Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. PETER D. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pia nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama kuchangia kidogo hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema mambo matatu, lakini kabla sijasema naomba nimshauri kaka yangu Isdori kwamba msalaba aliopewa amepewa na Yesu mwenyewe, kwa hiyo amtegemee Yesu; yeye alisema njooni kwangu ninyi nyote mnaosumbuka na mizigo nami nitawapumzisha, lakini Yesu mwenyewe alipata msalaba mkubwa na alipokwenda Gethsemane alimwomba Mungu akasema nipishie huu msalaba lakini kwa mapenzi yako; na wewe umepewa msalaba huo na Yesu kwa kupitia kwa Mheshimiwa Rais, hebu asinung’unike, afanye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nichangie kwa kusema, bajeti ya Mheshimiwa Waziri imeonesha matumaini kidogo safari hii. Kwa sababu ameanza kusikiliza ushauri wa Bunge. Tangu Awamu ya Tano imeanza Bunge limekuwa likishauri mambo mengi; nitatoa mifano miwili tu kuonesha jambo jinsi ambavyo bajeti hii imefanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri ambao Bunge limekuwa likisema ni kuwasaidia wawekezaji waweze kujisikia wako nyumbani, kuweka mazingira bora ya uwekezaji; na nashukuru ukisoma kwenye kitabu chake utaona wameunda mpaka blue print maana yake wamewasilikiliza na wanazungumza nao kila baada ya miezi kadhaa. Kwa kweli tunaomba hii blue print basi mtuletee tuisoma na muitekeleze ili mazingira ya uwekezaji katika nchi yetu yaweze kuboreka na kweli uwekezaji uje katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni mfano ni kuhusu kodi. Mara nyingi tumekuwa tukisema kwamba kodi na tozo zitazamwe na hasa kenye kilimo. Nimeona kuna baadhi ya kurasa hapa, kwa mfano ukurasa wa 46 amepunguza corporate tax kutoka 30 mpaka 20 kwenye mazao ya ngozi, jambo hili litachochea sana ukuaji wa sekta ya ngozi. Naomba basi Mheshimiwa Waziri pamoja na hilo basi apeleke na kwenye mazao mengine ya kilimo, uvuvi na ufugaji ili tuchochee shughuli za uanzishwaji wa viwanda katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilitekelezwa mwaka jana ilikuwa ni VAT ilyokuwa imewekwa kwenye huduma za mizigo inayopita. Nakumbuka mimi nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati tulilisema na Serikali ikalisikia. Kwa kweli bajeti hii ya leo inaleta matumaini makubwa sana. Ipo mifano mingi sana ambayo ningeweza kusema lakini itoshe tu kuonesha kwamba bajeti inaleta mwelekeo wa kukuza viwanda katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nitoe ushauri, kwamba pamoja na mwelekeo huo bado kuna mambo makubwa ambayo Wabunge wengi wameyasenma na mimi nataka niseme mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ili tuweze kujenga uchumi wa viwanda ni lazima bajeti ya kilimo, Waheshimiwa Wabunge wamesema, iongezwe. Kwenye ukurasa wa 80 amesema ni kipaumbele cha Serikali lakini bajeti ni ndogo asilimia sijui ngapi. Tafadhali Mheshimiwa Waziri hebu ajaribu kuongeza hiyo bajeti, bajeti ijayo kilimo tusikie kwamba kweli tumepewa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kujenga uchumi wa viwanda pia linahusiana na ile miradi ya kielelezo waliyoiweka; mmoja ukiwa ni mradi wa Makaa ya Mawe na mradi wa Chuma Liganga. Chuma tukiweza kukipata ni dhahiri kabisa tutaweza kuendeleza miradi mingi, hata mradi wa Stiegler’s Gorge, mradi wa kujenga Reli, tutatumia chuma chetu, tutapunguza gharama kweli. Sasa tunauacha tu huu mradi unaendelea, kila siku, kila mwaka tunausema; na kwenye bajeti yako hapa hauoneshi. Kwenye bajeti ya Mheshimiwa Mwijage haukupewa kipaumbele cha kutosha. Najua matatizo yake ni vivutio vya kodi, hebu wamalize hilo jambo; kuna matatizo ya fidia ya wananchi wamalize hilo, lakini pia PPA kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kusema kwa kifupi ni kuhusu ETS. ETS ni mfumo mzuri, kwa maana ya kuhesabu uzalishaji na hakuna mtu anae pinga humu kwamba huu mfumo ni mzuri kwa sababu tutaweza kupata kodi halisia. Hata hivyo, changamoto zilizopo zilizoelezwa na wadau ni lazima Serikali wazisikilize, wanapotekeleza wasikilize gharama ya uwekezaji kwenye mradi huo. Pia waangalie namna ambavyo wataweza kufanya kiasi kwamba wawekezaji hawa waweze kuwa na gharama ndogo ili wananchi wasiweze kupata kodi kubwa kwenye vinywaji vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kutoka mwisho ni Akaunti Jumuifu (TSA), ni jambo zuri kwa maana ya kuweza ku-control liquidity ya fedha katika nchi. Hata hivyo, kuna changamoto kubwa, kwa sababu ukitekeleza utalazimika ukaangalie na sheria nyingine, unaweza ukaangalia hata Katiba ya nchi yetu tunatawalaje, kwa sababu hii inaonesha kwamba inaweza kwenda kuua Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa kwenye Kamati ya Bajeti kule niliwaambia nchi ya Marekani ina states 50 na kila state ina Bunge na ina bajeti na wimbo wake wa Taifa. Sasa zile fedha kweli zinapelekwa kwenye Mfuko Mkuu ili zirudishwe kwenye states? Nikasema inawezekana kabisa reporting information ya matumizi lakini si hela ziende na kurudi. Kwa hiyo tunapotekeleza ni lazima tufikirie kurekebisha na sheria nyingine. Kwa hiyo ni jambo kubwa ambalo linahitaji Serikali watazame vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni hili ambalo wenzangu wamesema; mimi nimetoka kwenye sekta ya madini; jambo la dhahabu. Dhahabu ni fedha na ukiangalia sheria ya BOT inasema inatunza fedha za kigeni lakini inatunza dhahabu safi. Niliwahi kusema nchi zote tajiri zina tani nyingi kweli za dhahabu kwenye central Banks zake, kwa mfano Marekani inatani zaidi ya elfu nane imetunza kwenye Central Bank. Uchina elfu moja mia saba, Ujerumani elfu tatu mia tano, Italy elfu mbili mia tano, Ufaransa elfu mbili mia nne; zote hizi zinaipa nchi ile nguvu ya kuwa tajiri. Sisi tuna dhahabu kwa nini tusitunze dhahabu?...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.