Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hoja hizi mbili ambazo ziko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu, kazi ni ngumu sana lakini wanaiweza, ni kazi ngumu kweli kweli. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kutoa hoja moja ambayo hailingani sana na hoja hii iliyo mbele yetu. Ziwa Rukwa miaka ya 60 na 70 mpaka 80 mwanzoni ilikuwa inatoa samaki wengi sana aina ya tilapia ambayo inaitwa ngege, walikuwa maarufu sana kwa Nyanda za Juu Kusini mpaka Zambia tulikuwa tunakula samaki hao. Miaka hii sasa hivi hao samaki hawapo, tumebaki tudogo hata huu mkono hauenei. Hata Serikali ikisimamisha uvunaji, miezi mitatu, miezi sita samaki havikui vinabaki pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hofu, kwamba kwa sababu katika Wilaya ya Chunya ambako ndio Mto Rupa unatokea ambao unaingia kwenye Ziwa Rukwa kuna uchimbaji mkubwa sana ambapo hapo zamani walikuwa wanatumia zebaki kusafisha madini ya dhahabu, nina wasiwasi kwamba samaki hawa wamekuwa contaminated na zebaki ndio maana havikui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ifanye utafiti haraka, ifanye utafiti tujue kama ni zebaki ipo basi tujue tiba ni nini tusije tukaharibu afya za watu. Kama imeshindikana basi Serikali ifanye mpango wa kupandikiza samaki wengine katika ziwa Rukwa ili tuendelee kuvuna kama tulivyokuwa tunavuna zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili naliunganisha na hoja ya kodi, tax measures ambazo Mheshimiwa Waziri ameweka mojawapo. Mheshimiwa Peter Serukamba juzi akichangia alidadavua sana kitaalam akiipongeza Serikali kwa kuanzisha electronic tax stamps, alidadavua kitaalam. Mimi nataka niiseme ki-layman, Watanzania tumekuwa tunanyweshwa mapombe makali, magongo kwa miaka mingi sana kwa sababu ya tax stamps ambazo zinaweza kuigwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifika mahali hapa Tanzania ilikuwa nusu ya consumption ya konyagi hapa nchini nusu ni original na nusu ni fake. Sasa ukinywesha population ya Watanzania gongo kwa muda wa miaka minne, mitano utapata watu wa ajabu sana. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuweka hii electronic tax stamp ambayo haiwezi kuigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na faida zote ambazo watapata za ku-count real time kupata kodi kuongezeka kwa mara dufu, lakini hili la Watanzania kunyweshwa gongo mimi namsifu sana kwa hilo Mheshimiwa Waziri na siyo gongo tu kwa konyagi hata kwenye brand hata kwenye vitu vingine wanaiga tax stamps wananywesha Watanzania. Aliwahi kusema Mheshimiwa wa Jimbo fulani hapa kwenye jimbo lake watu wanaume walikuwa wanashindwa kuhudumia ndoa, wanakwenda nchi nyingine kwa sababu ya mambo kama haya. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa kutumia uchumi wa jiografia kuweza kukuza mapato ya economy ya nchi, kupanua bandari ya Dar es Salaam, kujenga bandari ya Bagamoyo, kupanua bandari ya Mtwara, kujenga SGR na kuirekebisha meter gauge. Kwa hiyo, tutakuwa na reli mbili kwa upande wa kaskazini standards gauge ambayo ina mita 1.067 na meter gauge ambayo ni mita moja kamili. Vilevile reli ya TAZARA ambayo yenyewe ni cap gauge yenyewe upana wake ni mita 1.067, tutakuwa na aina tatu za reli. Hizi za Kaskazini zitaungana za Kenya, Uganda lakini hii ya TAZARA itaungana na South Africa na Zambia na Nchi zote za SADC huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pamoja juhudi zote ambazo tunafanya za kujenga reli mpya na kukarabati ya zamani reli ya TAZARA tusiisahau katika uchumi wa jiografia. Yenyewe inahitaji tuiweke umeme ibaki hivyo hivyo ni cap gauge tuiwekee umeme ili tuweze kuweka ma-train ya kwenda kwa kasi. Vilevile Serikali inaponunua mabehewa sasa, mabehewa ya hii reli mpya ya standard gauge inunue mabehewa na vichwa ambavyo ni adjustable ili viweze kutumika katika reli zote tatu. Vitumike kwenye SGR, vitumike kwenye meter gage na vitumike reli ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba niisihi sana Serikali, imejenga uwanja wa ndege wa Songwe, ni jambo nzuri sana, inahudumia Southern Highlands yote pamoja Nchi za Kusini mwa Afrika jambo nzuri sana. Hata hivyo, huu uwanja wa ndege hauna ukuta wa usalama, jengo la abiria halijakamilika, taa za kuongoza ndege hazipo, ni kama Serikali imekula ng’ombe wote, lakini mkia imebakiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara mbili nimeruka na ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya tumeshindwa kutua tumerudi Dar es Salaam. Ni hasara sana kwa shirika la ndege lakini vile vile inamuumiza yule abiria sana kwenye mwili wake. Naomba sana Serikali ifanye juhudi zote ili kukamilisha kujenga ukuta wa usalama, waweke hizo taa za kuongozea ndege na wakamilishe ujenzi wa jengo la abiria ili uwanja wa ndege wa Songwe uendelee kuhudumia Southern Highlands kama ilivyopangwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea kwa kifupi inatosha, lakini naomba sana kusisitiza sana kwamba, napongeza sana hizi juhudi za Serikali za kuweka Electronic Tax Stamps ambazo zitakuza mapato ya Serikali mara dufu na zitapunguza wananchi kuweza kuathirika kwa kunywa gongo na product nyingine za ajabu ajabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.