Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nami sina budi kuungana na wachangiaji wa hapo awali kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpango na Naibu, Mheshimiwa Dkt. Kijaji na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii ya Fedha ambayo kwa kweli ndiyo inakutanisha Serikali yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kusema kwamba mpango ni mzuri na kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, naomba kusema kwamba, mapendekezo yangu yanaenda moja kwa moja na Kamati yetu ya Bajeti ambayo sina budi kumpongeza Mwenyekiti wetu mahiri na Makamu wake, Mama Hawa Ghasia na Mheshimiwa Jitu. Kwa kweli, wanatuongoza vizuri na andiko lenyewe mnaliona kwamba limekaa vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, lililobaki ni Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Makamu wake ambao tunakutana nao mara kwa mara kutusaidia tu na sisi tuongeze zaidi yale tunayoyasema kwa namna ya ku-amplify. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, Mheshimiwa Waziri naunga mkono hoja iliyo mbele yetu, lakini nataka kufafanua mambo yafuatayo. Tuanze kabisa na Wizara yenyewe ya Fedha. Hii ni Wizara muhimu sana. Sina budi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuunganisha Fedha na Mipango, lakini naanza kuwa na wasiwasi nikiona mipango inafifia chini ya fedha. Nami kama mchumi, nakuwa na wasiwasi mkubwa sana nisipolisema hili kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie jinsi atakavyolinda capacity ya National Plan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa na naomba ieleweke kwamba bila kuwa na Commission for National Economic Planning itakuwa vigumu sana kujua tunakokwenda. Tunaweza tukajikuta katika mchezo wa juhudi bila maarifa na Mwalimu Nyerere alionya dhidi ya mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana suala hili la hatima ya National Plan Commission, sasa hivi ikiwa inafanya kazi vizuri ndani ya Wizara hiyo sio shida, lakini inakuwa na enabling legal framework ambayo inaruhusu mambo ya mipango kufanyika. Hili naomba liwe mezani na Mheshimiwa Waziri atufafanulie sasa kwamba anajipangaje? Dhana ya Commission for National Economic Planning tunailindaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; kwa kuwa tunangalia sasa bajeti ya Serikali, kuna suala zima la Mamlaka ya Waziri mwenyewe huyu. Nimefurahi sana; na kama Mwanakamati wa Bajeti tunaipongeza Serikali kwamba hatimaye wamekubaliana na mapendekezo ya siku nyingi ya Kamati kwamba, Waziri wa Fedha arejeshewe mamlaka yake ya uamuzi wa kusamehe kodi pale inapostahili, hususan katika mikataba ya wahisani au miradi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tupendekeze kama Kamati ilivyopendekeza kwamba mamlaka yake yasikomee kwenye miradi ya Serikali, lazima pia na Serikali ielewe kwamba, Halmashauri nazo ziweze kupata msamaha huu. Kwa hiyo, nafikiri mamlaka haya pia yawe total, yasiishie tu miradi ya Serikali, lakini yaende hata kwenye Halmashauri na miradi mingine inayoweza kupatikana yenye National interest.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kinachogomba ni lazima tuaminiane. Ifike mahali kama mtu amepewa dhamana ya Waziri wa Fedha, afanye kazi hiyo, tumwamini kwa sababu, tunajua kwamba atafanya in National interest. Tukiondoa mamlaka yake kisheria, anakwama na sisi tunakwama. Hilo naomba niliweke wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna dhana nzima ya ukuaji wa uchumi. Tunapongezana kwamba Tanzania ni kati ya nchi zinazokua kwa haraka, lakini mwisho wa siku ukuaji huu ni lazima uonekane pia kwa sura ya fedha za wananchi mifukoni au siyo? Kwa hiyo, sasa hivi wananchi walio wengi nadhani ni halali kusema kwamba hali yao siyo nzuri. Kama yale ninayoyaona Muleba Kusini kule kwangu kwa wale walionituma hapa, kwa kweli hali ni ngumu. Sasa tunafanyaje kusaidia wananchi wetu na wenyewe kuwa na ukwasi wa kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi kusema uchumi unakua, lakini hauonekani mifukoni mwa watu. Kuna njia mbili za kuboresha vipato vya wananchi. Njia moja ni direct income; Mheshimiwa Waziri hili analijua, lakini nyingine ni social income.