Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, nami napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa afya njema kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Fedha. Pili, napenda kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii nami niweze kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam ni kitovu cha biashara katika nchi yetu na wafanyabiashara wa Dar es Salaam wanachangia pato kubwa la Taifa, lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi sana. Moja ya changamoto ni utitiri wa kodi. Ili mfanyabiashara aanzishe biashara, kuna process nyingi anapitia. Lazima apate leseni na hupewi leseni mpaka ukakadiriwe mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiutaratibu ingefaa zaidi mtu kabla ya kufanya biashara kwanza apewe muda maalum halafu baadaye ndiyo wanamkadiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano Dar es Salaam, ukienda pale Mnazi Mmoja Anatoglo, unataka leseni unaambiwa kwanza nenda TRA pale Summit Tower Lumumba. Ukifika Lumumba wanakuuliza eneo la biashara liko wapi? Unaambiwa liko Kariakoo. Wanakadiria biashara kulingana na eneo na wala siyo biashara unayoifanya. Hii ndiyo inayopelekea wafanyabiashara wengi kufunga maduka yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaambiwa huko Kariakoo ni mkoa wa kodi shilingi milioni tatu. Mtu anakadiria akiwa ofisini; hajui biashara unauza shilingi ngapi na hujaanza kuweka hata display. Ni tatizo kubwa sana kwa wafanyabiashara na hii ndiyo inawafanya wafanyabiasha wengi kufunga biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia TRA sasa hivi imepata mwanya; usipotoa risiti kutokana na matatizo ya EFD sasa hivi, kitu cha Sh.5,000/= unaambiwa faini yake shilingi milioni tatu. Mwingine anashindwa sasa kulipa shilingi milioni tatu, mtu wa TRA anapata mwanya anakwambia sasa tuzungumze. Mnakosa mapato, mtu anapewa shilingi milioni moja yanaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri katika kuliendea hili, najua binadamu siyo malaika, anafanya makosa na makosa mengine yanatokana na hizi mashine; na mashine zenyewe inaelekea labda zina hitilafu. Wakati mwingine umetoa bidhaa unataka uandike risiti
unakuta mteja kaondoka, kumbe ameshawasiliana na TRA anakuja kukukamata anakwambia toa shilingi milioni tatu. Tuweke faini ambazo ni reasonable zinazolipika ili Serikali iweze kupata mapato yake kulikoni kuishia katika rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kikosi cha Zimamoto sasa hivi kimetokea kule Dar es Salaam, kinataka kila frame ya duka iweke Fire Extinguisher. Najiuliza sana Mheshimiwa, mfanyabiashara anafungua duka 12.00 asubuhi, anafunga saa 11.00 jioni. Short ya meme ikitokea usiku wa manane fire extinguisher iko ndani ya duka lake, itamsaidia nini kuzima moto kama siyo biashara? Mfano tu, tutoe sisi Wabunge wote, watu wa Zimamoto waje waseme kila Mbunge achukue fire extinguisher aweke chumbani kwake, kweli itawezekana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba utitiri huu wa kodi unapelekea wafanyabiashara kuonekana mwisho wa mwaka akipiga hesabu hapati faida, anafunga duka lake. Tuelekeze nguvu zetu katika kuwasaidia wafanyabiashara ambao huwa wanaleta ajira kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ambayo siyo rasmi hususan ya Machinga pia wanakwamisha wafanyabiashara kufunga maduka yao Kariakoo. Mfanyabiashara analipa kodi ya takakata na asipokutwa na dust been analipa faini shilingi 50,000/=. Nje, Machinga hana dust been na hajui takataka zake anatupa wapi, anauza bila risiti. Ile kauli mbiu ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti, ni kwa baadhi ya wafanyabiashara, lakini sio wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, sekta isiyo rasmi isajiliwe, watu waweze kulipa mapato na kila mtu kama ni haki wote wafanye biashara kwa haki na walipe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tendency ya watu watu wetu wa Tanzania wanaona biashara zinazouzwa barabarani ni rahisi kuliko za madukani. Kwa hiyo, wafanyabiasha wanakwazika, hawapati faida katika maduka yao, mwisho wa mwaka umemkadiria mapato makubwa, hajui atalipaje, ndiyo maana maduka yanafungwa. Kwa hiyo, naomba irekebishwe, mtu apewe grace period at least miezi mitatu kisha ndiyo wanamkadiria. Mapato, maana yake amepata. Mtu hajaanza kuweka bidhaa unamkadiria mapato, ameuza nini? (Makofi)
