Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Kojani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Naomba nianze na Kitabu cha Mpango kama Mheshimiwa Waziri Mpango alivyoelezea, kwenye ukurasa wa tisa uchumi wa Taifa, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba Pato la Taifa limepanda kutoka asilimia 7.0 hadi asilimia 7.1 ambapo pato hili lilikuwa ni trilioni 47.173 mpaka trilioni 50.5.
Mheshimiwa Spika, pato la Taifa najua ndilo linalo- determine kile kima cha kila mtu kwa nchi ile, sasa tukija kwenye kima cha kila Mtanzania kutokana na pato hili la Taifa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kima cha kila Mtanzania kitakuwa ni Sh.2,275,000 kutoka Sh.2,086,000.
Mheshimiwa Spika, tukichukua Pato la Taifa ambalo ni trilioni 50.5 sijui tugawe kwa idadi ya watu wangapi tulionao mpaka tupate milioni 2,275,000; kwa kweli naona kwamba bajeti imetudanganya katika kiwango hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hivyo kitabu cha CAG ukurasa wa 63 amesema kwamba Pato la Taifa ni trilioni 106.8 lakini kitabu cha Waziri Mpango kinasema ni trilioni 50.5, sasa sijui tushike ipi iliyo na ukweli ya CAG au ya Waziri Mpango? Inawezekana pengine na Kamati ya Bajeti na wao wana kima chao sijui ni ngapi. Kwa hiyo naomba Waziri atueleze je, wametumia takwimu ipi ya CAG ya kitabu cha Mpango katika kutuelezea pato la kila Mtanzania la 2,275,000 kwa kila mtu. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba niende kwenye mapato ya Taifa na matumizi. Bajeti ya 2018/2019, imekisia kwamba itakusanya trilioni 32.48, sasa tukija katika matumizi yaliyopangwa, tumepanga kwamba tutalipa madeni ya Serikali ambayo ni trillioni 10, sasa trilioni 10 hizi tukizilipa kwa mwaka tunakuta kila mwezi tukichukua calculation ya kila mwezi tunatakiwa tulipe bilioni 833.33, lakini baadaye tunakuwa na mishahara ambayo tumepanga kwamba kwa mwaka tutatumia trilioni 7.409. Hii tukiigawa kwa mwezi tunapata kwamba kila mwezi tunatakiwa tutumie bilioni 617, ambazo tukujumuisha hizi za madeni tu na mishahara ni karibu trilioni 1.4 wakati makusanyo ya Taifa tunasema ni kati ya trilioni 1.2 mpaka 1.3, hatujaingiza matumizi mengine hatujaingiza miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, matumizi mengine Serikali imepanga kwamba itatumia trilioni 3.054 kwa mwaka ambapo kwa kila mwezi tunatakiwa tutumie bilioni 254. Miradi tumepanga kwamba tutatumia trilioni 12, hizi tumesema trilioni 2.13 ni mapato ya nje, tuyaweke mbali inamaana tuna trilioni 10 ambazo zinatokana na mapato ya ndani. Trilioni 10 hizi tukigawa kila mwezi tunapata bilioni 833.33. Sasa tukijumlisha yote tunakuta kwamba tukitoa zile bilioni mbili tuwe na makusanyo ya shilingi trilioni 2.529, hivi kweli Serikali tuna uwezo wa kukusanya mapato haya kwa kila mwezi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watueleze Serikali wana mikakati gani wakati trend ya 2016/2017, imeonesha tumekusanya trilioni 21, trend ya 2017/2018 tumekusanya pia trilioni 21.89 je, kuna mikakati gani waliyoiandaa mpaka kuweka makisio makubwa kiasi hichi. Hii bajeti ni ya udanganyifu na wala haitekelezeki. Kwa hali hii inaonesha kwamba mkakati huu uliopangwa wa mapato na matumizi wote ni hewa, bajeti haitekelezeki. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tatu, naomba niende kwenye kueleza kwamba bajeti yetu ni hewa, tunapanga makubwa makusanyo yetu lakini uwezo wa kukusanya ni mdogo. Mwaka 2016/2017 tulipanga makusanyo ya trilioni 29.54 tukakusanya trilioni 20 ambayo ni sawa na asilimia 70, asilimia 30 hazipo, kwa hivyo inaonesha kwamba hizi asilimia 30 tulijikusanyia tu kumbe ni hewa hazipo, sawa tulijipangia kumbe ni hewa hazipo.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 tukaongeza yaani ule mzigo mdogo tuliokuwa nao 2016/2017, tukauona kwamba ni mdogo tukaongeza mwingine tukajikusanyia huku mgongoni kutoka 29 tukaja 31, hii 29 haikutekelezeka jamani tunakuja 31. Nashauri bora tungerudi nyuma tukaangalia ule uwezo wetu, kwamba hatuna uwezo wa nakusanyo ya trilioni 29 tuangalie reference kwamba reference inaonesha kwamba uwezo wa makusanyo yetu ni mdogo sana, kwa hivyo tusisogee mbele wakati pale tulipokisia mwanzo hatukupafika, nashauri kwamba tungerudi nyuma tukaweka makisio ya makusanyo ambayo tunaweza kuyatekeleza. Kwa hali hii inaonesha kwamba mipango tunayoipanga yote inakuwa ni mipango hewa, Serikali tupangieni mipango inayotekelezeka msitupangie mipango ya kisiasa, sawa jamani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie na kifungu cha nne ambapo ni suala zima la asilimia 10 ya vijana na wanawake. Naomba nimalize kwamba kwenye asilimia 10 hii ya vijana na wanawake mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, inaonesha kwamba takribani halmashauri nyingi zinakuja na bajeti yao kwamba 10 percent ya wanawake na vijana ni kwa mfano makusanyo ni bilioni 50, inawekwa ten percent kwamba ni pengine 25 millions lakini ukiangalia kilichotumiwa ni milioni 5,000,000! Sasa ukiuliza hiki chingine kiko wapi?
Mheshimiwa Spika, Kila Mkuu wa Mkoa anayekuja ukimuuliza hichi chingine kimepelekwa wapi, hakuna majibu. Kwa hiyo, ningeshauri kwamba asilimia 10 hii ya vijana na wanawake itolewe katika hali inayostahiki kwa sababu katika kupitia kwetu kwenye Halmashauri tumekuta kwamba asilimia 10 hii inatumika vizuri sana kwa vijana na wanawake na inatuondolea lile tatizo la ajira. Nashauri kwamba Wizara husika waisimamie katika hali ya asilimia mia moja ili itekelezwe kama inavyopasa.
Mheshimiwa Spika, namalizia na ushauri mwingine kidogo.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, siungi mkono hoja.