Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyoko mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mpango pamoja na Naibu wake Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. Hali kadhalika shukurani hizi pia zifike Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kazi nzuri ya ukusanyaji ambayo inaendelea na watendaji wote walioko katika Wizara hii. Mwisho, lakini si kwa umuhimu bali kwa kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya.

Mheshimiwa Mwen yekiti, mimi ningetaka kuanza na hili hili la korosho ambalo naona kama linataka kuligawa Taifa. Sisi ni watunga sheria, sisi tunasimamia maslahi ya wananchi, hivyo ni lazima wakati tunafanya wajibu huo tuhakikishe kwamba ndimi zetu tunazielekeza katika kujenga Taifa na si katika kulipasua. Tutajadiliana kwa hoja, tutabishana kwa hoja mbalimbali lakini msingi wetu mkubwa uwe katika namna bora ya kujenga, siyo namna ya kuanza kugawana mbao za Taifa hili la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tukianza kuzungumza kanda, kanda, kanda naamini hatutabaki kuwa na Taifa linaloitwa Tanzania. Kwa hiyo nitoe rai sana kwa Waheshimiwa Wabunge tujadili ma mbo haya kwa hoja, kwa fact, kwa data lakini tusiingize haya mambo ya kuanza kuvutana kwa misngi ya Kanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili suala la korosho ambalo kwa Sheria hii ya Mwaka 2010, nataka nianzie hapo hapo kwamba, lazima kwanza pia tutafakari kwamba kwa hiyo miaka mitano, hizi pesa zilivyokuwa zinakwenda zimefanya kazi ya kuongeza uzalishaji kwa kiasi gani? Sasa hapa ni lazima Wizara ikiwezekana ifanye uhakiki wa namna bodi ilivyoweza kusimamia hizi hela tangu hiyo mwaka 2010 hadi sasa; je, ni kwa kiasi gani imeongeza tija si tu katika uzalishaji lakini kwa yale makusudio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu mojawapo ya kuanzisha hii export levy ilikuwa ni ku-discourage kusafirisha korosho ghafi kwenda nje ili ikiwezekana sasa tuwe na viwanda vya kubangua korosho. Hata hivyo tunachoshangaa ni kwamba viwanda vingi vya kubangua vimezidi kufungwa. Wameanza Feeder Hussein na kiwanda chao cha Premier cash wamefunga, Olam wamefunga kiwanda wamepelela Msumbiji, Mohamed Enterprises nae amefunga kiwanda; kwa hiyo lazima tuone huu mchakato mzima…

T A A R I F A . . .

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza anachofanya yeye ni kuwahisha shughuli. Nilikuwa nataka nije kwenye sababu, sababu mojawapo ambayo viwanda hivi vimeshindwa ni kwamba wenzetu India kule wao korosho ghafi wanaipa incentive. Kwa hiyo maana yake ni kwamba huku wakati tunaweka export levy ku- ban export wenzetu kule wanatoa incentive ku- encourage watu wasafishe korosho ghafi. Kwa hiyo kama viwanda binafsi vimeshindwa hata vya Serikali pia haviwezi vika-compete kwenye hilo soko. Kwa hiyo lengo hapa ni kwamba, tutafute mjadala wa pamoja siyo huu wa kutishana. Tukianza kutishana na wengine tunazalisha carrot, tunazalisha viazi tutaanza kusema na vyenyewe…

T A A R I F A . . .

