Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie bajeti hii Kuu ya Serikali kwa mwaka huu 2018/2019. Nitangulie kwa kuunga mkono hoja, lakini pia nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mawaziri, Waziri wa Fedha na Naibu wake, kwa hotuba yao nzuri, yenye nia njema kwa nchi hii na kuifanya nchi hii ijitegemee kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia juhudi kubwa za Serikali katika kujitegemea katika umeme kwa kujenga sasa Stiegler’s Gorge. Vile vile nipongeze juhudi za Serikali za kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mawazo yangu kidogo ya kuishauri Serikali, kwamba sasa ione sekta ya kilimo inaweza ikawa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi hii, lakini ni sekta iliyoajiri zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania lakini haija-reflect vizuri katika bajeti hii ni namna gani tunawabeba wakulima wetu ambao baadaye tunatarajia kwamba sasa sekta hii iendelee kuajiri hata wasomi ambao wanatoka katika vyuo vikuu ambao ajira katika sekta iliyo rasmi imekuwa hamna kama inavyoonekana. Sasa nia yangu ni kuishauri Serikali tuone namna gani sasa tutawezesha kilimo hiki. Tukiendelea kutegemea kilimo hiki cha mvua bado hatutaweza kufika popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa Serikali ikatoa mwelekeo wa namna gani tutaweza kuwa na kilimo cha umwagiliaji maeneo mengi, ni namna gani tutawezesha miundombinu ya kufanya kilimo cha umwagiliaji kiwezekane hususani katika mikoa kame Mikoa ya Kanda ya kati ya Dodoma na Singida. Katika mpango wake kuna bwawa hili la hapa Farkwa ambalo kama litajengwa kwa wakati lina msaada mkubwa sana kwa wakulima wa Kanda ya Kati, Skimu za umwagiliaji ambayo ipo ya Bahi na maeneo mengine ya mkoa wa Singida yatanufaika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali ione ni namna bora ya kufanya sasa hata deep well za kutosha ambazo zitafanya maeneo mengi ya umwagiliaji. Tukitegemea kilimo hiki cha mvua ambacho tumekizoea mwaka ambao mvua itakuwa kidogo itakuwa ni namna ngumu sana ya kujitegemea hata kwa chakula ambacho kwa miaka hii mingi sasa tumeanza kujitegemea. Ni vizuri sasa Serikali ikawekeza pahali hapo ili wananchi wetu na nchi kwa ujumla iweze kunufaika. Hata hivyo, niipongeze Serikali kwa kutenge pesa kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima hususani mahindi ya kupitia NFRA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sekta pia ambayo imesahauliwa. Sekta ya misitu ilikuwa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi hii lakini hapa katikati kumeyumba, tumekuwa tunagemea export za species chache sana kama mitiki, lakini wakati huo wanunuzi wa tiki na wachakataji wa tiki wamekuwa na usumbufu lakini bei za mazao yale katika mashamba ya Serikali zimekuwa ni kubwa zaidi kuliko hata bei za masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uwezo sasa kuiambia Serikali ifanye machakato wa kutosha kuona specie nyingine ambazo ziko kwa wingi katika nchi yetu. Na-declare interest mimi ni mdau katika sekta hiyo, zinaweza kutuondoa katika changamoto hii ya maduhuli ya Serikali kwa kiwango kikubwa sana. Miaka 2011, 2012 hadi 2013 ukiangalia katika mchakato mzima wa export ya nchi hii sekta ya misitu ilikuwa na mchango mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea hapa katikati kumekuwa na ban za ajabu ajabu, zinafika mahali wananchi wajasiriamali na wenye viwanda sasa wanakosa malighafi katika viwanda ambavyo Serikali iliwashauri wananchi watoke kule ambako walikuwa wana export mazao ghafi. Sasa wamewekeza kwenye viwanda sasa hivi tena viwanda vile vile vimekosa malighafi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya misitu kama itasimamiwa vizuri itakuwa na mchango mkubwa sana kama zilivyo sekta za utalii na wanyamapori katika uwindaji wa kitalii; lakini sekta hii ya misitu nayo naamini kwa weledi ambao kama watasimama vizuri Wizara ya Maliasili wataisaidia Serikali kama Wizara ambayo ina mchango mkubwa kwenye kukusanya maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu na kuunganisha mikoa ya nchi hii kwa kiwango cha lami bado ni changamoto. Suala la Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya limekuwa likizungumziwa kwa muda mrefu. Wabunge wote wa miaka mingi ya nyuma, hata mwaka juzi mimi nilisimama na ilani hapa kuonesha, mwaka jana wakaonesha nia ya kutaka kujenga Barabara ya Mkiwa hadi Rungwa, kilomita angalau 56.9, ikawekwa kwenye bajeti ikatangazwa kazi mkandarasi akapatikana na Mheshimiwa Rais akaja pale akazungumza na wananchi akaonesha dhamira yake ya kujenga barabara lakini mchakato ule ukafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi hivi tunavyozungumza tumeona tu katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2018/ 2019 barabara hii imeonesha ukurasa wa 49 kilomita 56.9, lakini mpaka hivi wananchi wale wa jimbo ambalo mimi ni mwakilishi wao hawajui barabara hii itaanza kujengwa lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Serikali ioneshe dhamira ya kweli ya kuunganisha mikoa kwa njia ya lami, ndiyo itakayofanya wananchi wakimbie. Walipa kodi wa maeneo ya pembezoni watalipa kodi kwa sababu watakuwa wanafanya biashara zenye tija kwa kufuata biashara maeneo makubwa. Leo mji wa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi Dodoma imetangazwa kuwa jiji mikoa ya jirani kama mikoa na majimbo ambayo mimi natoka yatakuwa na manufaa sana kama yataunganishwa kwa kiwango cha lami na mikoa jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia niiombe Serikali iendelee kutia mkazo barabara hii ya kutoka Handeni, Kiberashi, Kijungu, Kibaya, Njoro, Olboroti, Mrijo Chini, Dalai Bicha, Chambalo, Chemba kwa Mtoro hadi Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuchumi barabara hii ina manufaa makubwa sana, ni njia ya mkato kabisa ya watu watakaokwenda Bandari ya Tanga; na tuna matarajio yetu kwamba tunajenga bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani Tanga. Kwa maana hiyo barabara hii kama itajengwa kwa kiwango cha lami itasaidia sana hata nchi jirani ya Rwanda, Uganda, Burundi kama watatumia Bandari ya Tanga kuondoa msongamano katika bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafsi na pia naomba niunge mkono hoja hii ya Waziri wa Fedha.