Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Pili, ninawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga kwa ushirikiano ambao wananipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kuchangia kwenye Mpango. Katika kitabu cha mpango, ukurasa wa tisa, limeelezwa kwamba pato halisi la Serikali limefikia trilioni 50 vilevile pia ni ongezeko la karibu trilioni 3.35 ukilinganisha na mwaka 2016.

Sasa hapa naona kuna marekebisho kidogo kwa sababu ukipiga hesabu vizuri, mgawanyo wa pato la Taifa kwa kipato cha kila Mtanzania kupata shilingi 2,275,601,000 kutoka shilingi 2,086,168,000 za mwaka 2016 naona panahitaji marekebisho kidogo. Namuomba Waziri alifanyie marekebisho hili ili kusudi hesabu hizi zikae sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la mfumuko wa bei. Katika Mpango ukurasa wa 12 kwenye kitabu kimeeleza kwamba mwenendo wa mfumuko wa bei ulikuwa tulivu. Sasa ukisema kwamba mfumuko wa bei ulikuwa tulivu wakati tuna mifano hai katika mwezi Mtukufu tu wa Ramadhani uliopita juzi ambapo leo ni siku nne tangu umemalizika, naona sio sawasawa. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu ukiangalia bei ya kio moja ya tambi kutoka shilingi 1,800 ilipanda mpaka shilingi 2,500 vilevile pia sukari kutoka kilo moja shilingi 2,000 ilipanda mpaka shilingi 2,500, ngano kutoka 1,200 ilipanda mpaka shilingi 1,800, vilevile pia mafuta ya kula kutoka shilingi 2,200 kwa lita yalipanda mpaka shilingi 3,000. Sasa tukisema kwamba eti mfumuko wa bei ulikuwa tulivu naona hilo haliko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza katika kitabu chetu hiki cha Mpango ni katika ukurasa wa 55 kuna ubia kati ya Sekta ya umma na sekta binafsi. Nimeona kwamba wamezungumzia zaidi katika masuala ya viwanda kwamba sekta ya umma ishirikiane au iwe na ubia na Serikali lakini kuna vyanzo vingine ambavyo vingeweza kuisaidia Serikali kimapato. Kwa mfano, kama Serikali ingeweza kuingia ubia na sekta binafsi na kuweza kujenga viwanja vya michezo kama vile michezo ya football, basketball, golf na tennis, angalau pia tungekuwa hapo tumeweka mazingira mazuri kati ya Serikali na sekta binafsi na ingeweza kutupatia kipato kwa sababu katika mipango hiyo sikuiona katika kitabu, sasa nashauri mipango hiyo nayo iingizwe katika Mpango wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni uandaaji wa wachezaji wetu. Nchi za wenzetu nyingi zimekuwa zinanufaika baada ya wachezaji wao kuwa wanacheza katika nchi za Ulaya. Kwa mfano, nchi kama Nigeria, Senegal, Mali, Tunisia, Algeria na nyinginezo, wameweza kukusanya mapato, hata Brazil Serikali inakusanya kodi kutoka kwa wachezaji kwa sababu kunakuwa na maandalizi maalum, lakini katika kitabu hiki sijaona kama kuna mpango wa kuiendeleza sekta ya michezo kupitia hivyo viwanja hata kwa wachezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia sasa niende moja kwa moja kwenye bajeti yetu. Katika bajeti kuna kitu ambacho ninakiona hakiko sawa, kwa mfano, katika bajeti ya Wizara ya Kilimo tumeona hapa kuna upungufu wa karibu asilimia 23 ambayo ni sawasawa na karibu kwa mfano katika fedha za korosho kuna pesa ambazo zilikuwa ni shilingi bilioni 211 za Mikoa ya Kusini, hizi zimeleta mkanganyiko, hazijapelekwa na hazijulikani ziko wapi.