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unapoleta dhana ya elimu bure, hiyo, ni njia moja ya kuboresha ukwasi wa wananchi, hawana haja tena ya kufanya michango. Sasa zile direct income zime-shrink. Mheshimiwa Waziri anajua, ni Mchumi, zime-shrink kiasi cha kwamba social incomes zinakuwa na impact kidogo. Kwa hiyo, sasa hivi tuko kwenye shule za msingi, kule kwangu Muleba Kusini watoto wamekuja, lakini hawajanywa uji, hawajapata chakula kwa sababu vipato vya wazazi havitoshi. Kwa hiyo, nataka kusema sasa suala la kuboresha ukwasi kwa kaya ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi zinakua. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri lazima pia ajue kuwa kuna indirect taxes, hasa tozo. Kwa mfano, kule kwangu Muleba sasa hivi bado naendelea kusema kwamba huwezi kuwasaidia wananchi kama hawauzi kahawa yao kwa haraka na kwa bei nzuri. Kwa hiyo, bado suala la kahawa ni kizungumkuti na unakuta kwamba sasa mwananchi anakwenda kubebeshwa mzigo wa kulipa madeni ya ushirika ambayo hakuhusika nayo. Hii ni njia moja ya kumdanganya mapato yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kahawa kwa mfano, Sh.400/= zitakwenda kulipia deni ambalo wananchi walikuwa hawahusiki nalo. Namna hiyo, unawanyima yale mapato yao ambayo wangeyapata kama direct icome. Kwa hiyo, suala hili la kuboresha ukwasi wa wananchi ni sehemu kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atuambie mikakati yake na hapo anahitaji wapangaji wake, Wachumi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyo mbele yetu, Kamati imeichambua kwa kweli kwa ufanisi mkubwa, lakini ukiangalia Deni la Taifa lilipofika hapa, naomba niseme kabisa, hii dhana ya kwamba deni ni himilivu, Mheshimiwa Waziri aje atuambie uhimilivu wake wakati linaswaga 49% ya mapato ya ndani. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba fedha nyingi zinapokwenda ku-service deni, hapo uhimilivu unaanza kuwa wa mashaka. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri a tuletee mikakati mizuri au majibu mazuri ya kutufanya comfortable, kutupa faraja kujua kwamba hili deni jamani tumejisahau wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati inaonesha kabisa kwamba uwezo; tunakopa zaidi, tunaendelea kutegemea kukopa, tunakusanya mapato ya ndani lakini yanaenda kwenye matumizi. Maendeleo yatakwama kwa sababu tunakopa na mikopo mingi ni mikopo ya kibiashara. Mheshimiwa Waziri ni lazima mkakati utafutwe kurudi kwenye mikopo ya bei nafuu ikiwemo kutafuta guarantees kutafuta ubia katika miradi mikubwa. Hata na Marekani mambo makubwa yamefanywa kwa ubia; Equity financing yamefanywa kwa government guarantees. Tukienda kichwa kichwa kwamba tunajitegemea, tunaweza kuja kuangukia pua. Nafikiri suala hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku nchi hii imesimama kwenye dhana ya Siasa ni Kilimo katika; katika nchi hii mtu ni afya; hiyo ndiyo miradi ambayo tumeiona. Sasa nimeshangaa sana kuona Mfuko wa Maji nao umepata hatima ya kutokupata fedha zote ambazo tunakusanya ambazo zimepangiwa. Tukisahau maji, tumesahau kila kitu. Maana yake kama nilivyosema, afya; maji ndiyo uhai na afya ni kitu muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyotangazwa hapo awali, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya jioni ambapo tunakusanya fedha. Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana kwa kuweka nguvu sasa katika kuboresha dhana ya usafi katika shule. Nataka niseme kwamba na mtoto wa kiume hatumsahau. Choo bora kinachojengwa kitajengwa pia na kwa watoto wa kiume na wenyewe watakuwa na sehemu yao na mtoto wa kike wana sehemu yao. Kwa hiyo, hili nalo nimeona nilifafanue. Tunamlenga mto wa kike lakini hatutaki kumwacha mwenzake nyuma. Kwa hiyo, tunakwenda pamoja kama tulivyo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti, nataka kusema kwamba Kamati ya Bajeti imefafanua mambo vizuri na sisi tunaongezea kama tulivyofanya, lakini hii dhana ya Mfuko Mkuu wa Serikali ni dhana nzuri, lakini kwani lazima imaanishe kwamba fedha zote hata zilizokusanywa na Halmashauri zije kwanza Hazina? Mfuko Mkuu wa Serikali kwangu mimi naona ni concept. Mheshimiwa Waziri nadhani anahitaji concept, wakati wote kweli Serikali Kuu tunakusanya nini? Siyo fedha zote zije pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.