Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi ninapenda kukushukuru kwa ajili ya kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba ya bajeti. Pia napenda kupongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli pamoja na Wizara hii ya Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri wake wanafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tumesikia sana humu ndani watu wakisema bajeti hii ni hewa ama bajeti ya tangu mwaka 2016 ni hewa. Sasa nashangaa sijui hawa ndugu zetu wanaishi nchi gani ambako hawaoni maendeleo makubwa anayoendelea kufanyika ndani ya nchi hii. Wenzangu wamesema tumeona mengi bajeti ya Wizara ya Afya imekwenda juu sasa hivi mpaka madawa yana-expire hayana watumiaji kule kwenye hospitali zetu, lakini bado watu wanasema bajeti ni hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchukua nafasi hii kupongeza sana Wizara ya Fedha kwa kuweza kuondoa tozo ya VAT katika taulo za watoto wetu wa kike. Kimekuwa ni kilio cha Wabunge wanawake na Wabunge wanaume ndani ya Bunge hili kwa ajili ya watoto wetu ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa shule kwa takribani siku 70 ndani siku zile zote za kusoma. Hili siyo jambo dogo, tunaishukuru sana Wizara hii na Serikali kwa ujumla, Mungu awabariki sana kwa jambo hili jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka kwa mtoto wa kike naomba nielekee kwa akinamama ambao muda mwingi wamekuwa wakitafuta maji na muda wao mwingi ukiwa

umepotelea kwenye suala zima la kusaka maji vijijini. Wabunge wenzangu wamezungumza suala la tozo ya Sh.50 kwenye mafuta, nami naomba niungane nao ya kwamba tuweze kutoza hiyo Sh.50 na kuweza kuongeza kwenye bajeti ya maji ili kuweza kumtua mwanamke ndoo kama ambavyo Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya 2015/2020 inasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba jambo lingine lolote katika maisha kwa mfano hata umeme unaweza ukawa ni option, lakini maji hayana mbadala. Kwa hiyo niiombe sana Wizara hii ya Maji iweze kupatiwa fedha na zaidi sana ipate hii Sh.50 ili kwamba akinamama waweze kuondokana na adha kubwa ya utafutaji wa maji na huku muda wao mwingi ukipotelea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumze suala la kutokupelekwa kwa fedha kwenye Halmashauri zetu mbalimbali nchini kwa wakati, pia fedha hizo zimekuwa hazipelekwi tu kwamba kwa wakati. Hii imekuwa ikiathiri hata ile asilimia 10 ya wanawake na vijana kwa kiwango kikubwa kwa sababu yale makusanyo ya ndani ambayo ndiyo yanapaswa kutoa asilimia 10 yamekuwa hayafanikiwi kwa kiwango kikubwa kwa sababu Wakurugenzi wetu wanaishia kutumia hizo fedha kwa ajili ya kukidhi matakwa na mahitaji mbalimbali katika Halmashauri zao kwa sababu ya kukosa fedha zile ambazo zinatakiwa kutoka Serikali Kuu kurudi kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali itazame hili kwa jicho pana kidogo ili kwamba fedha hizo kama ambavyo tulizungumza huku nyuma kwamba siyo ni za kihuruma huruma bali zipo kisheria ziweze kuwafikia wanawake na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hapa tumekuwa tukipendekeza katika Bunge hili kwamba kuna kundi maalum la walemavu. Hili kundi limesahaulika. Bado imeonekana asilimia tano vijana, asilimia tano akinamama, lakini bado naendelewa kushauri kama ambavyo iliwahi kushauriwa

hapa tutenge asilimia mbili katika hizo 10 ziende kwa walemavu. Hili ni kundi maalum. Mtu anaweza akawa na ulemavu wa kiungo kimojawapo lakini akawezeshwa na bado akaweza kufanya biashara ama kazi ambayo inaweza ikamfanya yeye na familia yake wakapata maisha. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kundi hili lizingatiwe la walemavu katika zile asilimia tano za vijana itolewe hapo asilimia moja na kwa akinamama itolewe asilimia moja zipelekwe kwa kundi hili rasmi la walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Waziri tumeona jinsi ambavyo amekuja na miradi ya kielelezo kama Stiegler’s Gorge mradi ambao kwa sehemu kubwa pia umekuwa ukibezwa. Niseme kama tulivyosema tunaelekea kwenye Serikali ya viwanda ama uchumi wa viwanda hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda pasipokuwa na umeme toshelevu. Kwa hiyo, naunga mkono hoja suala zima la huu umeme wa Stiegler’s ili kwamba tuweze kupata viwanda vya kutosha na hatimaye tuondoke katika umaskini na kuingia katika uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Waziri amekuja na Tax Amnesty kwa maana ya kwamba zimeondolewa riba katika madeni ya wafanyabiashara wengi wanaodaiwa, lakini muda uliotolewa nina wasiwasi kwamba hautoshi. Huu muda wa miezi sita kwa vile hawa watu wako hapa hapa nchini na hawaendi mahali popote na hawatoroki na Wazungu wanasema the payment delayed is interest saved, kwa nini basi Waziri asitazame namna gani wanaweza haidhuru hata miezi 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wamepewa muda mfupi wa miezi sita hii inaweza ikasababisha hawa wafanyabishara wakakimbia tena benki kwenda kukopa kwa riba ya juu ili kuweza kulipa haya madeni waliyopewa muda wa miezi sita. Hii inaweza ikaathiri working capital yao. Kwa hiyo, nilikuwa namuomba Waziri atazame namna gani anaweza akaangalia tena kwa mara nyingine, namna gani anaweza akaongeza huu muda kwani madeni haya yatakapolipwa bado uchumi wetu utaendelea kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote niwaombe tena wafanyakazi wa TRA wanapodai kodi waweze kuwa friendly na wale watu wanaowadai kodi. Tunajua kodi ni jukumu la kila Mtanzania na bila kodi nchi yetu haiwezi kwenda lakini haidhuru waweze kuwa na lugha rafiki na nina hakika Watanzania ni watu waungwana na waelewa watalipa tu hizo kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kumekuwa pia na changamoto kubwa kwenye suala zima la kilimo. Tumeona bajeti ya kilimo ya mwaka 2017/2018, ilikuwa imetengewa takribani bilioni 150, lakini sana kwa mwaka huu tumeona imeshushwa kwa asilimia 34.7 nini kimetokea. Huku tunazungumza uchumi wa viwanda. Viwanda vyetu vinategemea raw material kutoka sehemu kubwa ya wakulima kwa maana ya kwamba nchi hii ina wakulima asilimia zaidi ya 65 ama asilimia 66. Sasa kama bajeti hii imeshuka kwa kiwango hiki kama hatutaweka nguvu kubwa kwenye suala zima la kilimo tunatoa wapi malighafi ya kupeleka katika viwanda vyetu? Kwa hiyo, naomba sana Wizara itazame namna gani itaondoa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mwenyekiti, naunga mkono hoja.