Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti hii ya Serikali, hii ni mara yangu ya kwanza nachangia mjadala wa bajeti toka mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kushauri kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni kwamba mfumo wetu wa Bunge ni mfumo wa Kamati. Kamati za Bunge zinafanya kazi kwa niaba ya Wabunge wote. Kwa hiyo taarifa ambayo Kamati za Bunge zinaleta ndani ya Bunge, ndiyo taarifa ambazo zimefanyiwa kazi na kwa niaba ya Wabunge na Kamati husika. Kwa hiyo ni muhimu sana Waheshimiwa Wabunge kuwashauri tu kwamba turejee sana kazi ambazo wenzetu wamefanya kwa niaba yetu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kwamba panapokuwa na jambo ambalo unaona kundi la Wabunge wenzako wana mashaka nalo, jitahidi sana kuwaelewa kwa sababu humu Bungeni tunategemeana. Leo hii ukija humu Bungeni ukaanza kuwa-counter Wabunge wa kutoka mikoa inayolima korosho, kesho utakuwa na jambo lako hutapata mtu wa kukuunga mkono, hiyo ndiyo Parliamentary Politics. Parliamentary Politics ni Wabunge kushirikiana. Kama unaona mwenzako ana jambo hulipendi, busara inakwambia kaa kimya usiwapinge wenzako, kwa sababu wao ndiyo ambao wana-feel the pinch ya jambo ambalo linakuwa limetokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo naenda kwenye korosho moja kwa moja. Ukurasa wa 43 wa Kitabu cha Kamati ya Bajeti, kimeeleza wasiwasi wake kutokana na mapendekezo ambayo Serikali inaleta kuhusu kuweka fedha za kutoka kwenye mazao kuziingiza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilikumbushe Bunge mwaka huu 2017/2018, kama siyo korosho na transit goods kwenye forex tungekuwa na dola inakwenda mpaka kwa Sh.4,000. Korosho na transit goods ndiyo zimetusaidia kuingiza mapato ya fedha za kigeni, kwa sababu mazao mengine yote mapato yameporomoka. Pamba mapato yameporomoka ya fedha za kigeni, kahawa mapato yameporomoka na mazao mengine kama jinsi ambavyo Kamati ya Bajeti imeweza kueleza. Kwa hiyo, korosho ni zao ambalo limetuokoa, limeingiza dola za Kimarekani milioni 514 mwaka uliopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana tutazame nini kimesaidia korosho kuongeza uzalishaji na mauzo nje. Ni maamuzi tuliyoyafanya mwaka 2010 ya export levy asilimia 65 kwenda kuendeleza zao la korosho. Sasa hivi Serikali inataka kuchukua fedha hizo, itakuwa ni makosa makubwa sana kwa sababu unaenda kumshughulikia mtu anayefanya vizuri. Katika hali ya kawaida ilitakiwa Serikali ilete pendekezo asilimia 100 ya export levy iende kwenye korosho kwa sababu Mikoa inayolima korosho imeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi la kuzingatia hapa na ambalo Wabunge wa Mikoa ya Kusini wamelieleza vizuri sana ni kwamba fedha ambayo imetengwa kisheria wameichukua hawajairudisha, hawajaitekeleza sheria inavyotaka, halafu badala ya kulipa kwanza hizo fedha ndiyo waje na mapendekezo mapya, wanakuja na mapendekezo ya kuchukua na zingine zitakazokuja forever, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imefanya uchambuzi hapa. Shilingi Bilioni 755 fedha ambazo ziko ring fenced, ambazo zina matumizi maalum ya kisheria, Wizara ya Fedha haijazipeleka kule ambako kunatakiwa. Kawaida hapa tayari sheria imevunjwa! Sasa Serikali inapata wapi moral authority ya kuja na hoja ya kwamba sasa hizi hela zote sasa ziende Mfuko Mkuu wa Hazina, ni makosa makubwa sana ambayo tunakwenda kuyafanya, nami naungana mkono na taarifa ya Kamati ya Bajeti kwamba suala hili lisitekelezwe kama jinsi ambavyo linapendekezwa na Serikali.