Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii ili kutoa mchango wangu katika hoja iliyo mezani kwetu. Kwenye kitabu cha Mpango Hotuba ukurasa wa 15, mpaka 16, Mheshimiwa Waziri ameonesha changamoto tulizonazo ambazo zinatuletea mkwamo katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizo zilizotajwa, zipo tano, na tatu kati ya hizo, ameonesha kwamba ni ukosefu wa fursa za ajira, changamoto katika sekta ya kilimo, akisema kuna uwekezaji mdogo, tija ndogo, kutegemea mvua, sambamba na mchango mdogo wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa. Pia kuwepo kwa wigo mdogo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambao uwiano wa mapato ya ndani na Pato la Taifa ni takribani asilimia kumi na tano tu, ikilinganishwa na wastani asilimia kumi na saba.

Mheshimiwa Spika, niliposoma hivi, hizi kurasa za kwanza, nilitegemea kwamba huko mbeleni kurasa zinazofuata basi ni kuzigeuza hizi changamoto, kuwa opportunities (fursa). Sasa tukienda ukurasa zinazofuatia wanasema fursa, zipo, anakiri kwamba kuna nguvu kazi kubwa katika Taifa; halafu vikaishia hapo akaenda kuanza kuelezea mafanikio.

Mheshimiwa Spika, nilisikitika baada ya kuona hivi, kwamba ahaa kumbe tunajua shida yetu ni nini, kwa hiyo kwa nini hizi changamoto zisiwe reflected kwenye mipango yetu tunayojiwekea? Kwa nini changamoto hizi zisiwe reflected kwenye bajeti ambayo tutaitenga? Ukiangalia mipango tuliyonayo linganifu na bajeti tunayoitenga haviendani. Mpango wetu wa Miaka Mitano wa Taifa na mpango wa mwaka mmoja mmoja kwa kila mwaka wa fedha na bajeti tunazozitenga katika huo mwaka husika ni vitu vitatu tofauti. Hotuba ya mpango, hotuba ya bajeti, kitabu cha mpango, mapendekezo ya mpango havina uhusiano, ni kama vile vimeandikwa na taasisi tatu tofauti.

Mheshimiwa Spika, pia kuna mkinzano mkubwa sana kati ya sera na vipaumbele vyetu. Tunasema tuna Sera ya Serikali yetu ya Tanzania ni ya Viwanda. Viwanda hivyo haviwi reflected kwenye mipango strategy ni viwanda vya aina gani, sources za raw materials za hivyo viwanda ni vipi? Mheshimiwa usitingishe kichwa, kila kitu kimeandikwa kwenye vitabu, sijavitoa hewani. Ukiangalia pia na kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa letu, vivyo hivyo haiwi reflected japo inaonesha kwamba Kilimo kina contribute zaidi, nikisema kilimo, ni kilimo chenyewe, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu; tunasema ina- contribute asilimia thelathini, kinachofuata ni asilimia kumi na tano kutoka sekta ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Sasa tunatokaje hapa kwa sababu tuna maandishi ya tofauti tofauti? Nikawa nawaza shida ni watendaji, shida ni matamko ya kisiasa au kuna kitu cha ziada? Mfano tu wa haraka haraka labda kuna sintofahamu ya wafanyakazi katika Wizara husika inayohusiana na mambo yetu ya bajeti na mipango. Aidha, wafanyakazi hatuna motivation au kuna hidden agenda ambayo siielewi, kwa sababu kila kitu kiko wazi na Waziri mwenyewe amesema changamoto ni zipi zinazotukwamisha tusiende lakini hakuna solution, tunaruka hapa na pale.

Mheshimiwa Spika, katika kitabu chetu cha Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano ilisemwa kwamba tutahitaji takriban trilioni mia moja na saba kwenye shughuli za maendeleo ili tuvuke, ikimaanisha kwamba Serikali yenyewe itakuwa inatoa trilioni 11.8 takribani na sekta binafsi zitachangia trilioni 9.6, jumla trilioni 21 kwa ajili ya shughuli za maendeleo ili tuweze kuvuka.

Mheshimiwa Spika, lakini bajeti hii inayoishia na bajeti inayokuja tumetenga tuu trilioni 11 na kwa ajili ya shughuli za maendeleo na ni contribution ndogo sana kutoka katika Sekta binafsi. Mwaka huu unaoishia kati ya trilioni kumi na moja tuliweza kutoa trilioni 5.12 tu. Kati ya fedha hizo za maendeleo, kilichotolewa katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni asilimia 34. Tunaenda kujenga reli, kununua ndege na kadhalika, trilioni 1.7 zilitoka. Hizo zilizobaki sasa trilioni 2.43 ndizo zilienda kwenye sekta nyingine zilizobaki katika wizara nyingine. Cha kushangaza, katika hizo trilioni mbili zilizobaki, mifugo na uvuvi, hawakupata hata senti tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia sasa hiyo sekta ambayo ndio wananchi wengi tunasema wapo humo, according to statistics za nchi inasema inaajiri asilimia 66 lakini ninahisi ni zaidi ya hiyo asilimia 66.3 ya kaya zote nchini, ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu.

