Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAU S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushuru kwa kunipatia nafasi hii jioni ya leo kuchangia kwenye bajeti hii muhimu kabisa kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. Pia niungane na Waheshimiwa wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia lakini ambao wameona umuhimu wa kuendelea kuishukuru Serikali na kuipongeza kwa kazi kubwa ambayo imeendelea kuifanya katika kuhakikisha inatatua changamoto za Watanzania. (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yetu ni kwamba bajeti hii ya mwaka 2018/2019, pamoja na muonekano wake wa kwamba inakwenda kujibu changamoto nyingi ambazo tumekuwa tukizijadili kwenye miaka mingi iliyopita, lakini yako mambo ambayo ni lazima sasa tuendelee kuyazingatia. Kwa sababu tumeamua kuyaleta sasa ni lazima tuyasimamie ili utekelezaji wake ukaonekane moja kwa moja kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameongelea suala la uimarishaji wa viwanda vidogo kwa maana ya SIDO lengo lake likiwa ni moja tu kubwa kuendelea kutoa ujuzi na taaluma mbalimbali kwa vijana ambao hawajafikia kiwango kikubwa cha elimu ili wawe na ujuzi ambao utawasaidia katika soko la ajira hasa tunapokuja kuzungumza habari tarajiwa ya viwanda vingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la viwanda vya SIDO au wazo la hivi viwanda vidogo vidogo lazima liwe na mipaka. Inawezekana sana tunakosea; leo unakwenda kule kwa kina Mzee Lubeleje kijijini kabisa kule au kwa kina Mzee Mwamoto kule nako unataka kuweka kiwanda cha SIDO watu wengine wamezoea shughuli tu za kulima wanataka walime tu. Kwa hiyo nimwombe sana tuangalie, tuwe na malengo. Inawezekana tukachukua manispaa, halmashauri za miji na majiji tukaimarisha shughuli za viwanda vidogo vya SIDO kwa kuanzia ili tuzalishe wataalam wengi zaidi na kuzalisha vifaa vingi zaidi ambavyo vitasaidia kuvipeleka ma mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie juu ya habari ya wazabuni. Mheshimiwa Waziri ni shahidi wamekusanya fedha nyingi sana na Serikali imefanya kazi kubwa sana. Wazabuni waliofanya kazi na taasisi za elimu, shule, hospitali na maeneo ya taasisi za Jeshi la Polisi na wananchi wanapata tabu sana ya malipo yao kwa muda mrefu sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaomba sana tujitahidi kwa namna yoyote ile tuhakikishe tunalipa madeni haya, kwa sababu kwa kuwalipa hawa tunaongeza mzunguko wa fedha. Naamini Mheshimiwa Waziri fedha tunazo nyingi sana za kutosha na baadaye nitamwambia kwa nini fedha hizi naamini anazo kwa sababu ya mambo makubwa ambayo Serikali hii imeyasimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kodi ya ardhi; Mheshimiwa Kishimba hapa amelizungumza na mimi niliseme kwa namna ya tofauti kidogo. Niwashukuru sana Wizara ya ardhi kwa kuamua kuanzisha urasimishaji wa makazi kwenye miji yote mikubwa. Maana yake ni nini, kodi tunayokusanya sasa naamini kodi ya ardhi haijafikia hata asilimia 30. Tukiweka mfumo mzuri majengo yote ambayo tunataka yapimwe yakapimwa sawasawa, naamini Serikali hii kupitia kodi ya majengo peke yake Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango anaweza akakusanya fedha nyingi sana na zikaendelea kutusaidia katika kutatua changamoto tulizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivi hatutakuwa leo tunahangaika kuwa na bajeti ambayo mwisho wa siku hatufikii malengo ya ukusanyaji wa fedha. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, naamini, leo kila mtu anashangaa kwa nini Serikali inafanya miradi mikubwa, lakini ukiangalia fedha peke yake tunayokusanya kwa mwezi mmoja na matumizi tulioyonayo hayalingani na kiasi tunachokusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mheshimiwa Mpango anasahau naye kwenye hotuba yake amemsifu sana Mheshimiwa Rais, lakini naona amemsifu kwa vitu vidogo vidogo sana. Nimkumbushe Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango, wakati najaribu kusoma kuangalia, miaka ya nyuma huko wakati sisi tuko nje tunatamani kuja kwenye Bunge hili tulikuwa tunaona Bunge likisimamia