Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shaurimoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri ambazo anazifanya pamoja na Naibu Waziri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ambayo inakwenda katika uchumi wa viwanda; na ili tujenge viwanda, viendelee na viweze kufanya kazi kama nchi nyingine ambazo zimeshaendelea lazima tuimarishe uchumi wa nchi yetu na ni lazima tusimamie kilimo. Viwanda vyetu ili viweze kufanya kazi kwa hali nzuri lazima Serikali yetu iweze kuangalia sekta ya kilimo. Bila kuangalia sekta ya kilimo tutakuwa tunaimba viwanda lakini hatujafika mahali ambapo tunapataka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia sekta ya kilimo bado Serikali yetu haijaweka mkakati rasmi wa kushughulikia tatizo la kilimo. Ukiangalia bajeti ya kilimo bado ni ndogo na vile vile na upelekeaji wa pesa katika sekta ya kilimo bado ni mdogo sana na sisi tunahitaji kwenda katika uchumi wa viwanda kwa nguvu zote. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, jitahidi sana fanya kazi kuhakikisha sekta ya kilimo ndiyo sekta mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, ikiwa hatujaitizama kwa makini sekta ya kilimo basi hata hili suala la ajira kwa vijana wetu wa Tanzania bado haitofikia mahali pazuri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aiangalie sekta ya kilimo, ndiyo sekta mama katika nchi yetu, ndiyo sekta ambayo itatutoa hapa tulipo na kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kusikiliza hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi tulikuwa Njombe, tulipata tabu sana; kuna kelele sana za wakulima wanakosa mikopo. Sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie; wakulima wetu bado wanakosa mikopo katika benki. Sasa wataweza kufanya kazi vipi na mahali pa kupata pesa ili waweze kuimarisha kilimo pasipo na Serikali ni lazima waweze kupata mikopo ndani ya benki zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, benki zimekuwa sugu katika kutoa mikopo kwa wakulima wetu, tumepata kelele nyingi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kusimamia kwa makini utoaji wa mikopo kwa wakulima wetu. Wakulima wetu ukiwapa mikopo na ukisimamia vizuri ukiwapelekea watalaam vizuri tutatoka hapa tulipo na tutakwenda mahali pengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la maji. Hili bado ni tatizo; bajeti ya maji 2017/2018 ilipangwa kuwa takriban bilioni mia sita, zilizotoka ni bilioni mia mbili tu. Tulijadiliana na sisi kama Wabunge tumesema iongezwe Sh.50 kusaidia bajeti hii kuhakikisha wananchi wetu wanapata maji ya kutosha. Kama hatutaongeza Sh.50 tutakuwa hatufiki mahali pale ambapo tuliahidi Watanzania wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi ni Wabunge ambao tumekuja hapa kwa sababu ya kuwasemea wananchi wetu, tukiishauri Serikali tumwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kupokea mawazo yetu katika kuongeza Sh.50. Ukiangalia idadi ya bajeti hii, tukienda katika system ili tuweze kupata maji safi wananchi wetu wapate maji, tutachelewa kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulipokea, kuongeza Sh.50 katika lita ya dizeli na petroli ili tuweze kupata maji safi kwa sababu ukiongeza hakuna tatizo, mimi sijaona tatizo la kukosa kuongeza hili. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulichukua suala la ongezeko hili la Sh.50 kwenye lita ya petoli na dizeli ili tuweze kufika mahali tunapopataka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi wa bahari kuu bado ni tatizo, bado Serikali haijakaa katika kulisimamia, kuweka mikakati rasmi ili kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu unakwenda kwa kasi sana. Mahali hapa penye uvuvi wa bahari kuu tukipasimamia kikweli kweli kama Serikali, tukiamua kwenda kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu, nchi yetu itaweza kwenda mbele. Uvuvi wa bahari kuu unaweza kuchangia mapato mengi sana na sasa tunakosa mapato makubwa sana kupitia uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila tukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha hatujaona kipengele ambacho watasema sasa tutajenga bandari, kununua meli za uvuvi na kufanya tathmini ya samaki ndani ya bahari yetu ambayo tunayo; tuna uwezo gani na tuna samaki kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tukikaa tukisimamia suala la uvuvi, tukiweza kuwezesha hii sekta ya uvuvi kwa makini, tunaweza kufika mahali ambapo nchi yetu inapataka. Huu uvuvi tukiweza kusimamia kwa makini basi unaweza kuingiza Pato la Taifa kuliko hata hii sekta ya madini. Niiombe Serikali iweze kusimamia kwa makini kuhakikisha suala la uvuvi wa bahari kuu linatazamwa kwa jicho la huruma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunao Waheshimiwa Mawaziri wetu wa Wizara ya Uvuvi wako vizuri, wanafanya kazi vizuri na wanashaurika vizuri, basi niombe sana Serikali iweze kuita•izama kuhakikisha kwamba uvuvi huu unakwenda mbio kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya kazi. Uvuvi wa bahari kuu una uwezo wa kutengeneza ajira kubwa sana kutoka kwa wananchi wetu, ni kwa nini tusiweze kusimamia uvuvi wa bahari kuu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ndiyo hili la sekta ya uvuvi ambayo tuliiangalia kwa makini, tukiweza kujua tuna kiasi gani cha samaki katika bahari kuu, tukiweza kujua tuna uwezo gani na tukiweza kununua meli yale mapato ambayo tunakosa kutoka katika bahari kuu, tukiweza kuyapata tunaweza kufika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la kupatikana kwa ajira kwa vijana, bado ajira kwa vijana upatikanaji wake upo duni sana. Niombe sana, Wizara ya Elimu ipo, tuanze kuwafundisha vijana wetu jinsi ya kujiajiri kutoka shule za msingi ili wakitoka pale wakimaliza chuo kikuu watakuwa wameweza kujiajiri wao wenyewe kuliko kukaa tu kuitegemea Serikali ili iweze kuwaajiri. Suala hili haliwezekani, hakuna Serikali ambayo inaweza kuajiri watu wake wote. Ni lazima kama Serikali tujipange tuhakikishe kwamba vijana wetu tunaanza kuwafundisha mafunzo ambayo hata wakimaliza basi wanaweza kujiajiri wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.