Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuweza kunipatia nafasi jioni ya leo nami niweze kuchangia kidogo. Ninayo maneno machache sana ya kusema, lakini ni muhimu yakasemwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayofanya na Msaidizi wake Naibu Waziri, wanafanya kazi kubwa sana. Unajua suala la uchumi ni suala mtambuka na ni suala ambalo linahitaji umahiri wa hali ya juu. Kwa hiyo, ukisoma kitabu kimoja kimoja unaweza usipate mwelekezo vizuri, ndiyo maana inabidi usome nyaraka zote halafu ujue tunaelekea wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye suala zima la ukusanyaji wa mapato. Jambo la kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa kutoa tax amnesty kwa watu ambao wanadaiwa kodi, kwa kuondoa interest na penalty zote zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliposoma kwenye kitabu nikagundua kwamba kutakuwa na tatizo moja, wamesema kwamba ndani ya miezi sita hiyo amnesty ndiyo itaweza kutolewa. Ila nafikiri kwenye miezi sita, kutakuwa na mazungumzo (negotiation), kwa sababu wale wanaotaka kupata huo msamaha inabidi waende kwenye Ofisi za TRA wakazungumze nao, wakubaliane na watakuja kwa nyakati tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pesa kiasi cha shilingi bilioni 500 nafikiri inatarajiwa kukusanywa ndani ya mwaka mzima. Kwa sababu, kama mtu atakuja mwezi wa Nane wakazungumza naye na hawezi kulipa in lumpsum, atalipa kidogo kidogo, ina maana lazima atakwenda mpaka Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni muhimu kwa sababu baada ya miezi sita mamlaka husika itakapokwenda kwenye Kamati itakuja kuonekana kwamba hizi pesa hazijakusanywa, kumbe ni suala la administration. Kwa hiyo, suala hilo ni muhimu likaangaliwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la Revenue Forecasting. Nimeangalia hii schedule jinsi mapato yatakavyopatikana, Tax Revenue na Non Tax Revenue, lakini nikawa najiuliza swali moja. Mwaka 2015/2016 nafikiri TRA ndiyo walifikia ile target iliyokuwa imewekwa. Unaposema target, maana yake inakwenda in line na projected plan ambayo inakuwa imeandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zile data za kufanyia hizo revenue forecasting zikiwa haziko sahihi sana kwa maana ya sector wise ndizo zina-lead kwenye kufanya ile revunue forecasting ilete majibu ambayo siyo sahihi. Kwa hiyo, jambo hilo inabidi liangaliwe ili tuwe tunawapa malengo sahihi hasa wenzetu wa TRA kwamba waweze kukusanya kulingana na uchumi unavyoruhusu, kwamba uchumi unaruhusu kodi kiasi gani iweze kukusanywa? Kwa hiyo, ni jambo muhimu sana hilo likaangaliwa na wataalam wetu wakaweza kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la mawasiliano (telecommunication). Ukiangalia nchi za jirani, Sekta ya Mawasiliano ina mchango mkubwa sana wa kodi. Sasa hapa kwetu Tanzania sijui kuna tatizo gani kwa sababu bado mchango katika Sekta ya Kodi haujawa wa kutosheleza kwa maoni yangu. Kwa hiyo, nafikiri uko umuhimu wa kufanya utafiti wa kutosha kuona mapato yanavuja wapi, au kwa nini Sekta ya Mawasiliano haijatoa mchango wa kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hesabu ya haraka tu, ukiangalia idadi ya Watanzania walioko na wanaotumia simu; sasa mapato yanayopatikana watu hawatumii simu? Watu wanatumia simu, lakini nafikiri kuna namna ambayo inafanyika ambayo siyo sahihi aidha kwenye kutengeneza hesabu zao, zile expenses zinakuwa nyingi mpaka huko kwenye profit kunaathiri kwenye profit, lakini pia ku-capture data kwa ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la EFD, bajeti imesema kwamba watalipa 0%. Nikawa najiuliza swali, sasa hivi kuna suppliers ambao wana stock. Ile stock wanaifanya nini? Kwa sababu stock ilikuwa imelipiwa kodi. Sasa wanafanya nini ili kuweza ku-mitigate au kuweza kufanya kwamba kuwe na fair play kwamba, hawa watakaoingiza zero na hawa ambao walishaleta tunafanya jambo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, hatua kubwa imechukuliwa na TRA na Wizara kwa ujumla