na kulalamikia mambo makubwa. Leo tumekuja humu mambo haya yote yamefanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango hajatuambia kwa mfano wako Wabunge humu mwaka 2012/2013 alikuwa Mheshimiwa Mpina, Mheshimiwa Ndugulile na wengine wengi walifika hatua ya kugomea bajeti hii kama hii tunayoijadili leo wakitaka mambo ya msingi ambayo Serikali iilkuwa inashindwa kuyasimamia wakiamini yangeweza kuleta mapato mengi kwenye Serikali lakini yalishindikana. Leo Mheshimiwa Dkt. Mpango tunazungumza hapa, nimpe mfano wa mambo matatu tu kwa haraka haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi si Mhasibu lakini nilikuwa nasoma naona, wanazungumzia habari ya illicit financial flows; yeye anafahamu kwa kiasi gani Serikali ya Awamu ya Tano imezuia masuala yote yanayotokana na mfumo huu. Haya ni pamoja na mikataba ya kampuni nyingi ambapo mikataba ya kampuni zinazoshughulika na rasilimali za Taifa zilikuwa zinasimamiwa na zilikuwa zimeachwa wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango ni shahidi, hapa wamesimamia masuala ya mikataba, masuala ya usafirishaji wa mizigo. Kwa mfano mdogo alikuwa akija hapa tunasikia tunauza nguzo nje ya nchi, lakini zinauzwa hapa nchini zinapelekwa Kenya au south Africa halafu zinarudishwa hapa zinanunuliwa kwa gharama kubwa zaidi. Hili limekoma na limekwisha, leo ni kiasi gani cha fedha kimeokolewa hapa? Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri kuna kitu kinaitwa dollarization, matumizi ya dola nchini. Mtu alikuwa anaweza kuja na begi zake za dola akaondoka na begi zake za dola hapa hakuna mtu anauliza. Leo kwa kiasi gani Serikali yake imefaidika na kuzuia utaratibu wa matumizi ya dola yasiyokuwa na mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge hili mwaka 1992 Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi kwa kiasi kikubwa sana leo nchi yetu haiko kwenye mfumo wa matumizi ya moja kwa moja kwa dola kama Zimbabwe na nchi zingine. Sisi dola ni matumizi ambayo si ya lazima, lakini sheria iliyoruhusu kufunguliwa account za dola na matumizi ya dola imeweka mipaka ambayo ilikuwa wazi, leo wamedhibiti maeneo hayo na fedha zinapatikana kwa wingi; hii ni sambasamba na transfer pricing.
Mhehimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mambo haya makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya yametuongezea fedha kiasi gani, yameiongezea Serikali nguvu ya kiasi gani, aje hapa awaambie Watanzania wajue mabadiliko ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tukisimama hapa tunaongelea Mheshimiwa Magufuli kafanya mambo makubwa watu hawatuelewi na ndiyo maana wanasema msisifie tu. Yako mazingira yanatulazimisha tusifie na Mheshimiwa Waziri anapokuja atuambie kwa kiasi gani Serikali imeokoa fedha nyingi kwenye maeneo hayo matatu na ambayo leo tunazungumza Serikali hii tunaweza kuwa na miradi mikubwa ambayo inafikirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye kila halmashauri tunazungumzia kujenga vituo vya afya, hospitali za Wilaya 60, tunazungumzia kujenga vituo vya afya kila kata, fedha zinatoka wapi? Tulizonazo ukipiga hesabu hazitoshi, lakini kwa sababu kuna mifumo wamesimamia, wamezuia fedha nyingi zaidi zimepatikana, ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano ina fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie jambo moja dogo sana, tunazungumza habari ya mjadala hapa namna gani Serikali inataka kuanzisha Mfuko mmoja (Treasury Single Account); wala si jambo jipya. Tukifuatilia kwenye hotuba na mijadala ya Bunge la mwaka 2014 suala hili limepitishwa na maazimio ya Bunge hili bada ya umoja wa nchi za Afrika Mashariki na Kati kuamua kuwa na mfumo huo. Sasa leo hapa tunataka kulifanya kama jambo jipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ukichukulia kwenye halmashauri zetu, mwaka mzima uliopita leo kati ya halmashauri 151 tulikuwa na zaidi ya account 1,500, leo tuna account zisizopungua chache 150 na kitu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nilikuwa kwenye pick sasa, naunga mkono hoja kidumu Chama cha Mapinduzi. Ahsante sana.