Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMMANE J. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye bajeti yetu hii ya 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili au matatu kama muda utaniruhusu. Suala langu la kwanza alijaribu kuliongelea hapa Mheshimiwa Ngeleja. Suala hili la dhahabu tumekuwa tukiliongea leo mwaka wa tatu toka tumeingia hapa Bungeni, sijaelewa ni kwa nini Waziri Mpango hataki kulielewa. Mara ya kwanza mimi nilikuja na hoja ya one percent kwa dhahabu kwa watu wanaofanya export. Tuliongea na Mheshimiwa Mpango lakini baadaye sikupata jibu kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhahabu ni sawasawa na dola, sijaelewi kwa nini tunapuuza dhahabu ya wachimbaji wadogo ambayo ni karibu ya asilimia 70 ya dhahabu yote ya Tanzania na leo migodi yetu mikubwa imefungwa. Sisi tunaotoka maeneo hayo ya dhahabu tunaifahamu dhahabu vizuri sana. Benki Kuu ya Tanzania ilianza kununua, kama alivyosema mwaka 1991/1992, baadaye ilisimama baada ya matatizo yaliyotokea pale kwamba uaminifu uliokuwepo haukuwa mzuri kati ya wafanyakazi wa Benki Kuu na wafanyabiashara waliokuwa wanapeleka dhahabu pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiangalia trend ya dhahabu duniani, kama alivyosema Mheshimiwa Ngeleja, kwamba tangu mwaka 1999 kwa mfano dhahabu imekuwa ikipanda kwa speed nzuri sana. Serikali ingekubali kununua dhahabu kwa ushindani kwa bei ya soko la dunia kwa shilingi za Tanzania ingeweza kupata faida kubwa na ingeweza kuifanya pesa yetu kuwa imara. Sasa hivi kinachofanyika ni kwamba, Serikali inapotaka kulipa madeni lazima ichukue pesa za shilingi ika-source dola, lakini ingekuwa inanunua dhahabu ingeuza kipande cha dhahabu wakati inapotaka kulipa deni. Hii ingesaidia shilingi yetu vile vile isiweze kuporomoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nafikiri kinachotusumbua hapa huenda hii dhahabu ya local kwa kuwa haimo kwenye mitaala ya shule, labda kwa kuwa haiko shuleni kwa watalaam wa uchumi inawapa kigugumizi; kwa sababu Waamerica na Waingereza wanaotoa elimu hawana hiyo dhahabu ya kuokota mitaani. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa kwamba, kila ukimwambia mtu ambaye hafahamu anaona unaongea kitu ambacho si sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka 1999 kweli dhahabu ilikuwa dola 270 kwa Ounce, ambayo ni kama dola nane ama tisa; leo iko dola 1400 ambayo ni takriban dola 50. Kwa hiyo imepanda kwa asilimia 800. Pesa ya Tanzania mwaka 1999 ilikuwa 1,300 leo ni 2,300, pesa ya Tanzania ime-depreciate kwa asilimia 80. Kwa hiyo kama tungekuwa na stock ya dhahabu deni la Taifa tungelifuta lote mara moja na tusingekuwa na deni lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Mpango ajaribu aidha atuite watu tunaotoka maeneo ya madini, tujaribu kuongea na watalaam wake kama kuna sababu hasa, kwa maana hatupi jibu ni kwa sababu gani. Leo dhahabu yetu Uganda wana-charge 1.5 percent kwa export levy, Burundi 1.0 percent, Rwanda 1.0 percent; na watu hawa hawana mgodi hata mmoja na wote tuko Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sisi tunaletewa plastic na Wachina, sasa itawezekanaje? Sisi tuna kiwanda cha kuchapa dola, dhahabu ni dola, ni kama una kiwanda cha kuchapa dola, hutakiwi hata kufikiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo indication ya bei ya dhahabu duniani inaonekana kwamba itaendelea kupanda; nitatoa sababu tatu ambazo zinaonesha itaendelea kupanda. Sababu ya kwanza, ni kuwepo kwa sarafu mpya duniani; kuna sarafu ya Euro, kuna sarafu mpya ya China ambayo imekuwa imara, kuna sarafu mpya ambayo inatarajiwa ya nchi za Brazil, South Afrika na nchi za Asia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile dhahabu sasa hivi imeanza kutumika kutengeneza kwenye komputa na laptop, kiasi ambacho sisi ambao tunayo dhahabu, tunayo chance nzuri zaidi ya kupata faida kutokana na dhahabu. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Madini wajaribu, kama watalaam wao wanakuwa na kigugumizi kwa ajili ya matatizo yaliyotokea mwaka 1992, teknoloji ilikuwa bado, leo teknoloji ya dhahabu ni ya kugusa simu unajua ina percent ngapi ya dhahabu ndani yake; tunaomba wasiwasi huo uondoke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga reli kwenda Mikoa ya Mwanza na kwenda Mikoa ya Kigoma. Wajerumani wakati wanajenga walikuwa wakati huo huo wanaandaa na mazao ya kwenda kubebwa na treni ile. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mpango awekeze kwenye mazao ambayo treni standard gauge itakapokuwa imefika kule Kigoma na kule Mwanza licha ya abiria kuwe na mazao ya kuweza kubeba kurudi nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa idea ndogo tu, kwamba Malaysia kilichofanya wakafanikiwa kwenye michikichi ni kwamba walikuwa wanampa mtu mche wa mchikichi halafu kila mwezi wanamlipa pesa yule mtu. Baada ya miaka mitatu mchikichi ilivyoanza kutoa matunda yule mtu analipa. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aweke pesa pale, awapatie wananchi wetu michikichi na mikorosho awape Sh.1000 kila mche, gharama yake itakuwa Sh.40,000 peke yake kwa mche mmoja, lakini baada ya miaka mitatu atakuwa na miche mingi ya korosho nyingi na michikichi mingi. Kwa hiyo treni yake itakapofika Kigoma atakuwa na mizigo ya kurudi nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu, ningemalizia kwenye kodi ya viwanja na majengo. Tanzania ni nchi pekee ambayo ina-charge kodi ya viwanja na majengo kwa kumfata mtu. Nchi zote duniani zinatumia kwenye bill ya maji au umeme. Mimi kama kodi ya kiwanja ni Sh.24,000 au kodi ya jengo ni Sh.24,000 tunagawa kwa 12. Kwenye bill yangu ya maji unaleta elfu mbili ambayo inakuwa indicated pale kwenye bill ya maji au ya umeme. Nafikiri Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaweza akalichukua hili litamsaidia zaidi na hatakuwa na sababu yoyote ya kushinda kutwa nzima na majembe Auction Mart, kamata huyu, funga huyu, inaweza ikatusaidia sana sana, Mheshimiwa Waziri wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba nihitimishe mchango wangu kwa kuongelea suala la bandari. Bandari yetu ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri. Hata hivyo namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango aangalie zile bidhaa ambazo zinakwenda nchi za jirani, aongee na wafanyabiashara wa Kariakoo kwamba kwa nini bidhaa hizi haziuzwi hapa, ili aone ufumbuzi. Kama zinaweza kuteremshwa bei na hazina madhara kwa viwanda vya Tanzania ni vizuri ikafikia upya suala la kupunguza kodi juu ya bidhaa ambazo zinaweza kulipishwa ushuru hapa na wewe ukapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.