Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mapendekezo ya bajeti mwaka wa fedha wa 2018/2019. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Serikali kwa ujumla, tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais katika Wilaya ya Karagwe, tunashukuru sana kwa bilioni 70 ambazo Serikali ime-commit katika bajeti hii ya 2018/2019 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Rwakajunju, mradi ambao wananchi wa Karagwe wameusubiri miaka mingi sana, kwa hiyo tunamshukuru sana Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali kwa kutusaidia kupata Kituo cha Afya cha kisasa pale Kayanga na nashukuru Serikali kwa commitment ya kujenga kituo cha afya kingine katika Kata ya Nyaishozi, Kituo cha Afya cha Nyakayanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Watalaam wa Wizara kwa kutuletea mapendekezo ya bajeti ambayo kusema ukweli ni improvement ya bajeti zilizopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zipo na ndio maana tumekaa kama Bunge kuchambua mapendekezo haya na kuboresha na ni matumaini yangu kwamba, Mheshimiwa Waziri Mpango kwa kuanza mapendekezo ya Kamati ya Bajeti ni mazuri sana tunawapongeza sana Kamati ya Bajeti kwa mapendekezo mazuri. Kwa hiyo, naamini sana Mheshimiwa Dkt. Mpango akichukulia mapendekezo ya Kamati ya Bajeti kama msingi akaongezea na haya ambayo tunashauri, naamini kabisa tutapitisha bajeti ambayo ina weledi mkubwa kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimimwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nina machache ya kuchangia. Nianze kwa kusisitiza sana Serikali, hii ni bajeti ya fiscal year ya nne tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani. Tumekuwa tukilia sana kuhusu suala la stahiki za Walimu. Kuna Walimu wamemaliza toka mwaka 2015 mpaka sasa hivi hawajapata ajira na hawajapata ajira si kwamba shule zetu hayahitaji Walimu, kuna upungufu mkubwa wa Walimu katika mashule yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha akae na wenzake katika Serikali waliangalie hili kwa umuhimu wake na kwa manufaa ya watoto wetu ambao ni kizazi cha ni Taifa la kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Walimu ambao walipandishwa madaraja toka mwaka 2012, lakini mpaka sasa hivi mishahara yao haijarekebishwa ku-reflect yale madaraja ambayo wamepanda. Kwa hiyo, kiujumla changamoto ya upungufu wa watumishi ipo hata upungufu wa Wauguzi katika vituo vyetu vya tiba. Serikali wanafanya kazi nzuri ya kuweka miundombinu ya vituo vya afya, hospitali na zahanati, lakini itakuwa haina maana kama tunakuwa tuna majengo mazuri lakini hayana Wauguzi kwa ajili ya kuhudumia Watanzania. Kwa hiyo, hili naomba pia naomba waliweke katika vipaumbele vya mwaka huu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuchangia ni hili suala zima la takwimu ambazo Mheshimiwa Waziri kila mwaka wa fedha akisoma wastani wa kipato cha Mtanzania na uhalisia wa mtaani unaona kuna ukakasi. Sishangai na nitasema kwa nini. Ukiangalia mapendekezo ya bajeti hii ya 2018/2019, Serikali imefanya kazi nzuri katika kuhakikisha upande wa yule mpokea malighafi kwa maana ya msindikaji au manufacturing wameweka unafuu mkubwa sana na ndio maana tunapendekeza bajeti hii ni mwanzo mzuri wa kusaidia nchi kwenda kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda, kwa hiyo ni hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwaombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yao, waangalie hii 67% ya Watanzania ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi na hawa Machinga na Mamalishe hiyo ndio component kubwa. Kwa hiyo, unafuu wakiukita kwenye hiyo asilimia 67 ya Watanzania ile tunayoita source economic transformation tutaiona kwa haraka sana, lakini tukiendelea hivi hii asilimia
