Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. CHACHA R. MARWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nami nisome Mithali 29:1-2, halafu nitaendelea, inasema: “Aonywae mara nyingi akishupaza shingo atavunjika ghafla wala hapati dawa. Wenye haki wakiwa na amri watu hufurahi, bali muovu atawalapo watu huugua.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ni mbaya. Ukienda mtaani hamna hela, mimi sijui kwenye majimbo yenu, lakini mimi kwa Serengeti hela hakuna, wamepeleka wapi hela? Mheshimiwa Dkt. Mpango amepeleka wapi hela? Yaani hela hamna, hivi nini kimetokea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri, wala mimi siwezi kumlaumu Rais Magufuli, wala siwezi kuilaumu CCM; maana angalia kwenye kilimo; ukisoma ukurasa wa 15 ile namba tatu inasema sekta ya kilimo inayojumuisha mazao, mifugo na uvuvi ambayo inaajiri asilimia 66 ya Watanzania inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa. Inaendelea kukua kwa kasi ndogo ya wastani wa 3%, nani kasababisha ikue kwa asilimia ndogo?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpango ameandika yeye, aliyesababisha kasi ya ukuaji wa kilimo ikue kwa 3% ni nani? Ni yeye kwa sababu gani? Njoo kwenye bajeti, kwenye kilimo mwaka 2016/2017, walitengewa bilioni 100.5 wakapewa bilioni mbili, asilimia mbili aliyesababisha sekta ya kilimo isikue ni nani, ni yeye ambaye hakupeleka fedha. Mwaka 2017/2018, ilitengewa bilioni 150, akapeleka bilioni 16, sawa na asilimia 11, nani kaua sekta ya kilimo, ni yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Mifugo mwaka 2016/2017, ilitengewa bilioni nne, akapeleka 150 milioni yaani ni sawa na Landcruiser moja, sawa na 3%, nani kaua hii sekta ni yeye. Mwaka 2017/2018, mwaka huu wa fedha tulionao tulitenga sisi Bunge bilioni nne, amepeleka shilingi ngapi, sifuri. Nani kaua sekta ya kilimo na uvuvi na mifugo ambayo inaajiri 66% ya Watanzania? Ni yeye Mheshimiwa Dkt. Mpango na huyo Mheshimiwa ambaye wamekaa naye hapo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tusitafute mchawi kwamba kwa nini hela haiko mtaani, hela haiko mtaani kwa sababu hatujawekeza kwenye kilimo, mifugo na uvuvi. Kama tunataka hela iwe mtaani tupeleke pesa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo wanasema viwanda; kama kuna viwanda ambavyo tungewekeza vikaisaidia nchi cha kwanza ni Kiwanda cha Mbolea. Hebu aniambie Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuna viwanda vingapi vya mbolea? Kila leo tuna-import mbolea kwa ajili ya nchi yetu, tunatumia pesa nyingi za kigeni kwenda kununua mbolea nje, pesa ambazo zingefanya mambo mengine. Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko hapa, kwa nini Tanzania tusijenge kiwanda cha mbolea? Nini tunashindwa? Yaani kama kweli kiwanda tu cha mbolea cha kuwasaidia wakulima wetu tunashindwa sasa tunaongelea viwanda, viwanda gani? Maana kama kuna kiwanda cha kujenga ni cha mbolea.

Mheshimiwa Spika, maana tukisema tuna viwanda, viwanda gani? Kama mbolea hakuna una-import kila kitu unategemea nini? Kwa hiyo, haya mambo yanauma sana, hebu tusaidie wakulima wa Tanzania. Tuache mambo ya vyama, mimi ni CHADEMA lakini ninachoangalia hapa Utanzania wetu kwanza. Kule mtaani hamna hela, Mheshimiwa Jenista kuna hela kule? Hamna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hebu niambieni.