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni Treasury Single Account. Kwanza niseme kwamba wazo lenyewe siyo baya. Ni vizuri tuelewane hapo, wazo la Treasury Single Account si wazo baya, kwa sababu nimeenda kusoma kwenye taarifa za IMF na nitampatia nakala Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kuna working paper No. 10/143 iliyoandikwa na Sailendra Pattanayak nzuri sana inaeleza hili, lakini haielezi namna ambavyo Serikali yetu inataka kulifanya. Serikali yetu inataka fedha yote iingie Mfuko Mkuu wa Hazina na Serikali yetu inatuambia jambo hili ni la Jumuiya ya Afrika Mashariki, siyo kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama protocol zote ambazo tumesaini za Jumuiya ya Afrika Mashariki hakuna jambo hilo. Jambo hili ungeliona Afrika Mashariki kama tungekuwa tunaanza kutekeleza monetary union. Hatujaletewa hapa Bungeni protocol ya monetary union. Kwa hiyo, hoja ambayo Serikali iliileta kwamba hili jambo ni la Afrika Mashariki ilikuwa ni hoja ya kutushawishi tu, lakini siyo kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo hoja ni kweli Serikali ituletee hapa ni protocol ipi hiyo ya Afrika Mashariki ambayo inasema jambo hilo, siyo kweli! East Africa imetoa vigezo vya namna ya kuingia kwenye monetary union, ikiwemo nakisi ya bajeti na kadhalika, haijasema mtunzeje fedha zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zingine wanachokifanya hawasemi hela zote ziingie kwenye akaunti moja ya Benki Kuu au ya reserve bank na kadhalika. Wanachokifanya wanajenga system ambayo Hazina na Benki Kuu watajua pale Bariadi kuna balance cash kiasi gani siku ile wakati business day imefungwa. Kwa hiyo Serikali itajua kama ni cash management Serikali itajua Bariadi Halmashauri ina hiki, sijui Itilima Halmashauri ina hiki, Misungwi ina hiki, Kigoma ina hiki, lakini kilicholetwa na Serikali ni kwamba Kigoma tukikusanya tupeleke Benki Kuu, siyo sahihi! Kwa hiyo, nadhani Wizara ya Fedha ilitazame hili. Siyo jambo baya, hatuwapingi, liandaliwe vizuri na tulifanye kwa mazingira yetu ya Tanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hili jambo la stamp za electronic, msingi wa hoja siyo mbaya kwa sababu unaenda kudhibiti mapato, lakini tunatekeleza namna gani, lazima tulitekeleze kwa namna ambayo hatupeleki ushuru
kwa wananchi kinyemela. Kwa sababu kwa mazingira ambavyo lipo sasa hivi gharama kwa wananchi zitaongezeka. Waziri Mpango ametusomea hapa kwamba bidhaa za ndani soda, bia nini hazijaongezewa kodi, lakini ukitekeleza tu hii electronic stamp zinaongezeka kodi na baadhi ya bidhaa zitaongezeka kodi mpaka Sh.90 kama maji, soda na kadhalika. Kwa hiyo hatusemi kwamba ni jambo baya, liandaliwe utaratibu ambao likitekelezwa wananchi hawatapata madhara ambayo wanakwenda kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine mawili ya mwisho ambayo nitaenda kuchangia, Kamati ya Bajeti imezungumza kuhusu kodi, ushuru wa mafuta kwa ajili ya maji. Waheshimiwa Wabunge tulizungumza hapa wakati wa Wizara ya Maji na kuna consensus ya ndani ya Bunge kwamba tuongeze fedha kwenye ushuru, fedha Sh.50 ili tupate fedha za kutatua kero za maji kwa wananchi wetu, hakuna Mbunge ambaye hakuliunga mkono hili. Serikali haijaja na hilo wazo. Kamati ya Bajeti imependekeza kwamba Sheria ya Road and Fuel Tolls Act ibadilishwe tulete fedha hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha namwelewa ana wasiwasi wa masuala ya mfumuko wa bei na kadhalika, lakini namshauri Waziri wa Fedha akaangalie takwimu zake vizuri Dkt. Mpango. Ukiangalia mara ya mwisho tumepandisha ushuru huu kisawasawa ni mwaka 2007. Ushuru huu mwaka 2007 kwa dola (in dollar terms) ilikuwa ni senti za dola 0.42, leo ushuru huu kwa senti za dola leo 2018 ni senti za dola 0.34.