Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu lakini pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa bajeti hii ambayo mipango yake imekaa vizuri, yapo maeneo ambayo tunapaswa kuishauri Serikali vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliweke jambo moja sawa, unajua mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, Mheshimiwa Dkt. Mpango alisema vizuri sana, amesoma vitabu vya viongozi hawa amejifunza best practice na worse practice sasa afute nini? Mheshimiwa Dkt. Mpango nikupongeze sana. Nadhani mimi nilikuelewa vizuri wakati umezungumza na hiyo itakuwa imetusaidia sana lazima ujifunze sehemu zote mbili.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejikita katika uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu kwa jamii. Likisemwa hivi kwenye bajeti maana yake lazima tuone indicator za kuelekea kwenye uchumi wa viwanda. Serikali imeeleza vizuri imepunguza Corporate Tax kwenye kilimo lakini kwenye bidhaa za ngozi, nataka nijielekeze kwenye bidhaa za ngozi. Tukizungumzia bidhaa za ngozi ni lazima tujue kama viwanda vyenyewe vya kutengeneza ngozi vipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka hapa tujielekeze vizuri sana, tulikuwa na viwanda vya ngozi mimi sidhani kama vipo. Leo Mwanza hatuna kiwanda cha ngozi, ile Mwanza Tannery imebaki kuwa go-down. Ukienda Arusha kipo kiwanda kimoja kazi yake kubwa ni kutengeneza wet blue, inalainisha tu ile ngozi na kuisafirisha kwenda nje. Tuna Himo Tannery na tuna Kiwanda cha Moshi Leather ambacho kimefungwa. Morogoro tulikuwa na kiwanda pale na chenyewe kimefungwa kilikuwa kinafanya temporary.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujiuliza tumepunguza kodi kutoka asilimia 30 kwenda 20 kwenye bidhaa za ngozi wakati viwanda hamna. Nataka Serikali itusaidie hapa na nishauri vizuri, leo bidhaa ya ngozi hii tunayoizungumza ngozi yenyewe imeshuka thamani. Ngozi leo kilo moja inauzwa Sh.200 mpaka Sh.500 lakini hivyo viwanda viwili vinavyofanya finishing kwa maana ya Himo na Moshi Tannery, Himo tu kinaweza kununua ngozi tani 100 peke yake, Dar es Salaam peke yake inazalisha kwa siku ngozi tani 45 maana yake Dar es Salaam peke yake inaweza ikalisha hivi viwanda viwili basi, kwa hiyo, mikoa yote hii ikiwemo na Singida ngozi yetu imekosa thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa lazima tuishauri Serikali vizuri na iwe makini kwenye jambo hili. Tunapotaka kuonesha indicator kwenda kwenye viwanda kuna eneo la muhimu sana, tunataka mashine ziingie humu lakini kwenye Customs Duty ni lazima tuondoe Import Duty na VAT asilimia 18. Itakuwa imetusaida mno kwenye eneo hili ili viwanda na mashine ziingie ili tuweze kuanzisha hivi viwanda tofauti na hapo hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda lakini bidhaa tunazo. Ngozi hii tunayoizungumza ukitaka kuitoa nje unalipa kodi asilimia 80 maana yake ngozi ambayo umeinunua kilo Sh.500 unalipa kodi Sh.1,200 utaenda kuiuza wapi lakini ngozi inateseka leo. Nataka niiombe Serikali wakati tunajiandaa kuweka viwanda hivi iruhusu ngozi hii iuzwe ili Serikali ipate mapato na wananchi waweze ku- survive. Kwenye eneo hili nilikuwa nataka niombe Serikali iliweke vizuri sana taarifa hii haiko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata kwenye kilimo, nchi yetu leo kilimo ni uti wa mgongo kuondoa Corporate Tax kwa asilimia 10 peke yake haitoshi. Nashauri tuweke zero tu kabisa walau kwa miaka miwili itatusaidia sana ku-promote eneo hili la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko Regulatory Authority TFDA, TBS, TPRI, NEMC, Vipimo na wengine wengi. Tumezungumza sana kwenye bajeti iliyopita kwamba ifike mahali tu-harmonize hizi Regulatory Authority zote zinafanya kazi moja. Kila mmoja anakwenda kwa mfanyabiashara anatoza ada. Sasa tukaomba tufanye One Shop Stop Center nataka kusema leo hii nayo haiwezekani hawa wote wanafanya kazi ya Serikali, niiombe Serikali ilipwe ada moja tu ya mfanyabiashara kulingana na kiwango; kama mfanyabiashara ana mtaji wake wa Sh.100,000 mpaka Sh.10,000,000 whatever alipe ada moja tu hawa kazi yao waende wakatoe certificate, basi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aende