33 ambayo sana sana ambayo ni trade sector, manufacturing na service sector, sawa na yenyewe ni component muhimu, lakini, component hizi mbili kwa upande mmoja mkulima, mfugaji, mvuvi na mfanyabiashara mdogo mdogo machinga, mamalishe tukiweza kuwa-align vizuri na ile component ya ambayo ina receive kile kinachotengeneza yaani malighafi kwenda kwenye manufacturing sector tutakuwa tumefanikiwa kama nchi na tutainua Watanzania kutoka kwenye umasikini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza kwa sababu wameshaandaa kama ilivyo sasa hivi na improvement itakuwa ni incremental, sasa nishauri angalau mwaka huu wa fedha waangalie yale mazao matano tuliyoyafanya kipaumbele, waangalie namna gani tutamsaidia mkulima wa haya mazao matano angalau hii disposable income yaani kuanzia tarehe Mosi Julai, mwezi unaokuja tutakapoanza kutekeleza hii bajeti aanze kuona impact ya moja kwa moja kwenye kipato chake cha mfukoni. Tukifanya hivyo wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anasoma bajeti ijayo wastani wa kipato cha kila Mtanzania hatapata ukakasi ambao anaupata sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie informal sector, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wamekuwa wakiizungumzia sana, lakini naona bado iko changamoto ya namna gani tunafanya kui-tap ili iweze kuwa sehemu ya formal sector. Sasa nimezungumzia changamoto za Machinga, Mamalishe, Wafanyabiashara wadogo wadogo hawa wote wapo kwenye hii informal sector. Hii ni potential ya kuongeza kwenye tax base ambayo bado iko null. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia jinsi Tanzania bado tuko chini ya viwango vya kimataifa, ukichukua ratio ya tax collection as percentage ya GDP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze ku- broaden tax lazima tufike mahali hii informal sector ikiwezekana ndani ya Serikali kuwe na chombo maalum cha kuihudumia ikiwezekana hata Wizara, kwa nini, kwa maana hii ni asilimia kubwa ya Watanzania. Ukienda kwenye miji, ukienda kwenye mitaa kule vijijini akimama wanafanya kazi kwenye jua kali, wana familia zao kupitia kwenye vipato hivi vidogo wanasomesha watoto, wanatibu familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini kama Serikali tusifike mahali angalau kila halmashauri kunakuwa na mkakati maalum wa kuhakikisha hawa akinamama wanaofanya biashara ndogo ndogo barabarani tunawawekea miundombinu na kupitia miundombinu hiyo sasa tunawaingiza kwenye formal sector hata Serikali itapata mapato lakini wanyonge hawa nao wataweza kujikwamua kutoka kwenye umaskini. Kwa hiyo, ifike mahali Serikali iangalie hii informal sector ikiwezekana kuundwe chombo maalum ikiwezekana hata Wizara kwa ajili ya kushughulika na changamoto zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie changamoto ambayo ipo kwenye zao la kahawa. Natoka Mkoa wa Kagera, tunazalisha kahawa kwa wingi na tunachangia asilimia kubwa sana katika uzalishaji wa kahawa hapa nchini. Tumesema hapa Bungeni kwamba, stakabadhi ghalani kuna potential kubwa ya kumsaidia mkulima wa kahawa kutoka kwenye umaskini, lakini matayarisho bado kuna walakini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, hivi sasa kule Kagera na maeneo mengine nchini msimu wa kahawa umeshaanza, lakini sasa hivi mwananchi akipeleka kahawa kwenye Vyama vya Msingi, kwenye risiti anaandikiwa kilo lakini haandikiwi bei ambayo ameuzia. Kwa hiyo, napenda kuomba Serikali huu mfumo wa stakabidhi ghalani walichukulie kama yai kwa sababu usipokwenda vizuri huko mbeleni kuna hatari kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wananchi wakulima wa Tanzania wanategemea mazao haya ya biashara katika kujikwamua katika umasikini. Kwa hiyo, zao la kahawa naomba waliangalie kwa umakini mno, waende vijijini waangalie changamoto za wakulima wa kahawa na Serikali waweze ku- intervene ili stakabadhi ghalani iweze kumsaidia mkulima wa kahawa kweli. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.