Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Bismillah Rahmani Rahim .
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhannah Wataalah naomba nianze kuchangia hotuba hizi mbili, hotuba inayozungumzia Hali ya Uchumi wa Taifa na Mpango pamoja na Bajeti ya Serikali kwa kuanza na maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waingereza wanasema: “an old is wise, the more it hears, the less it speaks.” Waswahili wanasema kwamba, ndege huyu anayeitwa bundi ni ndege ambaye ana busara sana, lakini ukisikia bundi anazungumza, basi ujue kuna uchuro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza nitaongea maneno mazito kwenye Bunge hili katika hotuba hizi mbili ambapo sijawahi kuzungumza ambayo ni maagizo ya Wanamtwara. Jambo la kwanza, ili nchi yoyote iweze kuendelea, lazima kuwe na hali ya amani na utulivu. Hali ya amani inatengenezwa na Serikali iliyoko madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nazungumza ndani ya Bunge hili kwa muda mrefu sana, kwamba Serikali kwa mwaka 2012/2013, ilitengeneza mazingira ambayo hivi sasa nami nimechaguliwa kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, ambalo ni Jimbo mama Kanda ya Kusini na Waheshimiwa Wabunge wote wa Mikoa ya Kusini wana majumba ama wana viwanja vyao Jimbo la Mtwara Mjini. Hii inadhihirisha kwamba Mtwara Mjini ndiyo Jimbo mama Kanda ya Kusini. Wananchi wakanichagua mimi Maftaha Nachuma kuwa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, nije kuwakilisha kero za wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero ya kwanza ambayo walinipa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ni kuja kuzungumza ndani ya Bunge hili kuiambia Serikali iliyoko madarakani suala zima la maslahi ya gesi. Jambo la pili, ambalo walinituma wananchi wananchi wa Mtwara kuja kuzungumza ndani ya Bunge hili, kufikisha kilio chao, ni suala zima la migogoro ya ardhi ambayo Serikali ya Awamu ya Nne na Serikali zilizopita huko nyuma zilidhulumu wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini kwa kiasi kikubwa sana. Hali ilikuwa ni tete kweli kweli, wananchi wakanituma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa kwanza mkubwa ni mgogoro ambao Serikali ilichukua maeneo mwaka 2012/2013. Maeneo ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, panaitwa Mji mwema, Serikali iliahidi kulipa fidia. Eneo la Mji Mwema, limekuwa linazungumzwa suala hili, nimeleta swali siku ya pili, baada ya kufika Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura Mtwara Mjini, alielezwa kero hii na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Mwaka 2017 alipokuja Mtwara alielezwa jambo hili na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini pale kwenye Uwanja wa Mashujaa. Nikazungumza ndani ya Bunge hili zaidi ya mara tatu. Nimefikisha, nikapewa Hansard mbili ndani ya Bunge hili, kwamba Serikali iko tayari kulipa fidia ya wananchi hawa, wananchi 2,200. Hapa naomba nilithibitiishie Bunge hili, kwa sababu hili limekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezuia maandamano zaidi ya mara 10, wananchi wanataka kuandamana kwa sababu wamechukuliwa maeneo yao, wakaambiwa wasiyaendeleze. Nilipewa Hansard hapa na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwamba wanaenda kulipa. Mwisho wa siku wanakuja ndani ya Bunge hili, wanasema hatuwezi tena kulipa kama Serikali. Nikiuliza upande wa pili naambiwa, Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango hataki kupeleka fedha kupitia Taasisi ya UTTPID ambayo ilichukua maeneo haya ya Jimbo la Mtwara Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme Wanamtwara wanisikie. Kilio chao walichoniagiza nije kueleza ndani ya Bunge hili, wakaandamana kwa kiasi kikubwa ili niweze kutangazwa tarehe 26, nilivyoshinda zaidi ya vyama vitano pale Mtwara Mjini. Naomba nisome hii Hansard na Mwenyezi Mungu aweze kunishuhudia leo kwamba leo kilio cha Wanamtwara nimefikisha kwa mara nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hansard ya mwaka 2017 anasema: “Mheshimiwa Spika, fidia stahiki itaanza kulipwa kwa wananchi 2020 kuanzia mwezi Juni, 2017 hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018. Taasisi ya UTTPID (narudia tena Taasisi ya UTTPID) ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Halmashauri, inatarajia kutumia shilingi bilioni 7,523 kwa ajili ya malipo ya fidia kabla ya kuanza kwa kazi ya upimaji wa viwanja. Ofisi ya Rais TAMISEMI, ilitoa kibali cha kuendelea na utekelezaji wa mradi kupitia barua yenye kumbukumbu Namba GB203/234/01/117 ya tarehe 2 Septemba, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ulipaji wa fidia haukuanza mapema kutokana na Kampuni husika ya UTTPID, kutokuwa na Bodi. Bodi imeshaundwa na makubaliano ya pamoja yamefanyika katika Kikao cha tarehe 2 Mei, 2017 baina ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, UTTPID na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Hansard mbili