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni hoja yake yeye, sasa hiyo atabaki nayo yeye, mimi ya kwangu ni hayo ambayo nimeyaeleza kwa maana kwamba tujadili mambo haya kwa mapana zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala la transit goods; TRA hapa lazima tuangalie, tuongeze wigo wa hizi siku, siku 30 ku-clear mizigo ni siku chache sana. Kwa nini nasema chache? Katika siku 30 utoe weekend, wiki nne ukitoa siku mbili mbili ni siku nane, kama itaangukia nayo kuna sikukuu nayo uitoe. Pia tunajua utendaji katika nchi yetu, kuna siku utaambiwa leo system haiko vizuri siku zinazidi kushuka. Kwa hiyo unaweza ukakuta kwamba utendaji kamili wa hizi siku 30 za ku-clear mizigo ni kama siku 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili jambo kwa mapana. Ili bandari yetu iweze kushindana na bandari nyinginezo kama Beira, South Africa na kule Angola, ni lazima tuhakikishe kwamba tunaongeza wigo wa siku angalau zifike 60 hadi hata 90 kwa sababu hili ni eneo ambalo tunaweza tukalitumia vizuri sana kuongeza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mzigo unaotoka labda Burundi au Rwanda ukifika pale unatakiwa ndani ya siku 30 uwe umeondoka. Kwanza utakapobaki tunapata storage, tunapata wharfage, kwa hiyo ni lazima suala hili tuliangalie kwa kina; lakini sambamba na mafuta ambayo yanasafirishwa kwenda katika nchi ambazo zinatuzunguka, yakifika siku 30 wanatakiwa waya-localise kama bado yamebaki. Kwa hiyo namshauri sana Mheshimiwa Waziri jambo hili aliangalie kwa kina, linaweza likatusaidia sana kuongeza mapato na pia likaweza kuifanya bandari yetu iweze kushindana. Hii itatusaidia pia kuboresha Bandari hizi za Mtwara na Tanga na hata Bandari mpya hii ya Bagamoyo kwamba zitakuwa za kibiashara zaidi kuliko hivi zilivyo sasa, inakuwa kama ukiritimba umekuwa ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningelizungumza ni suala la kilimo hasa tunapoanza na Benki hii ya Kilimo. Benki ya Kilimo walitakiwa waanze katika mikoa mitano Tanga ikiwemo lakini mpaka sasa bado hawajaanza shughuli zote katika Mkoa wa Tanga. Nadhani kuja kwa Benki ya Kilimo ilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kuja kufufua zao la mkonge ambalo zao hili sasa limeanza tena kupanda soko huko ulimwenguni. Kwa hiyo nimsihi sana asimamie katika eneo hili ili Benki hii ya Kilimo iweze kwenda kwenye ile mikoa mitano ambayo inatakiwa ikafungue matawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala la kuangalia ushuru katika bidhaa za ambazo zinaingia kama vifungashio; hivi vinaingia kwa zero tax kiasi kwamba sasa vinaathiri uzalishaji wa magunia. Viwanda ambavyo vinazalisha magunia kwa kutumia bidhaa ya mkonge kwanza vinashindwa kupata soko kwa sababu mkonge kidogo upo ghali na hata hii korosho tunayoizungumza ingekuwa ina maana sana kama tungeisafirisha katika magunia yaliyotengenezwa kwa mkonge, maana yake tungeongeza uzalishaji zaidi. Kinachotokea sasa hivi kwamba, tunaingiza vifungashio vinaingia bila ya kodi, vinasafirisha korosho na mazao mengine; kwa hiyo matokeo yake ni kwamba viwanda vinavyozalisha bidhaa za mkonge vinakosa kuzalisha, vinakosa kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nizungumzie suala la chikichi kule Kigoma. Mheshimiwa Dkt. Mpango anaona wenzetu wanaanza kugawana mbao za Taifa naye anatoka Kigoma. Nadhani uwe ni wakati muafaka wa kuhakikisha kwamba zao la chikichi kule Kigoma nalo linapewa umuhimu wa kipekee. Tukishakuwa na uzalishaji mkubwa wa michikichi; na nadhani kuna maandiko kadhaa kwenye RCC yao kule Kigoma wameshayapitisha, itaweza kusaidia uzalishaji wa mafuta tukichanganya na mafuta haya ya alizeti. Matokeo yake ni kwamba tutaweza kuondokana na hii adha ya kuagiza mafuta kutoka nje na ambayo wakati mwingine yanatuletea shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimsihi sana, michikichi iliyopo kule imeshazeeka sana, haiwezi tena kuzalisha mafuta haya. Kwa hiyo lazima tuanzishe utafiti mpya kwa ajili ya kuweza kuangalia hali ya hewa lakini pia tupate mbegu bora zaidi ambazo zitakuja kuwa na tija katika uzalishaji wa hili ambalo tunalikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, ambalo ningependa kuzungumzia suala hili la electronic stamp naye jana alilizungumzia vizuri. Nakubaliana naye kabisa kwamba hili suala ni vizuri tukaenda kwa hatua; tukaanza katika haya maeneo ambayo tayari wameshaanza stamps hizi kawaida, kwenye maeneo ya mvinyo, vinywaji, sigara na vinywaji vikali, kwamba tungeanza huku kabla hatujaingia kwenye hizi daily
consumable goods hizi soda, maji na juisi, kwanza tuziache tuanze na hizi hizi ambazo wameanza nazo ili tuone performance iko namna gani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.