Mheshimiwa Spika, tunasema kwamba kilimo huchangia kwa ujumla wake, asilimia 20 ya mauzo ya nje na kinakua kwa pace ndogo sana, haishangazi kwa ni nini kwa sababu hatujawekeza katika hii sekta. Mifano tu dhahiri ya nchi za wenzetu, mfano nchi ya Brazili, wenyewe wametoka, ni nchi ya nane kwa uchumi mzuri duniani. Hata hivyo walitokaje? Wali-invest kwenye kilimo hususan kilimo cha kahawa. Wali-invest kwenye kilimo cha kahawa na waka- invest kwenye viwanda ambavyo vinashughulika na shughuli za kahawa, ikainua sekta nyingine baada ya kufanikisha kilimo.

Mheshimiwa Spika, sasa leo hii Tanzania labda tuna shida ya kuwa na rasilimali nyingi mno ambazo zinatakiwa zijenge uchumi, kwa hiyo hatujui Tanzania inasimamia wapi. Tanzania uchumi wake unaendeshwa na nini, tukimwuliiza leo Waziri wa Fedha, Tanzania inaendeshwa na nini? Is it kilimo, kilimo chenyewe ambacho hatuja-invest? Ni utalii, madini au ni kitu gani? Leo hii ukiwafundisha watoto wa shule Tanzania inajivunia kwenye nini katika kuendeleza uchumi wake hatuwezi kusema.

Mheshimiwa Spika, kama sekta hiyo sasa, ambayo tunasema ndiyo inayoajiri watu wengi zaidi, yaani wananchi ndiyo wanayotegemea hii sekta imenyamaziwa kimya, mifugo na uvuvi imenyamaziwa kimya. Sana sana sasa hivi tuna sintofahamu ya jinsi ya kutoka kwa kudhibiti uvuvi haramu tena kwa kutumia njia ambazo si sahihi, za kuzidi ku-frastrate hawa wananchi wachache.

Mheshimiwa Spika, mfano tu, sawa tumewanyima fedha za kufanya shughuli za maendeleo, lakini sekta hizi; si kilimo, si uvuvi, si kwenye sekta ya mifugo, kuna upungufu wa zile asilimia 50 ya wale maofisa wanaotakiwa wawaguse wananchi na kuwashika mkono kuinuka hapo walipo. Kwa mfano, Maafisa Ugani ambao ni muhimu sana waliopo ni elfu saba na kati ya vijiji elfu kumi na tano na, wakati kila kijiji kilitakiwa kiwe na Afisa Ugani mmoja.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa tunatokaje tokaje? Hatuwezi kutoka tutakuwa kila siku uchumi uko mdogo, kila siku tunaletewa makablasha na maandishi ambayo hayaendi kufanya kazi. Sasa unajiuliza ni kwa nini, wakati kila kitu kiko obvious na tunaweza tukatoka hapa? Nia ya Serikali ni nini?

Mheshimiwa Spika, katika kutuchanganya pia sasa Serikali kwa hiyo hela kidogo iliyonayo na hatuoni mkakati dhahiri wa kulea hizi sekta ambazo zinaweza zikatutoa, sasa wanakuja na proposal ya kuweka fedha zote za Taifa hili katika Mfuko mmoja ilhali kuna mifano mingi ambayo inawakwaza Wananchi. TRA wanasema wanakusanya mapato lakini literally wanakuwa wanashikia wa sekta binafsi fedha zao. TRA inadaiwa bilioni thelathini na sita kutoka katika sekta ya sukari, hii sukari ya viwandani, ile asilimia 15, wamegoma kurejesha. TRA hawa hawa wanadaiwa na Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund) bilioni 14.8. TRA hao hao wanadaiwa na REA.

Mheshimiwa Spika, apart from hayo madai wanayodaiwa ambayo hela sio zao nao wanazi-claim kama mapato na kudanganya Bunge lako kwamba in totality uchumi unakua, uchumi haukui, hizi ni hela za watu, Bodi ya Korosho wanadai bilioni themanini na moja, lakini in totality mwaka wa Fedha uliopita na huu wanawadai milioni mia mbili na, lakini wanaziweka kwenye Mfuko Mkuu na kusema kwamba mapato yameongezeka, lakini si mapato hizi ni hela walizokopa kwa watu wa Sekta tofauti tofauti.

Mheshimiwa Spika, kuna issue pia ya ucheleweshaji wa malipo ya watoa huduma, kama ni wakandarasi, na kadhalika. Mfano, TANROADS na TBA nchini wamekuwa wana-delays za kulipa wakandarasi na watoa huduma mbalimbali. Kwa mwaka huu wa fedha unaoisha TANROADS na TRA wanadaiwa jumla bilioni mia tano themanini na saba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mwenendo huu, kuna mchezo sasa hivi wa Serikali kupora mapato ya wengine kwa kusema kwamba tunawawekezea lakini hawayarejeshi, kuna mtindo wa kuchelewesha au kutokupeleka kabisa kwa wale wanaowadai Serikali. Sasa inasikitisha kwamba na changamoto zote hizi Serikali bado sasa inataka kurudi kwenye Centralization System na kuacha Decentralization ili tu kuficha ile aibu kwamba tuna shida ya fedha katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii haiwezi kututoa hapa kama hatuwezi kuleta mikakati mahsusi ya kututoa hapa zaidi ya wao Serikali, kung’ang’ania mapato ambayo si yao ili kuficha tuu aibu kwamba tuna shida katika uchumi wetu. Naomba kama Serikali kama inataka kurudi kwenye Centralization System waache D by D, walete sheria hapa Bungeni ili tuweze kuja na mkakati wa kusema kwamba tumeshindwa huku tunataka kurudi huku kuliko kutuchanganya wananchi na Bunge lako kujua kwamba direction ya Serikali hii inaendajeendaje.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.