kuhakikisha watu wanatumia mashine za EFD na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amelisemea sana hili suala. Tumekwenda kwenye hii informal sector. Nashauri kama itawezekana, zitafutwe EFD, halafu itafutwe sample group ambapo watu watapewa EFD bure kwenye informal sector waweze kutumia hizo EFD na tuone impact yake itakuwa ni nini? Itakuwa kama ni motisha kuweza kuwafanya watu waone umuhimu wa kutumia EFD, lakini pia watajifunza kufanya mahesabu ya kuweka na kutoa (simple book keeping), litakuwa ni jambo zuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia suala la kodi zilizo kwenye malimbikizo (tax objection) na lenyewe ni suala muhimu sana ambalo Wizara na TRA kwa ujumla wanatakiwa wasimamie waone kwamba zile tax objection zinakuwa cleared. Kwa kutumia window hii ya tax amnest inaweza pia ikasaidia kupunguza zile objections. Kwa hiyo, lazima kuwe na massive campaign ya kuweza kuwaelewesha watu wakajua hili jambo kwa sababu, watakuwa wanarudi nyuma, wanajificha kwa sababu, hawajui faida yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri nilibahatika kufika SAS, South Africa kule, waliwahi kutoa tax amnest na watu walilipa na walikuwa treated fairly na ilikuwa ni siri yao na kodi ilipatikana. Kwa hiyo, ni jambo muhimu sana kuwe na massive campaign na iwekwe bajeti ya kutosha kwa sababu ndiyo uwekezaji wenyewe. Kwa hiyo, tusibanie pesa mahali tunakoweza kupata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye lile la non tax revenue tumeona BoT walitoa gawio, NBC na CRDB. Ninachotaka kusema hapa, mashirika yanayosimamiwa na TR sasa imefikia wakati mchango wake uweze kuonekana. Kama mchango wa mashirika hayo ukiweza kuonekana, ndipo tutarudi hata huku kuweza kufikiria kwamba tupunguze baadhi ya viwango vya kodi au tuondoe kodi ambazo ni kero. Natambua kwamba ukisoma bajeti iko very tight kwa sababu vyanzo ni vilevile na lazima uwe na normal flow. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukipunguza Pay As You Earn utaleta madhara makubwa sana kwenye revenue collection. Jambo hilo nalifahamu na ni muhimu tukalifahamu wote tuangalie huku kwa TR anatuletea nini? Pamoja na hivyo, TR naye awekeze zaidi sasa. Kwa sababu, pamoja na mashirika yaliyopo, lakini lazima tuongeze uwekezaji kule ili tuweze kupata pesa za kuweza ku-finance bajeti yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nampongeza Mheshimiwa Waziri. Mimi natoka Singida tunalima sana zao la alizeti. Dodoma wanalima alizeti; kwa ku-protect viwanda vya ndani kwa kupandisha kodi, mafuta yatokayo nje ina maana uzalishaji wa ndani utaongezeka. Tatizo kubwa lililopo ukienda hapo Kibaigwa, ukaenda mbele kidogo, ukarudi Singida ukaenda Shelui, utakuta mafuta mengi yako barabarani. Sasa tunafanya utaratibu upi wa kuweza kuwasaidia hao wakulima kwanza kulima wapate mbegu bora, lakini pia kuweza kuyakusanya hayo mafuta yawe katika kiwango kinachokubalika na yaingie kwenye masoko rasmi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, watu hawa wanategemea masoko ya watu wanaopita barabarani na wakati mwingine uratibu wake sasa hata kodi hawalipi pia, lakini tukiweza kutengeneza centres katika maeneo hayo; na ndio hao wafanyabiashara wadogo wadogo ambao tunawazungumza, wajasiriamali, nafikiri mafuta yale ni mengi sana na hata tunaweza tukaya-count. Nina hakika kabisa hatujui kiasi gani cha mafuta kinachozalishwa na wazalishaji wadogo wadogo. Kwa hiyo, jambo hilo ni muhimu likaangaliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yote yakifanyika kwa ukamilifu wake, nina imani kwamba ile 32 trillion ambayo tunatarajia kuweza kuipata this year, itaweza kupatikana. Pia, mamlaka zinazohusika, wafanyakazi wa TRA basi wafanye kazi kwa juhudi na weledi mkubwa. Tunajua wanafanya kazi kubwa, lakini basi wahakikishe kwamba pesa au kodi inayostahili kukusanywa inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda kusema haya maneno machache, nafikiri yatakuwa yamemsaidia Mheshimiwa Waziri. Nashukuru sana.