ndani ya Bunge hili, Serikali ikiahidi kulipa fidia hizi pesa, shilingi bilioni saba kwa wananchi hawa wa Jimbo la Mtwara Mjini. Katika Mtaa wa Mji Mwema. Jambo hili limekuwa tete sana Mtwara. Nimezuia maandamano zaidi ya 10. Narudia tena, sasa nazungumza ndani ya hili Bunge lako Tukufu, safari hii nikiondoka hapa kwenda kwenye Jimbo la Mtwara Mjini, kwa sababu wananchi wamenituma kwa mara nyingine tena, naenda kutangaza maandamano makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maandamano hayo, aje kuyapokea Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu kaambiwa maneno haya ndani ya Jimbo la Mtwara Mjini zaidi ya mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo wamenituma wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini nizungumze hapa, ni suala hili, wenzangu wamezungumza; suala la pesa za korosho ambazo zilikusanywa, kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha korosho Mtwara na maeneo mengine. Kwa sababu Jimbo la Mtwara Mjini pia nina AMCOS zaidi ya mbili pale; nina AMCOS ya Mikindani na ya Naliendele. Zimekusanywa pesa za Export Levy. Pesa zilizokusanywa ni zaidi ya shilingi bilioni 210 ambazo zilitakiwa ziende kununua sulphur kuendeleza kilimo cha korosho. Zile pesa hazijaletwa Kusini kwa ajili ya kuendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana sana na hoja na mwelekeo wa Serikali hivi sasa, kwa sababu nchi zote zilizoendelea duniani walikuwa na sera tunasema, Strong State Intervention, kwamba lazima Serikali iwe na meno katika kusimamia uchumi. Napongeza hilo kwa sababu Serikali dira yake ni hiyo. Wenzangu wamezungumza kwamba tunahitaji kuwa decentralization sasa hivi inakufa, hapana. Ili nchi iweze kuendelea, lazima kuwe na Strong State Intervention.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kununua ndege ambazo zinaenda kuchochea Utalii hivi sasa Tanzania nzima. Ndege ni kielelezo kwamba ili nchi iweze kuendelea wageni waweze kuja ndani ya nchi kuleta pesa za kigeni, lazima tuwe na usafiri. Katika hilo niwashauri sana kwamba lazima tutoke na sisi kwenda kujenga mahusiano nje ya nchi ili tuweze kushawishi wawekezaji, kama Wabunge, kama Serikali, kama wananchi, Watanzania waweze kuja kuwekeza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayazungumza haya kwamba zile fedha za korosho ambazo Serikali ilikusanya shilingi bilioni 210 tunaomba zirudi. Mheshimiwa Dkt. Mpango, kazungumza hapa kwamba mwaka huu anapendekeza sheria kwamba pesa zote zinazokusanywa kupitia Bodi za Mazao zipelekwe katika Mfuko Mkuu wa Serikali, zikusanywe na TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema sheria haiendi retrospective. Sheria hairudi nyuma. Zile pesa zilikusanywa kabla ya hii sheria, shilingi bilioni 210. Wananchi wa Mikoa ya Kusini, Mtwara na Lindi ambao ndio walimaji wakubwa wa korosho, mwaka huu wamekosa sulphur kwa sababu hizi pesa hazijaenda. Wanasema katufikishie kilio hiki Mbunge wetu, kwamba tunataka zile pesa ziweze kuletwa ziendeleze hata kwa mwakani. Vinginevyo watafanya maandamano makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza maneno haya, sijawahi kuzungumza ndani ya Bunge hili. Hiki ni kilio cha wananchi wa Kusini, ni kilio cha wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Nimekuwa natumia busara nyingi sana, kila mtu anafahamu ndani ya Bunge hili kwamba ukisikia maandamano yameanza Kusini, yameanzia Mtwara Mjini. Nimekuwa natumia busara nyingi sana kuongea na vyombo vya Serikali, kuongea na vyombo vya Dola na kuwashawishi wananchi kuleta amani na utulivu ndani ya Majimbo ya Kusini kwa kuanzia na Mtwara Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, amekuwa hajibu maswali yangu, amekuwa hajibu hoja zangu; nimezungumza maneno haya wakati amewasilisha Bajeti yake, hakujibu hata moja. Hajajibu hata hoja moja na anazungumza kwamba ni maneno ya wananchi wa Mtwara. Mheshimiwa Dkt. Mpango amekuwa hajibu hoja za wananchi wa Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ananisikia ninavyozungumza maneno haya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aje kupokea maandamano makubwa kwa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini na Mikoa ya Kusini kwa kupokwa haki zetu hizi. Wananchi hawawezi kuchukuliwa maeneo zaidi ya miaka mitano mpaka hivi sasa hawajalipwa fidia zao na wala Serikali haisemi chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana Mheshimiwa Dkt. Mpango atakapokuja kuhitimisha hoja yake, mwaka 2017 niliunga mkono Bajeti hapa, nikasema ndiyo. Kama hatatoa hizi pesa shilingi bilioni nane hata kwa kunyang’anya, kwa kukopa na kufanyaje, waleteni. Wachukue kwenye korosho walipe wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, yale maeneo ya Mji Mwema, wanalalamika sana, wameambiwa kwamba eti wapimiwe tena viwanja, wamechukuliwa zaidi ya miaka mitano, halafu virudi tena. Haiwezekani, huku ni kuwadharau wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.