Mheshimiwa Spika, ahsante. Mazao ya biashara; hivi katika mazao ya biashara ya nchi hii ni mangapi, tumbaku iko wapi? Serengeti tulikuwa
tunalima tumbaku, pale Serengeti tumbaku ilikuwa inaleta bilioni kumi na sita mpaka bilioni ishirini. Wananchi unakuta bilioni kumi na sita ikimwagika kwenye ile wilaya, wilaya inachangamka. Sasa hivi Alliance One kampuni pekee iliyokuwa inafanya biashara ya tumbaku imeondoka. Unategemea hela itakuwepo, mzunguko wa hela utakuwepo, hakuna.

T A A R I F A . . .

MHE. CHACHA R. MARWA: Yuko sawa, si kwamba Watanzania wanashindwa kuzalisha tumbaku, wamezalisha nyingi imekosa soko, yuko sawa. Watanzania wamezalisha nyingi imekosa soko, nani alaumiwe? Wamevuruga wenyewe makampuni ya kununua. Watanzania wako tayari kulima tumbaku, kule Serengeti wamehama na maeneo mengine Songea huko walikuwa wanalima tumbaku, maeneo mengine wamevuruga. Nenda pamba, Mheshimiwa Waziri Mkuu namshukuru sana. Hebu tumpigie makofi Waziri Mkuu kafanya kazi kubwa. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. CHACHA R. MARWA: Mheshimiwa Spika, Serengeti wanalima tumbaku. Duniani yako makampuni manne yanayonunua tumbaku na Tanzania yako manne. Kwa hiyo, nadhani sijui anaongea nini, Watanzania hawajashindwa kuzalisha tumbaku, wanazalisha kwa wingi hata Serengeti ipo mpaka leo, imeshindwa kununuliwa.

Mheshimiwa Spika, pamba Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi nzuri, ndiyo maana nikasema tumpigie makofi amefufua zao la pamba, tatizo soko. Mpaka leo ninavyoongea Serengeti hakieleweki, wananchi wamekaa na pamba yao hawajui nini cha kufanya. Mheshimiwa Waziri Mkuu aangalie hawa wataalam wa Wakuu wa Mikoa sijui watu gani wanawadanganya. Ukienda kwa wananchi, mimi Mbunge wao napigiwa simu na si mimi peke yangu, Wabunge wengi wanaotoka kanda ya ziwa wanasumbuliwa na wananchi wao kuhusu ununuzi wa pamba, ni tatizo.

Mheshimiwa Spika, alizeti; mimi nimshukuru Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango huyu, wamepandisha ile kodi ya ku-import mafuta safi ili tuzalishe alizeti kwa wingi tuwe na viwanda vyetu. Hata hivyo, Mheshimiwa Dkt Mpango nikitaka kujenga kiwanda cha kuchakata alizeti kodi kwenye zile mashine ninazo-import si aondoe.

Mheshimiwa Spika, mimi siyo Mwanauchumi lakini ili u-import kuna VAT 18%. Sijui kuna import duty, sijui kuna nini, si waondoe. Kama kweli wanataka tujenge uchumi wa viwanda waondoe kodi kwenye mashine ambazo tuna- import kwa ajili ya viwanda, kama Ghana walivyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna issue ya corporate tax sijui na nini, naomba nihame hapo niongelee mambo ya wakandarasi. Wakandarasi sasa hivi wa Kitanzania wana hali ngumu, sijawahi kuona. Wakandarasi wana hali ngumu, ndiyo hiyo naomba kwenye wale wanaofanya mambo ya ujenzi, vifaa hivi vya ujenzi wanavyo-import, wapunguze kodi. Tutengeneze wazawa ambao watafanya miradi yetu wenyewe. Tunao vijana wazuri wenye makampuni lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, sijui niseme nini hali ni mbaya kweli kweli, naomba tuwasaidie Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nakupenda sana, nikwambie na ukisimama vizuri hawa jamaa watanyooka hapa, nchi itaenda vizuri, simama, mimi nakuunga mkono. Ahsante.