kwenye kiwanda kwa mfanyabiashara akague atoe taarifa Serikalini siyo na yeye aende akatoze faini na yeye anataka ada, hatuwezi kufika. Tunataka indicator hizi ziwekwe sawa. Kama tunataka uchumi wa viwanda hizi Regulatory Authority ni sehemu ya kumomonyoa hatuwezi kufika, ilipwe ada moja tu Serikalini. Mtu akilipa ada moja hawa kazi yao waende wakafanye auditing kuangalia kama hiyo bidhaa ni halali ama sio halali watoe taarifa Serikalini. Wanalipwa mshahara na Serikali lakini hawana sababu ya wao kuanzisha vyanzo vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwenye eneo moja la betting, amezungumzia Sheria ya Michezo ya Kubahatisha (sport betting) imeongeza kodi kutoka asilimia 6 mpaka 10 lakini kwenye slot mashine Sh.35,000 mpaka Sh.100,000. Tukizungumzia sport betting maana yake tunazungumzia Watanzania sasa wameamka na mwamko huu ni wa eneo la soka, wapenzi na wanachama wa soka wameona sasa kuna haja ya kuingia kwenye eneo hili na Serikali inapata mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa isiishie hapo, nataka nioneshe na eneo lingine kila mchezo wa soka unaochezwa Tanzania kwenye viwanja vyetu tunalipa VAT baada ya kutoa yale mapato yote get collection wanatoa asilimia 18 inayobaki ndiyo wanaita asilimia 100 wanaanza kugawana. Naiomba Serikali kwenye eneo hili tunataka kuboresha michezo Tanzania na tuboreshe mchezo huu wa soka ili tupate mapato zaidi maana yake hii asilimia 4 na hii shilingi sabini na kitu inayoongezeka tuwape Baraza la Michezo la Taifa ili liweze kujielekeza kuhakikisha kwamba tunapata viwanja na kuboresha mchezo huu wa soka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania hii leo hata ukipewa msaada wa vifaa vya michezo kutoka nje maana yake unalipa kodi. Sasa niiombe Serikali vifaa vya michezo hivi hebu viingie bure hatuna sababu ya kulipa Import Duty wala VAT sababu tunaboresha michezo Tanzania. Nataka niiombe sana Serikali eneo hili iliangalie vizuri sana. Hata ile asilimia 18 ya get collection ambayo inapatikana kwenye viwanja wapeni Baraza la Michezo waweze kuboresha michezo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lingine la wafanyakazi hapa, niipongeze Serikali kwa kuweka single digit kwenye Income Tax lakini single digit tunayoizungumza hapa inazungumzika kwenye eneo la kima cha chini, hao wengine inaendelea kama kawaida. Serikali izungumze single digit kwenye Income Tax kwenye mshahara wote bila kujali kima cha mshahara cha mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu alifafanua vizuri sana kuhusu mishahara ya wafanyakazi, sina sababu ya kurudia eneo hili kwa sababu ya muda lakini nataka niombe eneo moja muhimu sana. Tangu Serikali imeingia madarakani mwaka 2015 tulianza zoezi la uhakiki la wafanyakazi tukasimamisha madaraja ya watumishi wakiwemo walimu, madaraja haya yamesimama mpaka leo. Maana yake mtu aliyeanza kazi 2015 na 2012, 2018 tutawakusanya pamoja waweze kulipwa daraja moja, this is unfair, halitakubalika. Niombe kama alistahili kupanda daraja 2015 kama anaenda daraja D, mwaka 2018 alipaswa kuwa daraja E apewe daraja lake la sasa E na tusirudi huko kumpa daraja D, tutakuwa tumemuonea. Nataka niiombe sana Serikali kwenye eneo hili itusaidie ihakikishe watumishi wetu wanapata haki yao. Hawa watumishi hawana kosa lolote, uhakiki ulikuwa ni wa kwetu wenyewe Serikali siyo wa watumishi, tutoe mwongozo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie eneo lingine la PPP (Public Private Partnership). Nataka niende haraka hapa nitolee mfano, leo eneo la UDART pale Dar es Salaam kwenye usafirishaji mwendokasi mradi ule unakufa lakini Serikali tuna asilimia 49, mtu anaye-hold share na sisi ana asilimia 51, mradi unakufa. Mradi unakufa kwa sababu gani na Serikali imekaa kimya?
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi tunaendelea nayo, juzi Mheshimiwa Rais amezindua Agricultural Sector Development Program Phase II lakini Phase I hatujaitathmini ikoje. Hapa tunazungumzia PPP, hata tunapokwenda kwenye standard gauge tunatarajia kwenda kwenye PPP tutakwendaje? Niombe Serikali ituletee taarifa kuhakikisha miradi hii ya PPP inatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.