Sasa atakapokuja Waziri hapa atueleze pia kwanini ninagusa kwenye zao la korosho kwa sababu na sisi Tanga katika baadhi ya maeneo korosho zinalimwa. Sasa ikiwa imeguswa Mikoa ya Kusini maana yake na Tanga pia imeguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni katika kupunguza kodi kwa taulo za kike. Mimi naipongeza Serikali kwamba imepunguza kodi, lakini katika siku za karibuni mimi nilichangia nikatoa mfano wa nchi ya Kenya. Rais Uhuru Kenyatta alitia saini sheria ambayo Kenya watazitoa taulo bure badala ya kusema wanapunguza kodi. Kwa nini ninalisema hili? Kenya wameondoa kodi lakini wakaamua pia zitolewe bure, hapa katika viwanda ambavyo vinazalisha hizo taulo za kike, baadhi ya viwanda vimepunguziwa tu kodi, lakini baadhi ya kodi zipo. Kwa hiyo, tufikirie wale watoto wa kike ambao wako maeneo ya vijijini, hiyo taulo ya kike iliyokuwa inauzwa shilingi 3,500 hata ikiuzwa shilingi 1,500 bado kwao itakuwa ni tatizo kwa sababu hawana njia za kipato ambazo zitawawezesha kulipia taulo hizo za kike. Kwa hiyo, naishauri Serikali badala ya kuondoa kodi, zitolewe bure kwa watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulichangia ni kuhusu wastaafu. Serikali yetu kwanza katika kipindi cha miaka miwili hii tumeshindwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi. Sasa bado pamoja na kushindwa kuongeza mishahara, kuna tatizo la wastaafu, wale waliokuwa watumishi wa Serikali waliongezewa kutoka shilingi 50,000 mpaka shilingi 100,000 tena wanalipwa kila mwezi, lakini wale waliokuwa watumishi wa mashirika ya umma bado wako pale pale katika kiwango cha shilingi 50,000 na wanaendelea kulipwa shilingi 50,000 tena kwa malimbikizo baada ya kila miezi mitatu.

Kwa hiyo, naishauri Serikali kwanza hawa wastaafu waliokuwa katika Mashirika ya Umma nao waongezewe wafikie shilingi 100,000 lakini walipwe kila mwezi na isiwe wanalipwa kila baada ya miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninalopenda kulizungumza ni deni la ndani tumeambiwa ni himilivu, lakini bado kuna wazabuni ambao wana-supply vyakula katika magereza, katika shule na taasisi nyingine ambazo zinahitaji vyakula kama vile hospitali. Wazabuni hawa wengine wanapelekwa mahakamani, wanadaiwa kwa muda mrefu na kila mwaka imekuwa inatolewa ahadi tu kwamba wataanza kulipwa.

Kwa hiyo, nashauri Serikali ituambie hapa/Waziri atakapokuja atuambie ni lini wataanza kuwalipa wazabuni ambao wanaidai Serikali. Kwa mfano, katika Jiji letu la Tanga wapo wazabuni wengi tu ambao wanadai ambao wame- supply vyakula magerezani, hospitalini na shuleni, lakini nimeshuhudia wengine wanataka kufilisiwa, walichukua mikopo kwenye benki, wanashindwa kulipa mikopo ile lakini Serikali inaendelea kuwapa ahadi. Naitaka Serikali ijibu kwamba ni lini wazabuni wale watalipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni katika miradi. Miradi bado inapelekewa fedha kwa kuchelewa na fedha hizi zinakuwa hazitoshi na bahati mbaya mara nyingi zinapelekwa katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha wa Serikali matokeo yake sasa miradi baada ya kuwa fedha zimeshafika Wakurugenzi, wataalam na wanaohusika wengine inapelekwa haraka haraka matokeo yake inakuwa chini ya viwango. Kwa hiyo, naishauri Serikali iendelee kupeleka fedha mapema lakini pia namtaka Waziri wa Fedha Tanga katika Halmashauri yetu tumetenga shilingi milioni 300 kwa jengo la Hospitali ya Wilaya na tulikwishaanza kipindikilichopita (mwaka jana) tukajenga administration block kwa takriban shilingi milioni 400 lakini sasa hatujapata fedha kwa ajili ya kuweka hii OPD, kwa hiyo naiomba Serikali ituongezee fedha ili tuweze kujenga jengo la OPD.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kuhusu wastaafu wanaotarajiwa kustaafu, kama Serikali imeshindwa kuwalipa wafanyakazi au kuwaongezea mishahara katika miaka miwili hii, je hawa watakaostaafu mwaka huu, Serikali ina fedha za kuwalipa? Naomba atuthibitishie Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba hata watakaostaafu waweze kulipwa fedha zao. Kwa nini nalisema hili? Naogopa kwamba Watanzania wataendelea kuwa maskini na mtu baada ya kustaafu anakuwa hana umri mrefu, anapoteza maisha kwa sababu anakuwa hana kipato. Kwa hiyo, ninamtaka Waziri atakapokuja hapa aje atuambie kwamba wamejiandaa vipi kuwalipa wastaafu wanaotarajiwa kwa sababu watumishi wengi wa Serikali ni wastaafu watarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.