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hali ya kawaida in real terms utakuwa umefanya marekebisho ya ushuru na katika hali ya kawaida Mheshimiwa Waziri wa Fedha ushuru ungepaswa kupanda kwa Sh.160. Kamati ya Bajeti inaomba Sh.50 tu lakini ushuru unaweza ukapanda mpaka Sh.160 bila kuathiri mfumuko wa bei, kwa sababu tutakuwa tunafanya rationalization na exchange rate kwa sababu hayo mafuta tunayanunua kwa
dola. Kwa hiyo ni sahihi kabisa kuhakikisha ya kwamba tuna-relate huo ushuru kutokana na dollar terms.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu, Waziri ametueleza hapa kwamba kipaumbele ni kilimo. Kilimo hakijatengewa fedha za kutosha, umwagiliaji haujatengewa fedha za kutosha. Ukifanya 160 Mheshimiwa Dkt. Mpango, akisema Sh.60 ziende kwenye umwagiliaji unapata shilingi bilioni 190 ambazo hata kwa ambao tunataka michikichi watu wanaoleta mafuta ghafi wameongeza kodi ili tuweze kuzalisha hayo mawese kwa ndani, si tunahitaji uwezekezaji, hela hii hapa kwa ajili ya kuja kuwekeza. Watu wa alizeti hela hiyo hapo kwa ajili ya kuja kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza katika Road and Fuel Act tufanye marekebisho hayo tuendane na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti na tunaweza tukaenda mpaka Sh.160 tukapata fedha za umwagiliaji, nchi ikajitegemea kwa mafuta ya kula ya kutosha ndani ya muda mfupi ambao unatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa, kuna makosa tuliyafanya mwaka 2016/2017, lazima tukiri. Matatizo ya kibajeti tuliyonayo sasa hivi, matatizo ya ukwasi wa fedha tuliyonayo sasa hivi ni measures tulizozifanya kwenye bajeti ya kwanza ya mwaka 2016/2017. Lazima tuanze kurekebisha, tulipandisha bajeti kwa thirty one percent (31%) ndiyo maana leo bajeti hii tunaijadili hapa ukilinganisha na mwaka jana imepanda kwa asilimia mbili tu ili kurekebisha makosa ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kosa tulilofanya mwaka ule ni kodi kwenye huduma za utalii. Kasi yetu ya kuongeza wageni wa utalii ilikuwa twelve percent (12%) kabla ya kuongeza hii kodi. Leo hii kasi yetu ni asilimia tatu. Nataka niwaambie jamani sasa hivi ukicheza na utalii, ukicheza na transit goods, Bandari ya Dar es Salaam na ukicheza na korosho ya kina Mzee Mkuchika shilingi itafika Sh.5000 au Sh.6000 kwa dola, sababu haya ndiyo maeneo yanayotupa forex sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba ile kodi ya ile VAT kwenye tourism services iondolewe. Pili sasa hivi kwenye mapendekezo haya kwenye kukodisha ndege pia tumeweka VAT tena. Tumeleta mapendekezo kwenye Finance Bill ya sasa hivi, namwomba Mheshimiwa Waziri aitazame. Kwa kweli kama tukisimamia vizuri na ikiboreshwa iwe electronic stamp tutapata fedha za kuziba haya maeneo. Napendekeza maeneo hayo yaweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango kuhusu mambo mengine nimepeleka kwa maandishi na tutajadiliana zaidi kwenye Finance Bill wakati wa mjadala kuweza kuboresha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.