanikiwa, tukajiondoa, lakini wakati tunajiondoa wakati ule bei ya dhahabu kwa mfano kwa kigezo cha ounce… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya dhahabu haikuzidi dola 270, leo ni zaidi ya dola 1,400. Kilichotokea ni nini? Shilingi toka miaka ya 1990 Serikali tulivyojitoa kwenye kununua dhahabu, shilingi yetu imeporomoka kwa kiwango cha 80% na wataalam wa uchumi wako hapa wanaweza kurekebisha, lakini dhahabu imepanda ka zaidi ya 700%. Tungekuwa na dhahabu zetu ambacho tungekuwa tunafanya katika wakati wa mshtuko, unatoa dhahabu yako kutoka kwenye ghala lako, unaingiza sokoni unauza, unapunguza Deni la Taifa. Nikadhani kwamba Serikali itafasiri hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa gesi. Miaka ya 1992 tulipigwa na ukame ndiyo maana yakaja masuala ya IPTL ambayo yamekuja kuliyumbusha Taifa, ilitokana na ukame. Kutegemea chanzo kimoja kuna risk kubwa.

Ninashauri kwenye eneo ambalo nalifahamu kidogo. Suala la gesi tuliyonayo, leo tunajivunia trilioni 57 cubic feet za gesi ambazo tunasema ni probable, lakini ukizileta sasa kwenye uzalishaji normaly unazalisha 30% ya hiyo gesi uliyonayo. Asilimia hiyo 57 tunayoizungumzia, unaongelea trilioni 10 ziko nchi kavu, trilioni kama 40 na kitu ziko baharini kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ianze kuwekeza kwenye hii gesi iliyoko nchi kavu, kwa sababu, tusitegemee chanzo kimoja tu cha miradi ya maji, ni hatari kubwa kwa Serikali ya viwanda ambayo tunaitarajia kama tutakuwa na chanzo kimoja. Miaka ya 1990 tulikwama na ndiyo maana tukaenda kwenye mipango ya dharura, matokeo yake tukaja kuyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda huu tunaouzungumzia, hauwezi kuhimiliwa na Megawati 2,100 tu za Stiegler’s Gorge ama za viwango vingine vilivyoko hapa, ni pamoja na miradi ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana. Serikali itafakari, twende kwa pamoja, uwekezaji wa Stiegler’s Gorge ni mzuri, lakini tusipuuze pia suala la uwekezaji katika sekta ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.