Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kwa kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu. Kwa namna ya kipekee, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri na ya kizalendo anayoifanya katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Ndugu yangu Mheshimiwa Silinde namheshimu na najua wakati mwingine anachangia vizuri, lakini kuna watu katika nchi zingine wanampongeza Mheshimiwa Dkt. Magufuli anafanya vizuri. Profesa Patrick Lumumba mpaka amembandika jina na kumuita Magufulification kutokana na performance yake. Kuna watu wanataka kujifunza the way Mheshimiwa Dkt. Magufuli anavyofanya kazi nzuri katika nchi ya Tanzania. Kwa hiyo, mnyonge mnyongeni lakini kuna maeneo tunafanya vizuri. Katika nchi za Afrika Mashariki na Kati hata wenzetu wa Kenya wanatamani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais wao. Ameweza kusimamia matumizi ya pesa kwa nidhamu na kuna baadhi ya mambo makubwa ambayo tumeweza kuyafanya kwa hela yetu hiyo ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni rasimu ya bajeti na siyo bajeti. Sisi Wabunge ni wajibu wetu kuikosoa na kuielekeza Serikali kwenye maeneo ambayo tunaona kuna upungufu. Kwa hiyo, tukikataa kabisa kwamba hakuna jambo la maana lililofanywa kwenye hii rasimu ya bajeti tutakuwa tunakosea. Yapo mambo mazuri Mheshimiwa Dkt. Mpango amekuja nayo nasi lazima tuyaunge mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni viongozi wa wananchi, tumetoka kwenye Majimbo yetu, pamoja na uzuri wa rasimu hii ya bajeti lakini kuna maeneo Mheshimiwa Dkt. Mpango alitakwa ayaangalie kwa ukaribu sana kwa sababu yanawagusa watu direct. Kwa mfano, eneo la kilimo linaajiri Watanzania wasiopungua asilimia 66.6 na yeye anajua, lakini ukiangalia bajeti iliyokwenda kwenye eneo hili hairidhishi kabisa. Tunaomba aliangalie maana tulitakiwa tuweke bajeti ya kutosha kwa sababu kwenye eneo hili kuna ajira, kuna usalama wa chakula, kuna malighafi ya viwanda ambapo tunataka twende kwenye uchumi wa viwanda. Sasa tusipowekeza vizuri kwenye eneo la kilimo tunategemea nini, tutaendaje kwenye uchumi wa viwanda? Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango tuliangalie mara mbili eneo hili la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wenzentu ambao tumesoma bajeti pamoja nchi za Afrika Mashariki na Kati, asilimia 10 ya bajeti nzima ndiyo wametenga kwenye bajeti ya kilimo, lakini bajeti yetu haifiki hata asilimia 3. Sasa tujiangalietutafika huko. Shilingi bilioni 170 against shilingi triolioni 32 wapi na wapi? Tutakwenda kwenye uchumi wa viwanda kweli? Kwa hiyo, Mheshimia Dkt. Mpango naomba sana eneo hilo tuliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambayo anaiongoza mwenyewe. Wale watu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo hawapeleki hela kwa wakulima. Walianza na mtaji wa shilingi bilioni 60, ukakua ukafika shilingi bilioni 67, wakakopa mpaka wakafika shilingi bilioni 287, lakini tujiulize kwenye shilingi bilioni 287 ni kiasi gani wamewakopesha wakulima? Utakuta hela zile wanazokopa na wenyewe wanaenda kuweka dhamana kwenye mabenki mengine, ndiyo madhumuni ya kufungwa hiyo benki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye jambo hili nataka awaambie tumeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima siyo kwa ajili kufanya biashara. Wafanye yale ambayo tumekubaliana katika uanzishaji wa Benki hii ya Kilimo, kwenye jambo hili hatuko sawa. Mahitaji ya Watanzania kwenye eneo hili ni shilingi bilioni 800 lakini hata shilingi bilioni 287 zingekuwa zinakwenda direct kwa wakulima sasa hivi wakulima wangekuwa wamebadilika kwenye eneo hili. Kwa hiyo, naomba eneo hili tuliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo amelizungumzia ni suala la Bodi ya Mazao Mchanganyiko, amesema wanataka kuunganisha Bodi. Mheshimiwa Dkt. Mpango, hawa wananchi ndiyo wanatengeneza hela zao pale, mnataka mfanye nini pale, interest yenu ni ipi? Kama kuna watu wana ubadhirifu wa hela si wapelekwe Mahakamani. Wamelalamika kwenye maeneo ya korosho lakini hakuna hata mtu mmoja mpaka leo amepelekwa mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sikubaliani na hoja ya kutaka kuunganisha Bodi, kwenye eneo hili siwezi kukubaliana hata kidogo. Mkitaka kwenda vizuri kwenye eneo hili angalieni Bodi za Udhibiti (Regulatory Board) zina tozo mbalimbali ambazo hazina tija na tozo hizo zinawagandamiza sana wakulima na kuwaongezea gharama. Kwa hiyo, naomba tuangalie sana kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wana shida ya maji na Wabunge wote tulikuwa tunasema hapa tunataka maji na mpaka tukasema tuko tayari kuwashawishi watu wetu kuongeza tozo la shilingi hamsini, lakini hakuna respond yoyote tuliyopata. Mwaka jana collection ya ndani iliyokuwa inatakiwa iende kwenye maji ilikuwa shilingi bilioni 250 lakini mpaka tunakuja kwenye bajeti ni shilingi bilioni 26 tu ambayo ni asilima 11 ya collection ya ndani ambayo ilikwenda kwenye maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti ambayo ilikuwa inatokana na Mfuko wa Maji ya shilingi bilioni 158 hela zote karibu zimekwenda kwenye miradi ya maji. Kwa hiyo, tukiongeza kwenye eneo hili tutafika mbali. Sasa Waziri hajakubaliana na shilingi hamsini angesema basi niwafikirie hawa Wabunge hata niwape shilingi thelathini au shilingi ishirini, akituacha hivi anatuacha solemba. Kazi ya Wabunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, lakini inawezekana ikawa kila siku tunashauri hakuna hata siku moja mmewahi kuchukua mawazo ya Wabunge mkaamua kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, tunaomba eneo hili mliangalie.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine Mheshimiwa Dkt. Mpango amezungumza vizuri sana kuhusu kusamehe kodi kwenye chakula cha mifugo, yuko sahihi. Kama unasamehe kodi kwenye chakula cha mifugo halafu unatoza kodi kwenye mashudu umesamehe wapi sasa hapo? Unasamehe kushoto kulia unachukua hela ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sikubaliani na hiyo hoja, hujasamehe hapo. Umetuvisha blanketi hapo, kwamba nimesamehe kodi kwenye chakula cha mifugo halafu unasema mashudu yatozwe VAT, haiwezekani. Kama tumeamua kusamehe kodi, iwe ni kwenye maeneo yote ili kusudi tupate tija kwenye eneo la kilimo.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni suala la viwanda vya maziwa na nyama. Mheshimiwa Waziri yuko sahihi, ameamua kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuongeza kodi ya mazao ya mifugo kwa maana ya mazao ya nyama na maziwa yanayotoka nje ya nchi, lakini tunavisaidiaje viwanda vya ndani hapa. Namwomba ili kusudi twende kwenye ushindani halali, maana sasa hivi maziwa yetu ukilinganisha na maziwa ya Kenya na yanayotoka Uganda maziwa ya Tanzania gharama zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja.