Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kidogo kwenye Wizara ya Mipango na Fedha kwa maana ya bajeti nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa namna anavyofanya kazi, nimpongeze pia Naibu Waziri namna wanavyofanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba Watanzania mipango ya fedha na mipango mingine inaenda vizuri; niwapongeze wanakwenda vizuri. Nimwombe Mwenyezi Mungu aendelee kuwajalia afya njema ili wasikate tamaa wasirudi nyuma, waweze kwenda mbele na kutusaidia kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi hii zinawekwa vizuri na hatimaye zinagawanywa vizuri kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, nianze kusema kwamba wananchi Watanzania walio wengi wamejiajiri kwenye shughuli za kilimo, takribani asilimia 65.5 wanajihusisha na kilimo. Kwa hiyo tafsiri yake ni kwamba uchumi pengine wa nchi ya Tanzania unategemea sana kilimo. Kwa hiyo ni lazima tujikite tuhakikishe kwamba tunaboresha sekta ya kilimo ili tuweze kupata pato la Taifa na liweze kukua kutokana na shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Spika, shughuli za kilimo haziwezi kukua kama hatujaweka miundombinu mizuri wezeshi; na moja ya miundombinu wezeshi mizuri ambayo inaweza ikasababisha kilimo kiweze kukua na hatimaye pato la Taifa liweze kukua ni barabara. Sote tunatambua kwamba kilimo kinafanyika maeneo ya vijijini na huko ndiko wakulima wetu waliko, wanazalisha kwa kiasi kikubwa, lakini changamoto kubwa imekuwa ni barabara. Imekuwa hawawezi kufikisha mazao kwa wakati, mazao hayawezi kufikia soko kwa wakati na hata yakifika yanakuwa tayari yameshapoteza ule ubora wake.

Mheshimiwa Spika, juzi wiki iliyopita tulikuwa kwenye mkoa wetu, Mkoa wa Njombe na Kamati ya Kilimo. Kamati ilijionea yenyewe namna jinsi wakulima wetu wanavyopoteza fedha nyingi, rasilimali nyingi kutokana na changamoto kubwa sana ya barabara. Njombe tunazalisha mazao mengi; tunazalisha chai, tunazalisha matunda, tunazalisha mbao, tunazalisha kila aina ya mazao ambayo yanazalishwa hapa nchini, lakini changamoto kubwa ukiangalia mazao yote kwa ujumla wake kwa hali ya hewa ya Njombe ni hali ya mvua. Kwa hiyo yamekuwa yakiathiriwa sana na barabara zetu ambazo si nzuri sana, kwamba hazipitiki wakati wa kifuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme juu ya zao mojawapo zao la Parachichi. Zao la parachichi katika nchi hii linalozalishwa Njombe ni la tofauti sana. Ni wakati ambapo Njombe peke yake inazalisha hili zao, maeneo mengine duniani kunakuwa hakuna uzalishaji wa parachichi. Sote tunajua matumizi makubwa ya parachichi katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta, mafuta ya nywele, dawa mbalimbali, lakini ukiangalia miundombinu ambako hili zao linazalishwa ni mibovu sana.

Mheshimiwa Spika, niombe kwenye upande hasa wa barabara, tukiangalia barabara zetu hasa kwa mfano, kwenye jimbo langu Jimbo la Lupembe, barabara ya kutoka Kibena kwenda Lupembe mpaka Madeke ambako huko kuna uzalishaji mkubwa sana wa parachichi, barabara hii imekuwa haipitiki wakati wa kifuku.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili tumepitisha bajeti mara kadhaa, tumepitisha bajeti ya mwaka 2016/2017, tumepitisha tumeweka fedha. Tumepitisha bajeti ya mwaka 2017/2018 na hata mwaka huu 2018/2019, tumeweka fedha pale. Fedha hizi zimekuwa hazitoki, kwa hiyo kimsingi tunapoteza fedha nyingi kwa kuacha yale mazao yaliyopo kule vijijini yasiweze kutoka kwenda kwenye lami, kwenda kwenye soko kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango lakini pia niombe kwa Serikali yetu kwa ujumla, niombe kwenye bajeti hii ya mwaka huu tujitahidi basi barabara ya Lupembe kwa maana ya Kibena – Lupembe- Madeke na kuunganisha kwenda Morogoro iweze kupewa fedha ianze kujengwa kwa kiwango cha lami ili mazao haya niliyotaja kama chai na parachichi yaweze kusafirishwa kirahisi zaidi na yaweze kufikia soko.

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa tukizalisha kwa wingi, tukiweka barabara zikawa zinapitika kipindi chote cha mwaka mazao kama chai, parachichi kama nilivyosema, mbao na nguzo za umeme zitaweza kupitishwa kwenye barabara hii na hatimaye tutaokoa fedha nyingi sana ambazo tumekuwa tukipoteza wakati wa mvua kutokana na ukosefu wa barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Mpango kwa kushirikiana na Serikali nzima na Wizara zote tuhakikishe hii barabara inatengenezwa kwa kiwango cha lami na barabara nyingine zilizopo katika Mkoa wa Njombe ambako kama nilivyosema kuna uzalishaji mkubwa sana wa parachichi ambazo zinazalishwa Njombe tu.

Mheshimiwa Spika, katika dunia nzima kuna msimu ambako Njombe tu zinapatikana na wafanyabiashara wote duniani wanakuja kununua parachichi Njombe ili ziweze kwenda kwenye masoko hayo na tuweze kupata mabilioni ya fedha mengi na hatimaye kukuza pato la Taifa, tuhakikishe kwamba barabara hizi zinatengenezwa kwa kiwango ili ziweze kutumika wakati wa kifuku.

Mheshimiwa Spika, pia niseme jambo moja juu ya risiti za EFD hasa kwa wazalishaji wa mazao ya misitu hasa mbao. Kumekuwa kuna tatizo Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa wakulima wangu wa Lupembe wanaozalisha mbao. Zinapokwenda sokoni njiani wanakutana na kikwazo kwamba ni lazima aliyeuza hiyo miti, aliyezalisha hiyo mbao lazima awe ana risiti ya EFD. Sasa mkulima ameuza miti yake ameuza heka mbili, heka tatu, heka tano tu unamwambia awe na risiti ya EFD na anauza pengine kwa miaka 15 mara moja tu; sasa hii mashine ya EFD atapata wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya Fedha wajaribu kuliangalia jambo hili hasa la EFD mashine kwenye mbao zinazotokana na wakulima wa misitu, hasa wakulima wa misitu ya mbao. Kwa hiyo niombe tuliangalie vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia nataka niseme kidogo juu ya jambo moja la vifungashio. Tulipita na Kamati ya Kilimo na Uvuvi, kuna maeneo ambako tayari kuna wafanyabiashara wananunua mazao haya, kama nilivyosema matunda na mazao mengine kama njegere na mazao mengine. Wanatumia vifungashio kutoka Kenya na pale nje wanaandika Made in Kenya. Kwa hiyo, inaonekana kwamba zao lile au njegere hizo au parachichi hizo zimezalishwa Kenya wakati zimezalishwa Lupembe au zimezalishwa pale Njombe. Kwa hiyo niombe wajaribu kudhibiti hasa hawa wanaochukua mazao yetu haya wafungashie vifungashio ambavyo vitaandikwa kwamba hilo zao au hiyo bidhaa aliyozalisha imezalishwa sehemu fulani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo itajwe sehemu ambako bidhaa hiyo imezalishwa, lakini siyo itajwe eneo lingine kwa mfano wanaandika Made in Kenya na mwisho wa siku inaonekana Kenya ndiyo inayozalisha hayo mazao kumbe tunazalisha hapa Tanzania, tunazalisha Njombe. Kwa hiyo niombe wajaribu kufuatilia hili na kulidhibiti kwenye upande wa vifungashio ili vioneshe sehemu ambako zao hili limezalishwa na hasa kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niseme juu ya kodi ya mapato hasa kwa wazee wastaafu ambao wamefungua vibiashara vidogo vidogo. Wazee hawa wamekuwa wakipata zile pensheni zao wanafungua biashara ndogo, anakuwa na biashara ya milioni tatu, nne, tano halafu tunakwenda kuwadai kodi. Hebu tuangalie hawa wazee wamefanya kazi miaka mingi sana, wametusaidia sana, tuangalie kama biashara ndogo hizi angalau tuwaachie ili waweze kujiwezesha waweze kujikwamua kwenye maisha yao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru sana, naamini Wizara itayachukulia kimakini haya mambo na niunge mkono hoja kwa asilimia mia hoja hii iliyopo mbele yetu. Ahsante sana.