Waheshimiwa kuna kodi nyingine ambazo kwa kweli zinasikitisha sana. Nitazungumzia tozo ambazo zinatozwa marehemu kwenye hospitali zetu. Mtu amefiwa na ndugu yake, amemuuguza kwa gharama kubwa, anaenda kulipa matibabu pale na yuko mortuary. Akifika mortuary tena anambiwa marehemu kalala siku tatu, Sh.60,000/=. Pale siyo guest. Yule ni Mtanzania, alikuwa analipa kodi wakati wa uhai wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, katika tozo alizozifuta naomba afute na tozo za maiti katika hospitali zetu. Tutafute sehemu nyingine ya kukusanya kodi lakini siyo kwa maiti, tuwaonee huruma wafiwa na marehemu wenyewe ambao wameshatangulia mbele ya haki na wakati wa uhai wao walikuwa wanalipa kodi kama Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia pia suala la viwanda. Tuna viwanda vingi takriban 53,050 katika nchi yetu na kuna viwanda 3,306 ambavyo vinafanya kazi. Naishauri Serikali, kwanza tuanze na vile viwanda vikubwa vilivyobinafsishwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi hapa kaona kuna watu walimilikishwa mashamba wakashindwa kuyaendeleza, wakafutiwa hati zao. Sasa twende kwenye viwanda pia; viwanda vingi vilikuwepo na wawekezaji wameshindwa kuviendeleza. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati wanatafuta mapori ya kufyeka na kutengeneza viwanda vipya, tuanze kwanza na viwanda vya zamani, tuvifufue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitolea mfano hapa Mkoa wa Morogoro, kuna takriban viwanda vingi. Mwaka 1985 Morogoro ukifika ilikuwa unapata ajira, lakini nyumba hupati. Kulikuwa kuna kiwanda cha Canvas, Ceramics, Moproco, Magunia, Tanneries, Morogoro Shoes, Polyster; viwanda ni vingi zaidi ya kumi. Kuna Sukari Kilombero na Sukari Mtibwa. Viwanda vile tuvifuatilie. Viko zaidi za kumi na ajira zake siyo watu wawili watatu, vinaajiri watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunatafuta mapori ya kujenga viwanda, naishauri Serikali ipitie viwanda vyote vile vya zamani ambavyo hawaviendelezwi; kuna viwanda vya mafuta Moprocco, tulikuwa tunapata mafuta mazuri sana, lakini sasa hivi uzalishaji wake ni wa kusuasua. Tuvifuatilie tuone kama wale wawekezaji wameshindwa kuviendeleza tuvichukue ili tuwape wawekezaji wengine kuliko kuhangaika sasa hivi wananchi hawana ajira, viwanda vikubwa unaambiwa kiwanda kinahitaji watu wanne watano. Haiwezekani hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni sana wakati tunatafuta mchakato wa kukata mapori, tuangalie viwanda. Tanga kulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, kimekufa. Sasa hivi wanaweka depot ya mafuta. Kiwanda cha Mbolea kilikuwa kinasaidia wakulima wetu, naomba sana Waheshimiwa kila mkoa unajua kabisa Tanga kuna wakulima wa matunda. Tuanzishe viwanda vya matunda ili wakulima nao wapate sehemu ya kuuzia bidhaa zao. Tuanzishe viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana hapa hapa Tanzania kuwezesha wakulima wetu kulima na kwenda kuuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano General Tyre. Kiwanda hiki malighafi zake zinapatikana mikoa miwili tu; mpira unapatikana Tanga na Morogoro, lakini mashamba yake pia yana mgogoro mpaka sasa hivi. Ndiyo maana mwekezaji anashindwa kufanya uzalishaji. Kwa hiyo, nashauri kwa kuwa ardhi ya Tanga na Morogoro iko katika mikoa mingine, tuhamasishe wakulima wetu, tuwape mikopo Serikali isimamie hili ili mikoa mingine ilime kilimo cha mpira ili kuweza kupata malighafi katika kiwanda chetu cha General Tyre. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia pia mambo ya miundombinu. Madaraja yote Tanzania watu wanapita bure, lakini daraja la Kigamboni kuna tozo, watu wanatozwa pale. Wanatozwa kwa sababu NSSF pia imeshiriki ujenzi wa daraja lile. Sasa naishauri Serikali, ni muda mrefu sana sasa lile daraja watu hata ukiwaelezea wanaona limekaa kibiashara zaidi. Walielewa na matarajio ya wananchi wengi ni kwamba Daraja la kigamboni litakuwa kama lilivyokuwa Ruvu, daraja la Mkapa na Daraja la Kilombero watavuka bure. Sasa liko kibiashara zaidi, linawakwaza wananchi wa Mkoa Dar es Salaam hususan Wilaya mpya ya Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa huruma yake, najua kuna deni kubwa NSSF wanadai, lakini tuwasaidie watu wa Kigamboni. Kama ni kulipa hilo deni, basi madaraja ya Mkapa na Kilombero nayo yatozwe ili kusaidia daraja la Kigamboni nao watu wapite bure kama madaraja mengine. Kwa sababu inaonekana sasa lile halifanyiwi service, ni daraja kama madaraja mengine. Pale linaonekana liko kibiashara zaidi, hata ukipita, utakuta Polisi wana SMG wanalinda yale maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuangalie, hii huduma tunayoitoa kwa wananchi wetu iwe sawa na huduma katika mikoa mingine. Najua NSSF wanadai, lakini watafute mbinu ambayo itasaidia sasa wananchi wa Kigamboni nao wapate faraja katika daraja lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea Tanga. Nikinunua bidhaa kutoka Kariakoo nikipeleka kwetu Bumbuli nalipia tu usafiri, silipii chochote. Sasa Tanzania ni Muungano, ni nchi moja, angalau hata nikitoka Zanzibar, nikiingia Dar es Salaam, basi ushuru mdogo mdogo hata kama ni zawadi tuachiwe. Maana ukifika pale inaonekana ni nchi mbili tofauti, unadaiwa ushuru. Tufanye kama ninavyotoka hapa Tanga kwenda zangu Dar es Salaam nikiwa na bidhaa hata kama ni zawadi nilipie tu katika chombo cha usafiri, lakini siyo kulipia ushuru kama ilivyokuwa sasa na kuwapa nafuu ndugu zetu Wazanzibari na wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana.